TUONDOE MITAZAMO HASI DHIDI YA WATU WENYE ULEMAVU
Na Mwandishi Wetu, Moshi
JAMII imetakiwa kuondokana na mitazamo potofu juu ya watu wenye ulemavu, kwamba kundi hilo haliwezi kujitegemea hata kama likiwezeshwa. Pamoja na hayo ujenzi wa sasa wa majengo ya huduma na miundombinu hayana budi kuzingatia kundi la walemavu ili kulijali kundi hili.
Rai hiyo imetolewa na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVAWATA) mkoani Kilimanjaro, wakati wa mafunzo ya kuvijengea uwezo vyama vya watu wenye ulemavu Manispaa ya Moshi, ambapo yalijadiliwa mambo anuai ikiwemo vikwazo na mitazamo hasi iliyojengeka juu ya watu wenye ulemavu.
Akizungumza Katibu wa Shirikisho hilo mkoani Kilimanjaro, Zacharia Masawe alisema walemavu wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mtazamo hasi, ambapo wamekuwa wakionekana kuwa ni watu ombaomba na watu wasioweza kufanya chochote jambo ambalo si sahihi.
Alisema mitazamo hiyo katika jamii imekuwa ikisababisha walemavu kudharaulika na kukosa haki zao za kimsingi ikiwemo elimu, ambapo hata wakati mwingine hukoseshwa haki ya msingi ya kuishi kwa kuuawa.
“Kumekuwepo na mitazamo hasi katika jamii kuhusiana na sisi watu wenye ulemavu, kwani katika jamii tumekuwa tukionekana kuwa sisi ni watu ombaomba na hata wakati mwingine unakuta unakwenda katika ofisi ya kiongozi ikiwemo za Serikali lakini unapotaka kumuona kiongozi huyo unashangaa unaletewa sh. 500 na kuambiwa uondoke kwakweli hii ni udhalilishaji na uonevu kwetu sisi,” alisema Masawe.
Masawe alisema ufike wakati sasa jamii ibadilike na iwaone walemavu kama watu wengine ambao wanahitaji kuthaminiwa, kuajiriwa na wasiwanyanyapae kwani hakuna mtu aliyezaliwa na kutaka kuwa mlemavu.
Kwa upande wake Rumisha Masam alisema walmavu wamekuwa wakikumbana na vikwazo mbalimbali ikiwemo miundombinu mingi kujengwa pasipokuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.
Alisema watu wenye ulemavu hasa wale wa viungo ambao wamekuwa wakitumia viti mwendo, wamekuwa wakishindwa kingia katika maeneo na ofisi mbalimbali kutokana na miundombonu kutozingatia mahitaji yao.
“Jamii kwa saa inapaswa kuthamini watu wenye ulemavu na kuondokana na ile dhana kuwa walemavu ni watu wa kusaidiwa na hawana msaada wowote kwa jamii na sasa ibadilike na iwathamini kwani walemavu ni watu kama watu wengine na wanaweza kufanya kazi endapo wataendelezwa lakini pia ihakikishe miundombunu yote inayojengwa inazingatia mahitaji yao,” alisema Rumisha.
Comments
Post a Comment