"JENGENI MOYO WA HURUMA, UPENDO NA UVUMILIVU KWA WATOTO WENYE ULEMAVU"!




Kituo cha Watoto Walemavu cha Siuyu, Jimbo Katoliki Singida, kilizinduliwa rasmi na Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Singida, kunako tarehe 20 Februari, 2007. Kituo hiki kinahudumiwa na muungano wa Shirika la Wamissionari wa Pallotini pamoja na Watawa wa Pallotini pamoja na waamini walei, wanaopenda kumwilisha karama ya Mtakatifu Vincenti wa Palloti katika maisha yao ya Kikristo.  
Wamissionari hawa wanashirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba, watoto wenye ulemavu wanaonjeshwa kwa namna ya pekee, ile Injili ya Upendo kutoka kwa Kristo mwenyewe. Wengi wa wafanyakazi katika kituo hiki ni watu wa kujitolea, lakini walau kila mwezi, wanapata ruzuku kidogo kama alama ya shukrani kwa mchango wao kituoni hapo. Jumla ya Euro 90,000 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki, mchango kutoka kwa Wasamaria wema. Vatican kwa upande wake, imechangia kiasi cha Dolla za Kimarekani 15, 000.

Kituo cha walemavu Siuyu, Jimbo Katoliki Singida, kinaendeshwa kwa asilimia kubwa kwa kutegemea misaada kutoka ndani na nje ya Tanzania. Kwa mwaka huu, anasema Mheshimiwa Padre Tommy Ryan, SCA, kwamba, Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu limewapatia kiasi cha Dolla za Kimarekani 10,000. Anasema, Serikali ya Tanzania imeahidi kukisaidia Kituo hiki, lakini bado wanasubiri kuona ahadi hii ikitekelezwa kikamilifu. Wazazi na walezi wenye watoto wao katika Kituo cha Watoto wenye Ulemavu cha Siuyu, wanachangia, kila inapowezekana mazao ya chakula kwa ajili ya hifadhi na matunzo ya watoto wao.

Kwa mwaka 2011, Kituo kina jumla ya watoto walemavu sabini na saba na kati yao sabini na nne, wanaishi kituoni hapo. Baadhi yao wanahudhuria masomo ya shule ya msingi kwenye shule jirani na kwa namna ya pekee, wanapata uangalizi maalum kutoka kwa waalimu wao, kwani watoto sitini na tisa wanamtindio wa ubongo.

Kukaa pamoja na kujifunza na watoto wengine wasiokuwa na ulemavu anasema Padre Tommy Ryan, ambaye tangu mwaka 1985 amekuwa akiishi na kufanya utume wake nchini Tanzania, ni jambo la maana sana, kwani linawasaidia kuondokana na ubaguzi unaoweza kujitokeza ndani ya jamii kutokana na ulemavu wao. Kuna vituo vichache sana nchini Tanzania vinavyojikita kwa ajili ya huduma kwa watoto wenye ulemavu navyo vinapatikana: Dodoma na Ifakara. Ikumbukwe kwamba, watoto hawa wanapaswa kupata huduma hii kutoka katika Jamii, kumbe ni jukumu la Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, ili kutambua na kuthamini haki msingi za watoto walemavu ndani ya jamii.

Padre Tommy Ryan anasema, umefika wakati kwa wazazi na walezi wenye watoto walemavu kuondokana na mawazo na imani potofu zinazowapekea kuwaficha majumbani mwao, bali waweze kupata mwamko wa kuwatafutia fursa za elimu kwa ajili ya maendeleo yao kwa siku za usoni.

Kituo cha Watoto Walemavu Siuyu kina endelea kumwandaa Sista Rose Ombay, kama mtaalam wa viungo, ili atakapohitimu masomo yake, aweze kuwasaidia watoto wenye ulemavu kufanya mazoezi kituoni hapo, akishirikiana na kundi la akina mama wengine wanaoendelea kujitolea. Kituo kinaendelea kujikita katika kujitegemea, ili kuwa na uhakika na usalama wa maisha ya watoto walemavu kwa siku za usoni. Kituo kina mashine mbili za kukamua mafuta ya alzeti, mashini moja ya kusaga nafaka.

Kuna vyumba saba ambavyo vinakodishwa kwa ajili ya matumizi mbali mbali. Kituo kinatarajia kujenga nyumba kwa ajili ya kukodisha pamoja na kujenga ukumbi, ikiwa kama hali ya uchumi itaruhusu. Miradi yote hii, inachangia kwa asilimia sabini na tano ya matumizi ya Kituo cha Watoto Walemavu Siuyu, kilichoko Jimbo Katoliki Singida. Anawashukuru Wasamaria wema wanaoendelea kuchangia kwa hali na mali kwa ajili ya Kituo cha Watoto Walemavu Siuyu Singida na sehemu mbali mbali za Tanzania. Anawakumbusha wananchi kwamba, wanapaswa kujenga ndani mwao moyo wa huruma, upendo na uvumilivu kwa walemavu.

Mheshimiwa Padre Tommy Ryan anasema, hawa pia ni watoto wapendwa wa Mungu, hata ikiwa kama wakati mwingine wanasahauliwa katika kutekelezewa mahitaji na haki zao msingi ndani ya jamii, lakini, kwa Mwenyezi Mungu wanaupendeleo wa pekee, kama alivyoonesha Yesu Kristo mwenyewe enzi ya utume wake hapa duniani.




 

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU