AJIRA KWA WATOTO HUZAA TAIFA MASKINI



KWA miaka mingi haki za watoto zinakiukwa hasa katika suala la kuwaajiri kinyume cha umri wao, hili ni kosa kisheria.
Baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wanasema pengine ni kutokana na watoto hao kutokuwa na uamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa na kama wanashirikishwa huwa ni kwa kiasi kidogo.
Kwa sababu hiyo katika jamii zetu wengine wanatumia nafasi hiyo kuwapa ajira ngumu watoto chini ya miaka 18 ambao sheria huwatambua.
Mtoto Addul Ismail (15) anayeosha magari eneo la Kigogo Mbuyuni anaeleza kuwa ndoto zake kutoka awali ni kusoma na kuja kuwa mwanasiasa katika kulisaidia taifa lake, lakini haikuwa hivyo baada ya wazazi wake kumwachisha shule akiwa darasa la sita na kumlazimisha kwenda jijini Dar es Salaam kujitafutia kipato ili kuisaidia familia yake.
“Mimi wazazi wangu wanaishi Mtwara Vivijini nimekuja huku kutokana na hali ya maisha ya familia, ndoto yangu ilikuwa kuja kuwa mwanasiasa maarufu hapo badaye lakini ndoto hizo kwa sasa zinafifia siku baada ya siku kwa kuona kuwa matarajio ya kusoma hamna tena,” anaelezea Abdul.
Katika makala hii mtoto mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bahati (10) mkazi wa Ubungo ni mwenyeji wa Mbeya anayeishi na shangazi yake jijini Dar es Salaam, anasema baada ya kushindwa kuendelea na masomo shangazi yake alimchukua na kumwajiri kwenye kibanda chake ili amuuzie maji na juisi wakati huo huo ni mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Ubungo, Manispaa ya Kinondoni.
Hapa inadhiririsha kwamba kupitia kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla elimu inahitajika kuelezea umuhimu wa haki za watoto hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania ambapo unyanyasaji wa watoto unaonekana ni jambo la kawaida.
Mwandishi wa makala hii pia amepita katika maeneo ya Fire, Kariakoo na kushuhudia baadhi ya wazee wakiwa wanatembea na vijana wadogo na kuwatumia kama ombaomba kwa niaba yao.
Baadhi ya watoto hao ni binti aitwaye Rahel Chilinwo (12) anatoka mkoani Dodoma na mama yake kuja Dar es Salaam kutokana na migogoro ya kifamilia kati ya baba na mama, hali iliyowasababishia ugumu wa maisha na kuendesha maisha yao kwa njia ya kuomba mitaani.
“Shule siendi, baba hajanipeleka kila siku mama ananituma kuomba kwenye magari na maduka ya Wahindi na kwa siku tunapata kati ya sh 1,500 hadi sh 2,000 inatusaidia kula,” anasema Rahel.
Ni dhahiri kwamba jamii bado inahitaji kupewa elimu kwa kina zaidi juu ya haki za watoto na umuhimu wa kuzilinda haki hizo kutokana na matukio ya ukiukwaji wa haki za watoto licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na mashirika mbalimbali yanayojishughulisha na utetezi wa haki za watoto.
Kwa mujhibu wa sheria na haki za watoto, kuna ajenda muhimu 10 zilizoainishwa katika kulinda haki za watoto kwa kila taifa, ajenda hizo ni Kuwekeza katika kuokoa maisha ya watoto na wanawake, lishe bora, huduma bora za maji na usafi wa mazingira hasa vyoo shuleni na kwenye vutuo vya afya.
Ajenda nyingine ni kuwekeza katika kumwendeleza mtoto mdogo, elimu bora kwa watoto wote, shule kuwa mahali safi na salama, kuwalinda watoto wachanga na wasichana dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Nyingine zilizoainishwa ni pamoja na kupunguza mimba za utotoni, kuwekeza katika kuwanusuru watoto na vitendo vya vurugu, udhalilishaji na unyonyaji.
Ajenda zilizoainishwa ni muhimu lakini makala hii inalenga katika ajenda ya kuwekeza katika kuwanusuru watoto na vurugu, udhalilishaji na unyonyaji.
Watoto wengi wananyonywa hasa wanaotumikishwa katika ajira ya ujira mdogo na mabosi wao hali isiyoendana na kazi wanazofanya, wapo ambao wanadhalilishwa kijinsia katika mazingira wanayoishi na kutumikishwa katika kazi ngumu kama migodi.
Ajenda hii inaakisi maisha ya mtoto Dickson Temba (13) mkazi wa Morogoro anayeuza mayai ya kuchemsha eneo la Ubungo darajani, ambaye anaelezea kwa uchungu kwamba amejikuta katika kazi hiyo baada ya mwajiri wake aliyekuwa akimchungia ng’ombe huko Kilosa kumtumikisha kwa mda mrefu bila ujira kwa miezi mitatu.
Utafiti unaonyesha kwamba watoto walio wengi wanajua haki zao lakini tatizo ni kukosa sauti kutokana na mfumo wa maisha yetu ya kuheshimu wakubwa ndio maana hivi karibuni kupitia baraza la watoto waliamua kukutana na Rais Jakaya Kikwete kumweleza umuhimu wa kutekelezewa ajenda zinazowahusu watoto.
Katika harakati hizo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 baadhi ya mashirika yanayohusika na haki za watoto likiwamo UNICEF walikutana na baadhi ya wagombea katika kujadiliana nao hasa kubeba ajenda ya watoto kuwemo katika ilani zao ili kutekeleza haki za watoto katika sekta mbalimbali.
Kwa mujibu wa takwimu zinaonyesha kwamba kuna zaidi ya watoto milioni mbili yatima ambao hulelewa na ndugu ama walezi wengine hupelekwa kwa jamaa na wengi kuishia mitaani.
Watoto ambao umuhimu kuckukuliwa kama ajenda ya lazima huanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa ujumla, pia elimu ya kina inahitajika katika kuelimisha jamii suala la haki za watoto na watoto wenyewe kuzijua ili pale wanapoonewa wapaze sauti zao na kukataa vitendo hivyo.
Aidha, juhudi hizi zinaweza kufanikiwa ikiwa asasi mbalimbali za kiraia, vyombo vya habari, mashirika binafsi hasa yale ya dini na serikali yakishirikiana kufanikisha kuondoa tatizo hili.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU