AJIRA MBAYA ZA WATOTO KUBONDA KOKOTO.

Kundi la watoto likiwa katika eneo hilo hatari kwa afya na ustawi wa elimu ya mtoto wa kitanzania, kwani hata akiwa darasani anawaza ajira hiyo.
Baadhi ya watoto wa kike wanaojishughulisha na ubondaji wa kokoto katika eneo la Zizi la Ng'ombe, Manispaa ya mji wa Iringa.
 Mama akiwa na watoto wake katika eneo la Zizi la Ng'ombe, hali hii licha ya kuchangia  ajira kwa watoto pia si ajira hiyo si salama kiafya kutokana na vumbi kali linalotokana na kugongwa kwa mawe kuwadhuru.
 Badhi ya watoto waliokutwa na mtandao huu, wakiwa wamejipumzisha, lakini wakiendelea na biashara ya kuuza ndizi.
 Watoto wakiendelea na ajira, ambayo ina madhara kwa siku za usoni, kwani baadhi yao hutoroka shule ili kujipatia ajira hizo

KWA miaka mingi haki za watoto zinakiukwa hasa katika suala la kuwaajiri chini ya umri wao, hili ni kosa kisheria, kwani baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wanasema pengine ni kutokana na watoto hao kutokuwa na uamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa na kama wanashirikishwa huwa ni kwa kiasi kidogo.

Kwa sababu hiyo katika jamii zetu wengine wanatumia nafasi hiyo kuwapa ajira ngumu watoto chini ya miaka 18, na hapa Iringa  inadhiririsha wazi katika eneo la Zizi laNgombe, ambapo kundi kubwa la watoto kuanzia miaka 5 wanapatiwa ajira na watu ambao sijui niseme hawana huruma, au huruma zao zimezidi kiwango.
Ni kweli yawezekana mtoto mwenyewe akaomba apatiwe kazi hiyo ili kupata kujikimu na mahitaji nyumbani, lakini kuna haja gani ya kumpa kazi hiyo hatarishi kama kweli ni huruma ili apate fedha??.
Huu ninaweza kuuita ubepari unaotokana na kipato cha mtoa ajira, kama huruma zimetoka rohoni basi hakuna haja ya kuwafanyisha kazi kwanza ndipo tuwalipe ujira, tuwasaidie kwa kuwapa fedha na kuwahimiza warudi darasani lengo likiwa ni kuwapunguzia kiwango cha miaka ya mateso, kwani wakisoma watajikomboa kwa kupata ajira halali zisizo hatarishi.
Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla elimu inahitajika kuelezea umuhimu wa haki za watoto hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania ambapo unyanyasaji wa watoto unaonekana ni jambo la kawaida.

Kwani kwa mujhibu wa sheria na haki za watoto, kuna ajenda muhimu 10 zilizoainishwa katika kulinda haki hizo, ajenda hizo ni Kuwekeza katika kuokoa maisha ya watoto na wanawake, lishe bora, huduma bora za maji na usafi wa mazingira hasa vyoo shuleni na kwenye vituo vya afya.

Ajenda nyingine ni kuwekeza katika kumwendeleza mtoto mdogo, kwa kumpatia elimu bora, shule kuwa mahali salama, kuwalinda watoto wachanga na wasichana dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Nyingine zilizoainishwa ni pamoja na kupunguza mimba za utotoni, kuwekeza katika kuwanusuru watoto na vitendo vya vurugu, udhalilishaji na unyonyaji, kwani watoto wengi wananyonywa kwa kutumikishwa katika ajira zenye ujira mdogo.
Utafiti unaonyesha kwamba watoto walio wengi wanajua haki zao lakini tatizo ni kukosa sauti kutokana na mfumo wa maisha yetu ya kuheshimu wakubwa ndio maana hivi karibuni kupitia baraza la watoto, waliamua kukutana na Rais Jakaya Kikwete kumweleza umuhimu wa kutekelezewa ajenda zinazowahusu.
 
Katika harakati hizo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 baadhi ya mashirika yanayohusika na haki za watoto likiwamo UNICEF walikutana na baadhi ya wagombea katika kujadiliana nao hasa kubeba ajenda ya watoto kuwemo katika ilani zao ili kutekeleza haki za watoto katika sekta mbalimbali.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU