Skip to main content

TAFAKARI,,,, CHUKUA HATUA.

Jamii inapaswa kutambua na kuweka mazingira sahihi kwa ajili ya Walemavu

(835) Views
ULEMAVU ni athari ya muda mfupi au ya kudumu inayosababishwa na hitilafu za kiwiliwili au hisia mfano uoni, usikivu, akili, kusema na kumsababishia mtu kushindwa kufanya kazi kikawaida.
Jamii ya watu wenye ulemavu nchini ni kundi kubwa miongoni mwa takribani ya watanzania milioni 45, ambao wamesahaulika katika sekta mbalimbali kutokana na jamii kuwatenga na kusahaulika kabisa bila kuwasaidia katika maisha ya kila siku. Kwa miaka mingi, suala la ulemavu halikupewa umuhimu na uzito wowote katika jamii kutokana na mitizamo na imani potofu. 
Kuna aina nyingi za ulemavu, kuna ulemavu wa viungo, ulemavu wa uoni, kiziwi na matatizo ya kusema, ulemavu wa akili, albino (ulemavu wa ngozi) mwingineo kama kifafa, kichwa kikubwa mpasuko wa mdomo pamoja na ulemavu mchanganyiko ambapo mtu anakuwa na ulemavu zaidi ya mmoja katika jamii tunayoishi.
Wahenga walinena kuwa “hujafa hujaumbika” na “usimtukane mamba kabla ya kuvuka mto” nimeanza maudhui haya kwa methali hizi lengo likiwa ni kukumbushana umuhimu na wajibu wetu wa kuwaenzi na kuwajali watu wenye ulemavu.
Aidha, ni vyema kila mtu akatambua kuwa ulemavu umegawanyika katika viwango tofauti, kuna ulemavu mdogo ambao mtu anakuwa na kasoro ndogo katika mwili au hisia lakini anaweza kujihudumia na kufanya kazi zote. Tafsiri halisi ya mlemavu imepindishwa paia hata sera, mikakati na hata utekelezaji wake navyo vimekuwa hivyo hivyo.
Tunapozungumzia ulemavu wa kiasi mtu anaweza kujihudumia na kufanya kazi endapo atatumia visaidizi na mazingira yanapoboreshwa katika kiwango cha ulemavu mkubwa mtu huitaji kusaidiwa katika maisha yake yote kwa ujumla.

Chanzo cha ulemavu

Katika suala hili zipo sababu nyingi zinazoweza kumfanya mtu anaweza kupata ulemavu kama kurithi, vita, utumiaji ovyo wa dawa za kulevya, magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari, homa kali, surua, ajali, kupigwa na huduma duni kwa mama wajawazito wakati wa kujifungua na kupata mimba kwenye umri wa chini ya miaka 18.
Wakati tukiishi na kundi hili katika jamii zetu ninatambua kuwa zipo changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na jamii kuwabagua kijamii, kisiasa na kiuchumi mambo ambayo yakuwa vikwazo juu ya maisha yao ya kila siku na kusababisha wao kujiona kama watu ambao hawana umuhimu au haki ya kuishi kama watu wengine katika maeneo wanayoishi.
Takwimu za Twaweza kupitia utafiri wa "Sauti za Wananchi" zinaonyesha kwamba asilimia 10 ya Watanzania ni watu wenye walemavu na hivyo kunifanya kuelewa kuwa jamii tunawachukulia watu wenye ulemavu kwa mitizamo tafauti na kusahau kuwa ulemavu hautokani na mapenzi ya mtu fulani, bali ni jambo, ambalo humpata mtu yeyote bila kutegemea.
vyanzoulemavu
Jendwali ikionyesha vyanzo vya ulemavu tokana na maoni ya wanajamii
Imekuwa heri kwamba, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 iliyopo sasa inaeleza bayana kuwa ni wajibu wa serikali kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu.
Pamoja na katiba kueleza hivyo, hali imekuwa tofauti kabisa na mara nyingi watu wenye ulemavu wamekuwa wakihudumiwa na mashirika ya dini na vyama vyao vya hiari vya kutetea haki zao.
Huduma muhimu
Shule za Msingi na Sekondari zilizopo karibu na vituo vya daladala sio rafiki kwa watoto wenye ulemavu, wanazidi kupata usumbufu wa kukabiliana changamoto barabarani kwenye magari na hakuna askari anayewavusha katika maeneo mengi nchini.
Kwa mfano, karibu vyombo vyote vya usafiri vinavyoingia nchini havina vigezo vya kimataifa vinavyowawezesha watu wenye ulemavu kupanda na kuteremka bila tatizo
Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya marekebisho yanayotakiwa kufanyiwa kazi ni pamoja na kuweka sehemu maalum kwa ajili ya walemavu ni vyoo vya umma ambavyo havijawekewa utaratibu wa kulisaidia kundi hilo na badala yake wanalazimika kushika maji (kwa wale wanaotumia mikono kutembea kutoka eneo moja kwenda eneo lingine) machafu yanayoweza kuathiri afya zao pamoja na kukosekana kwa ngazi (ramps).
Kwa ujumla mazingira yasiyofikika nayo ni kikwazo kikubwa kwa watu hawa kwani wanashindwa kufikia huduma muhimu za kibinadamu hususani sehemu za majengo ya kwenda juu yanayojengwa na serikali pamoja na taasisi binafsi kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii ujenzi huo hauzingatii miundo mbinu ya watu wenye ulemavu kutokana na hali waliyokuwanayo ya kimaumbile unakuwa usumbufu kufikia sehemu za juu ndani ya majengo hayo kwani hapana visaidizi vya kisasa vilivyowekwa kwa ajili ya watu hawa.
Sheria inasema nini?
Sheria ya watu wenye ulemavu (haki na fursa) na.9 ya mwaka 2006 inasema `watu wenye ulemavu wanatakiwa kuwa na fursa iliyo sawa kwa manufaa ya taifa katika nyanja zote za kijamii na katika elimu, habari, mawasiliano na mazingira ya kimaumbile kama vile lugha ya alama, tafsiri kwa visiwi, kanda, maandishi ya nukta nundu, taarifa na vipindi vinavyotokana na kompyuta, tovuti na kuweka mpangilio wa mazingira halisi kama vile nyumba, majengo, usafiri na mitaa ili waweze kuifikia.
Ajira kazini
Kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2010, inahamasisha na inataka maeneo yote ya ajira kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu, ili waweze kupata ajira sawasawa na watu wengine.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la TWAWEZA, umeonyesha kuwa nusu ya Watanzania wameshuhudia ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu katika jamii bila kutoa msaada, na kulifanya kundi hilo kuendelea kubaguliwa na kubaki katika hali ngumu ya maisha licha ya kutupiwa lawama kuwa hawajishughulishi.
Pia utafiti huo umeonyesha kuwa idadi kubwa ya wananchi kwa asilimia 91 waliripoti kuwa wanawaona watu wenye ulemavu kama watu wanaohitaji kutunzwa. Vile vile mwananchi mmoja kati ya watatu aliripoti kuwaona watu wenye ulemavu kama siyo watu kamili kwa asilimia 33 au kuwa ni watu ambao ni kikwazo kwao kwa asilimia 32. Na ni wananchi wawili tu kati ya kumi 17 waliokiri kufahamu asasi au mashirika yanayotoa upendeleo kwenye suala la kuwaajiri watu wenye ulemavu.
Aidha, mbali na utafiti huo katika jamii imani potofu zimekuwa zikisababisha baadhi ya wanajamii kudhani kwamba, ulemavu wa mtu unaweza kumtajirisha mwingine kwa kumkata kiungo au kumchuna ngozi na kuipeleka kwa waganga wa kienyeji.
Kadhalika, ombi langu kwa serikali ni kwamba uhakikishe inazitaka idara inayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ihamishwe na kupelekwa Ofisi ya Rais.
Utafito unaonyesha kwamba mahitaji ya watu wenye ulemavu ni mtambuka, hivyo Ofisi ya Rais ina uwezo zaidi wa kutatua matatizo yao.
Kwa hali hiyo, watanzania wenzangu ni muda mwafaka wa kuachana na dhana potofu kwamba, ulemavu ni ugonjwa jamii pia tutambue kwamba, ulemavu siyo kizuizi cha kumfanya mtu ashindwe kushiriki kwenye ujenzi wa taifa walemavu ni wanadamu kama walivyo watu wengine na hata mahitaji yao ni sawa.
Umefika wakati wa serikali kukunjua mbawa zake katika jamii na kusimamia ipasavyo haki na fursa kwa watu wenye ulemavu ili nao waweze kuondokana vilio vya muda juu ya ubaguzi, mateso, machungu yaliyopelekea kukata tamaa kwa walio wengi,ni muhimu kufikiria zaidi juu ya uwepo wa watu hawa wenye uwezo mkubwa wa kiutendaji wakiwezeshwa na kupewa mbinu za kujikwamua pia washirikishwe katika mambo mbalimbali ya kitaifa na kijamii.
Je, mimi na wewe tuna uhakika gani kuwa tutaendelea kuwa na viungo vyetu timamu hadi mwisho wa maisha yetu? Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu na anayemcha Mungu daima hawezi kuwanyanyasa au kuwafanyia unyama walemavu.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU