CHANGAMOTO KATIKA KUFUNDISHA WATOTO WALEMAVU

                                  Baadhi ya wanafunzi wasioona
Na mdau Fred Azzah
NI nadra kwa  watu wengi kuchagua kufanya kazi ngumu tena wakijua haina maslahi mazuri. Kwa wanaojitokeza kuchagua kazi za aina hii, nawaita watu majasiri wakiwamo walimu wa elimu maalum ambao licha ya kujua kwamba kufundisha watoto wenye ulemavu  ni kibarua kigumu, bado wanatekeleza majukumu yao kwa moyo mkunjufu.

Mmoja wa majasiri hawa ni mwalimu Andrew Koti wa kitengo cha wanafunzi wasiosikia na  wasioona katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko ya jijini Dar es Salaam,  anayesema inahitaji uvumilivu mkubwa na wito kuwafundisha walemavu wa aina hiyo.

Hawa watoto huwa wanakuja hapa hawajui kufanya kitu chochote, inabidi mwalimu uanze kuwafundisha jinsi ya kula, kwenda chooni, kutembea na vitu vingine kama hivyo.  Mara nyingi  watoto hawa huwa  ni wale wanaofungiwa ndani hawajui kufanya chochote, anasema Koti na kuongeza:
Wengi huwa wanatupiwa chakula tu, hawajui hata kula kwa kutumia mikono, wanakula moja kwa moja na mdomo. Wakija huku tunaanza kuwafundisha jinsi ya kula na vitu vingine kama hivyo, baada ya mwaka mmoja ndiyo unaanza kumfundisha mambo ya taaluma.

Tofauti na wanafunzi walemavu wengine, mwalimu Koti anasema walimu wanaowafundisha wanafunzi wasiosikia na kuona wana changamoto nyingi hasa katika nchi  masikini ikiwamo Tanzania.
Mojawapo ya changamoto anazotaja ni pamoja na ukosefu wa vifaa ambavyo hata vikipatikana huuzwa kwa bei ghali.

Wakati mtoto wa kawaida akitumia Sh100 tu kununua kalamu, hawa wenye ulemavu kalamu yao ambayo ni mashine ya nukta nundu, moja inauzwa Sh1.5 milioni. Mashine za kutoa photocopy (kudurufu) zinauzwa kuanzia Sh16 milioni,   bunda moja la karatasi maalumu wanazotumia ni Sh 30,000 wakati hizi za kawaida ni Sh 6,000, anafafanua.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU