HIZI NDIZO GHARAMA NA ADHA ZA KUZALIWA MLEMAVU TANZANIA

Mtoto Alewis akiwa na mama yake Roswita Mhagama katika ofisi za Mwananchi. Picha na Daria Erasto  
Na Daria Erasto, Mwananchi
 
Ni jambo la kawaida siku hizi kusikia habari kuwa baba amemkataa mtoto wake  kwa sababu tu amezaliwa na ulemavu uwe wa viungo au hata akili.
Katika toleo la gazeti hili, Jumamosi Juni 22  mwaka huu kulikuwa na habari ya Grace Joel aliyekimbiwa na mume wake kwa sababu ya kuzaa watoto mapacha wa kiume  walioungana  sehemu ya kiunoni na hivyo kutumia njia moja kujisaidia.
Grace aliiambia Mwananchi  kuwa amejikuta kwenye hali ya mateso na uchungu mwingi baada ya familia yake, hususan mume wake, Erick Mwakyusa kumtelekeza kwa kile alichodai kuwa hana haja na watoto walioungana.

Alisema Erick na  ndugu zake walimkataa kwa sababu katika ukoo wao haijawahi kuzaliwa mtu wa jinsi ile.
Ashukuriwe Mungu kwa msaada wa wauguzi na madaktari wa Hospitali ya Uyole, Hospitali ya Rufaaa Mbeya na Hospitali ya Taifa Muhimbili sasa watoto hao wamepata fursa ya kupelekwa India ili kufanyiwa upasuaji wa kutenganishwa.

Hali si tofauti kwa Alewis Mhagama (7), mlemavu wa viungo vya mikono na miguu anayetokea kijiji cha Mlimba, Ifakara Mkoani Morogoro. Ukimwangalia na kumsikiliza mtoto huyo utagundua kuwa ni mwerevu na mchangamfu wa hali ya juu.

Lakini, kwa undani Alewis anakabiliwa na upweke kwa kukosa mapenzi ya baba yake mzazi pamoja na ndugu za baba yake, kwani pamoja na kuishi kijiji kimoja, baba yake alimkataa mara baada ya  kuzaliwa.
 Kwa maelezo ya mama  mzazi wa Alewis,  Roswita Mhagama anasema mwanaye  alizaliwa na ulemavu wa viungo vya mikono  na miguu mwaka 2007 kijijini Mlimba.

Baada ya kuzaliwa baba Alewis alimkataa mtoto huyo na kumwita laana na mikosi katika familia.
Roswita anasema alifukuzwa na ndugu wa mwanaume huyo na kumwambia kuwa ana laana na dhambi  ndiyo maana amezaa mtoto anayefanana na chura. Anasema amemlea mtoto wake huyo kwa mateso makubwa,kwani kutokana na ulemavu alionao Alewis amekuwa tegemezi kwa mambo mengi hivyo hutumia muda wake mwingi na kumfanya ashindwe kufanya  kwa umakini shughuli zake za kilimo na upikaji pombe za kienyeji alizokuwa anafanya awali ili kujipatia kipato.

“Kwa kweli hali ya maisha yangu imebadilika tangu nipate mtoto huyu,pamoja na kwamba nimekosa usaidizi, lakini pia nakosa muda wa kufanya shughuli zangu zingine kwa sababu Alewis anakuwa anahitaji uangalizi muda wote,” anasema.

Anaongeza kuwa hali hiyo imefanya kipato cha familia yake kushuka zaidi, kwani tayari ana watoto wengine watatu ambao baba yao alifariki naye ndiye anayewasomesha. “Hivi ninavyoongea nawe, mwanangu anayefuatana na Alewis kuzaliwa ambaye yuko kidato cha tatu sasa alisimamishwa shule kutokana na kutolipa ada,” anaeleza.
Anasema kutokana na maisha duni aliyonayo ameshidwa kumpatia mwanae baiskeli ya miguu mitatu ili kumrahisishia katika kutembea, hivyo hulazimika kumbeba mgongoni kila anapotaka kwenda.

Maisha ya Alewis
Kwa sasa Alewis amefikisha umri wa kwenda shule na kutokana na kufundishwa na kaka yake nyumbani anajua kusoma  baadhi ya herufi na maneno kama mama, baba na dada.
Hata hivyo, kikwazo kikubwa kilichopo ni upatikanaji wa shule itakayomfaa kulingana na hali yake ya ulemavu.

Nilipomuuliza anataka kuwa nani Alewis alijibu kuwa  akiwa mkubwa anataka kuwa daktari na tayari anajua kusoma kwani kaka yake aliyemtaja kwa jina moja la Jumbe huwa anamfundisha akiwa nyumbani.
“Najua kusoma mimi, kaka Jumbe akitoka shule ananifundisha mama, baba, dada na kaka,” anasema Alewis.

Kwa upande wake, Roswita anasema  mwaka jana alikwenda Shule ya Msingi Viwanja Sitini iliyoko Ifakara kumwandikisha mtoto wake, lakini walimu wa shule hiyo walimwambia shuleni hapo hakuna nafasi ya kusoma mwanae Alewis kutokana na hali yake.

Alisema alielekezwa kwenda katika shule nyingine huko Ifakara ambayo huhudumia watoto wenye mtindio wa ubongo, lakini nako alipofika, walimu wa shule hiyo walimwambia hiyo ni shule maalumu kwa watoto wenye ulemavu wa akili na lewis hana tatizo hilo.
“Alewis ana hamu ya kwenda shule, na  hapa alipo anajua kusoma na kuandika baadhi ya maneno, tatizo hajapata shule, ndio maana naomba msaada wa jinsi ya kupata shule ya watoto kama huyu”, anasema Roswita.

Baada ya kutafuta shule bila mafanikio huko Ifakara, Roswita anasema amekuja Dar es Salaam ili kupata msaada wa kutafutiwa shule mtoto wake huyo.
Katika pilika pilika hizo amefanikiwa kupata shule iliyokubali kumpokea Alewis ili awaeze kuanza shule ya awali.
Shule hiyo inaitwa St. Bernard iliyoko Mbezi Kibamba, lakini kikwazo kingine ni kuwa shule hiyo haina bweni, hivyo itamlazimu yeye (Roswita)  kumpeleka Alewis shule na kumrudisha kila siku.

Kitu ambacho pia ni kigumu kwani Dar es Salaam amekaribishwa na  ndugu yake anayeishi Kimara na si mkazi.
Kikwazo kingine ni ada, kwani shuleni hapo anatakiwa kulipa Sh 300,000 kwa muhula, kiasi ambacho ni kikubwa mno ukilinganisha na kipato chake.

Wito wake kwa jamii
 Roswita anawataka wanajamii kuachana na dhana potofu juu ya ulemavu,anawaomba wasiwatenge  bali wawapokee na kuwafariji ili nao wahisi ni watu wa kawaida ndani ya jamii.
Anawaomba wasamaria wema kumsaidia mtoto wake kupata shule ya walemavu ya gharama nafuu na pia ikiwezekana wamsaidia  baiskeli ili naye aweze kutimiza ndoto yake ya kupata elimu.
Kwa kumsaidia Tumia namba 0716 676665

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU