MTOTO ANUSURIKA KUUAWA... WAZAZI HAKUNA MTOTO ANAYEPENDA KUZALIWA AKIWA MLEMAVU.....

BAADHI YA WATU WAMEKUWA NA MITAZAMO HASI DHIDI YA WATOTO WANAOZALIWA NA ULEMAVU WA AINA MBALIMBALI, NA HICHA NI CHANZO CHA NDOA NYINGI KUVUNJIKA, HAKUNA MTOTO ANAYEPENDA KUZALIWA MLEMAVU, WALA MAMA ANAYEPENDA KUJIFUNGUA MTOTO MLEMAVU ILA YOTE NI MIPANGO YA MUNGU WETU AMBAYE NDIYE MUUMBAJI, SIO MKOSI WALA LAANA KUZAA MTOTO MLEMAVU...

Mkazi  wa Kawe, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam,  Betty Mwani (25) amewaomba Watanzania na mashirika  yasiyo ya kiserikali kumsaidia  mahitaji  mbalimbali mwanaye Saraphina Huruma Msaka (7) (pichani) ambaye ni mlemavu aliyenusurika kuuawa.

Akizungumza hivi karibuni nyumbani  kwa dada yake, Kawe anakoishi, Mwani alisema kwamba mwanaye alitaka kuuawa kijijini kwao kutokana na imani za baadhi ya watu kuwa katika ukoo wao mtoto kuzaliwa na ulemavu ni mkosi.

Hata hivyo, Mwami alisema aliweza kuondoka na kuja jijini ambako mtoto wake anakabiliwa na matatizo mengi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa baiskeli ya magurudumu matatu , nguo na kusomeshwa kwani  tayari ameshafikisha umri wa kuanza kusoma.
“Sijui nimpeleke shule gani, nimekuwa naishi kwa ndugu mbalimbali baada ya mwanaume niliyezaanaye kumkataa nikiwa nafanya kazi za ndani Bagamoyo,” alisema Mwani.

Aliongeza kudai kuwa  baadhi ya watu anaoishinao wamekuwa wakimbagua mtoto huyo na wengine kumzushia makosa asiyoyafanya ili mradi atafute  mahali pa kuishi.

Akielezea historia yake, Mwami alisema mara baada ya kumaliza elimu ya msingi kijijini kwao Ihomasa,  Wilaya ya Mfindi  mkoani Iringa mwaka 2002, alichaguliwa kujiunga na  kidato cha kwanza  katika Shule ya Sekondari Itengule lakini hakuweza kwenda kutokana mama yake kukosa fedha za maandalizi kwani baba yake alikwisha fariki mwaka 1994.

 Alisema  kilichomuuma zaidi  ni pale alipowaona wanafunzi wenzake aliofaulu nao  wakiendelea na masomo  lakini yeye alibaki  kijijini jambo lililomsononesha sana hivyo akashawishika  kwenda Bagamoyo mkoani Pwani kufanya kazi za ndani  kwa mama mmoja ambapo alikaa huko  kwa muda wa mwaka  moja na nusu.

Mwani alisema akiwa Bagamoyo, ndugu wa bosi wake waliyekuwa wakiishi nyumba moja alimrubuni  wakaanzisha uhusiano wa kimapenzi uliosababisha kupata ujauzito.

Aliongeza kuwa, alipomfahamisha kuhusu hali aliyokuwanayo, alimsihi asimwambie mtu na kumweleza alikuwa akitafuta chumba ili waishi pamoja.

“Baada ya kujifungua  mtoto Saraphina akiwa hana baadhi ya viungo vya mwili, huyo kijana alibadilika na kuniambia  mimba haikuwa yake kwani katika ukoo wake hawana watu kama mtoto wangu,” alisema Mwani huku akibubujikwa na machozi.
Aidha, alidai kuwa kufuatia kuzaa mtoto mlemavu watu aliokuwa akiishi nao hawakuwa na mapenzi tena kwani waliona kuishi na Saraphina ulikuwa mzigo.

Dada huyo aliongeza kuwa, bosi wake alimpeleka kijijini kwao Iringa ambapo baadhi ya watu walimshangaa mtoto wake mlemavu.

“Niliumia sana lakini baada ya  siku mbili watu walianza kuja nyumbani, baadhi wakiwa wamebeba zawadi za sabuni lakini  lengo lao lilikuwa ni kutaka kumuona Saraphina kwani waliambiwa jinsi alivyolemaa  huku wengine wakisema ni mkosi kumpeleka mtoto  kama huyo katika ukoo wao,  hivyo itafutwe njia atoweke duniani,” alisema Mwani kwa huzuni.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU