RIPOTI MAALUMU.
ELIMU KWA WATOTO WENYE ULEMAVU, CHANGAMOTO KILA KONA.
Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wenye ulemavu wanaojiunga na shule mbalimbali za msingi siyo ya kuridhisha.
Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mambo ya afya (WHO), linakadiria kuwa
asilimia 10 ya watoto duniani wana ulemavu wa aina mbalimbali.
Matokeo
ya utafiti wa watu wenye ulemavu (Youth with Disabilities Community Project,
2007) yanaonyesha kwamba asilimia tano ya watoto nchini wana ulemavu wa aina
mbalimbali.
Utafiti
uliobuniwa na kugharimiwa na Benki ya Dunia (Filmer, 2005) ulipitia takwimu za
kila mwaka za kaya katika nchi 11 zinazoendelea na kuhitimisha kwamba kiwango
cha ulemavu ni kati ya asilimia moja hadi mbili ya watu wote waliohusika.
Matokeo
hayo yanaendana ya ulemavu ya Umoja wa Mataifa (DISTAT), pia yanaendana na ya
Sensa ya Taifa ya mwaka 2002 ambayo ilibainisha kwamba asilimia mbili ya watu
wote waliohesabiwa wana aina fulani ya ulemavu.
Vyanzo
vingine vinaweka makadirio ya kati ya asilimia 2.5 mpaka tatu ya jumla ya
watoto wa umri wa kwenda shule kuwa wana ulemavu.
Taarifa
ya Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi 2009 /17, inasema kuwa kama kiwango cha
ulemavu miongoni mwa watoto wa umri wa kuwa shuleni ni kati ya asilimia mbili
mpaka tano, maana yake kati ya watoto 150,000 na 350,000 wa umri wa miaka 7 -13
wana ulemavu.
Inasema
kuwa, takwimu za Wizara ya Elimu zinaonyesha kuwa watoto 34,661 wenye ulemavu
walihudhuria shule za msingi katika mwaka 2008, idadi ambayo ni kati ya asilimia
tisa hadi 20 ya watoto wote wenye ulemavu .
Msemaji
wa Wizara ya Elimu, Ntambi Bunyazu anasema wizara hiyo imekusudia kutoa frusa
sawa na kiwango bora cha elimu kwa wanafunzi wote.
Hata
hivyo anasema wanafunzi wenye mahitaji maalumu kielimu wamekuwa wakikabiliana
na vikwazo dhidi ya uwepo, ushirikishwaji na ujifunzaji.
“Ili
kufanikisha utoaji wa fursa sawa na kuboresha kiwango cha elimu kwa wanafunzi
wote, Elimu Jumuishi imeonekana kuwa ni mpango sahihi,” anasema Bunyanzu:
“Kwa
muktadha wa Kitanzania, Elimu Jumuishi ni mfumo wa elimu unaotoa fursa ya elimu
kwa watoto, vijana na watu wazima wote kupitia shule za kawaida na programu
nyingine za elimu bila kujali majaliwa yao ya nyuma na tofauti zao za kiuwezo,
bila ubaguzi, kwa njia bora na kwa matumizi mazuri ya rasilimali.”
Anasema
inajumuisha wanafunzi wenye mahitaji maalum kielimu wakiwamo wenye ulemavu,
yatima, kutoka familia zenye kipato duni, walioathiriwa na virusi vya ukimwi na
wale wa kutoka jamii za wafugaji, wavuvi na wawindaji.
Anasema
Wizara ya Elimu ilianza kutekeleza mpango wa Elimu Jumuishi mwaka 1997/10
katika halmashauri 77 ambapo kila moja ilichagua shule nne na kufanya jumla ya
shule 308. Kutokana na mpango huo walimu 1,232, Waratibu wa Elimu Kata 308,
Wakaguzi wa Shule wa halmashauri 77 na Maofisa Elimu wa halmashauri 77 walipata
mafunzo.
Anasema
kuwa, pamoja na mambo mengine mafunzo hayo yalilenga kuwafanya wasimamizi hao
wa elimu waweze kuanzisha madarasa ya elimu jumuishi, kufundisha na kufuatilia
kikamilifu maendeleo ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kielimu.
Anasema
pia kuwa, Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi 2009/17 moja ya lengo lake kuu ni
kuweka mwongozo wa utekelezaji wa elimu hiyo nchini.
“Lengo
la Elimu Jumuishi ni watoto wote, vijana na watu wazima wa Tanzania wawe na
fursa sawa ya kupata elimu bora katika mazingira jumuishi. Mkakati wa Taifa wa
Elimu Jumuishi ulithibitishwa na serikali mwaka 2010,” anasema Bunyanzu.
Anasema
mambo muhimu ambayo yatafanikisha utekelezaji wa elimu jumuishi ni pamoja na
kubaini mahitaji maalumu ya kielimu ya mwanafunzi, kuwepo vifaa vya kufundishia
na kujifunzia na kuelimisha wadau wa elimu kuhusu elimu jumuishi.
Anasema
pia kuwa ushirikiano baina ya wadau wa elimu, mazingira rafiki ya shule na
upatikanaji wa fedha za kuendesha mipango ya elimu jumuishi ni vitu vitakavyo
saidia kuendeleza elimu hiyo.
“Ni
vema ieleweke kuwa utekelezaji wa mpango wa Elimu Jumuishi si wajibu wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pekee; bali inahitaji ushirikiano na ushiriki wa
taasisi zote za kielimu,” anasema.
Juma
lililopita serakali ilitangaza majina ya wanafunzi 18,754 waliochaguliwa
kujiunga na vyuo vya ualimu kati yake 11,806 wamechaguliwa kusomea ngazi ya
cheti (Grade A) na 6,948 watasoma stashahada.
Waliochaguliwa
kusoma elimu maalumu ni 420 kati yake 363 watasoma cheti na 57 stashahada.
Akizungumzia
kuwepo kwa idadi ndogo ya wato wanaochaguliwa kusomea ualimu wa elimu maalumu,
Bunyanzu anasema hali hiyo inatokana na jinsi ambavyo wanafunzi wenyewe
wanachagua.
“Kufundisha
elimu maalumu inatakiwa mtu apende mwenyewe, lazima ndani ya moyo wako uwe na
wito huo, siyo rahisi sana kwenda kuwafundisha hawa watoto ndiyo maana hauwezi
kumpeleka tu mtu ambaye hataki,” anasema Bunyanzu.
Hata
hivyo anasema kuwa, bado idadi kubwa ya wazazi wenye watoto wenye umri wa kwenda
shule wanawaficha watoto badala ya kwenda kuwaandikisha shuleni.
“Kazi
kubwa inayotakiwa kufanyika kwa sasa ni kuwashawishi wazazi wawapeleke watoto
hawa shule, kwenye baadhi ya maeneo walimu wapo lakini watoto hakuna,” anasema
Bunyanzu.
Baadhi
ya taarifa zinaonyesha kuwa, kwa baadhi ya watoto wenye ulemavu ambao wapo
shuleni wanakabiliwa na changamoto za moundombinu ya shule kutokuwa rafiki.
Sheria
ya Elimu ya mwaka 1978, inatambua kisheria haki ya kila mtu ya kupata elimu ya
msingi. Ni jukumu la wazazi kuhakikisha kwamba watoto wao wanaandikishwa na
kuhudhuria shule bila kukosa.
“Hakuna
mtu atakayenyimwa nafasi ya kupata elimu kwa sababu tu ya mbari, dini au imani
yake ya kisiasa au ya kimrengo,” inasema sheria hiyo.
Comments
Post a Comment