WOTE TUSHEREKEE SIKUKUU YA EID, ASANTE MHESHIMIWA RAIS JAKAYA KIKWETE.
Mh. JAKAYA KIKWETE AWAKUMBUKA WENYE UHITAJI KATIKA EID
EL FITRI..
            Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ametoa zawadi
 za sikukuu ya Idd El Fitr zenye thamani ya Sh8.5 milioni kwa makundi 
maalumu, wakiwamo watoto wenye ulemavu, wazee, yatima pamoja na watoto 
walio katika mkinzano na sheria ili kuwaandalia mazingira mazuri ya 
kushiriki na kusherehekea sikukuu hiyo.
                
              
Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Rabikira Mushi 
jana kwa niaba ya rais alikabidhi zawadi hizo kwa vituo vya Dar es 
Salaam, katika hafla fupi iliyofanyika kwenye Mahabusu ya Watoto Kisutu 
na kuhudhuriwa na wawakilishi wa vituo husika.
Alisema, Rais ametoa zawadi ya mchele, mafuta ya 
kupikia pamoja na mbuzi kwa baadhi ya vituo vya Pwani, Kagera, Mbeya, 
Morogoro, Tanga, Zanzibar na Dar es Salaam.
Kaimu kamishna huyo alivitaja vituo vya jijini Dar
 es Salaam vilivyopatiwa zawadi hizo kuwa ni pamoja na Kurasini, 
Msongola, Chamanzi na kituo cha ushauri cha vijana cha Temeke.
Vingine ni pamoja na Mahabusu ya Watoto Kisutu, 
Mburahati, Msimbazi,Tupendane na Wazee Nunge Kigamboni Chuo cha Ufundi 
Stadi kwa wenye Ulemavu Yombo.
Mushi alibainisha kuwa mgawanyo wa zawadi hizo uliangalia idadi ya watoto katika kituo.
Akitoa shukrani baada ya kupokea zawadi, Ofisa 
Mfawidhi Jela ya Watoto Upanga, Alex Bwire alisema anamshukuru Rais kwa 
kuwapa faraja watoto lakini pia aliiomba jamii nzima ihusike katika 
kutoa michango kwa makundi maalumu badala ya kuachiwa Rais pekee.
Pia alizitaja changamoto wanazokumbana nazo katika
 mahabusu za watoto kuwa ni pamoja na kupokea idadi kubwa ya watoto 
isiyoendana na vyumba vya malazi, lakini pia bajeti ni finyu suala 
linalosababisha watoto kukosa baadhi ya mahitaji.
Comments
Post a Comment