AJIRA KWA WATOTO MAJUMBANI ZIKOMESHWE: ILO
Kufua nguo, kuteka maji, kulea watoto wenzao na hata kulea wazee, ni majukumu ambayo Shirika la kazi duniani, ILO limetaja katika ripoti yake kuwa yanakabili watoto walioajiriwa majumbani kinyume cha sheria na kutumikishwa kama watumwa. Ripoti hiyo ambayo inazinduliwa leo siku ya kimataifa ya kutokomeza ajira kwa watoto inaitwa Kutokomeza ajira za watoto majumbani na inasema watoto zaidi ya Milioni Kumi duniani kote wamenaswa kwenye mtego huo. Kati yao hao Milioni Sita na Nusu wana umri wa kuanzia miaka Mitano hadi Kumi Nne, na wengi wao ni watoto wa kike.
Mkurugenzi wa ILO anayeongoza mradi wa kutokomeza ajira kwa watoto, Dkt.Constance Thomas amesema ni nadra kwa watoto kuweza kujinasua kwenye mtego huo kwa kuwa wengi wao wanakuwa wanafanya kazi hizo kwa ujira mdogo na hata bila ujira kwa ndugu, jamaa au marafiki wa jamaa zao.
"Kazi ya nyumbani ni ajira, na watoto wanaoajiriwa majumbani ni ajira kwa watoto na inapaswa kuzuiwa, na pia suala lingine ni utungaji sheria na sera kwa sababu kuna mataifa yale ambayo hayana umri wa chini wa kufanya kazi majumbani, waweke umri huo, na umri huo usiwe chini ya umri wa miaka halali ya mtu kufanya kazi."
ILO inataka hatua za pamoja za kitaifa na kimataifa ili kuondoa tatizo hilo ambalo linawanyima watoto haki zao za msingi za kuishi, kulindwa na kuendelezwa.
TUSHIRIKIANE PAMOJA KUTOKOMEZA AJIRA KWA WATOTO, MAJUMBANI, VIWANDANI NA MIGODINI.
Comments
Post a Comment