ULEMAVU SI MKOSI WALA LAANA.
WANAUME
WATELEKEZA WATOTO WALEMAVU ARUMERU
|
Wanawake
wasukumiwa mzigo
Tatizo la wanaume kuwatelekeza
watoto wao wenye ulemavu, limetajwa kukithiri katika Kijiji cha Ambureni,
Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa
na JAMHURI
hivi karibuni, umebaini kuwapo kwa
familia zaidi ya 15 zenye watoto walemavu zilizotelekezwa na waume, hivyo
wanawake kuachiwa mzigo wa kuzilea.
|
Tabia hiyo imesababisha familia
hizo kuishi katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na kuishi katika nyumba
za kupanga, huku zikiwa hazina kazi za kujipatia kipato. Mateso
yanayowakabili wanawake hao yanatokana na kujifungua watoto wenye ulemavu,
kwani bila kujifungua watoto hao wangeendelea kuishi na waume zao.
Zeana Athuman, mkazi wa Ambureni
ambaye pia ni mwanawake aliyeathirika na hali hiyo, anasema mume wake
aliondoka nyumbani baada ya kujifungua mtoto mwenye ulemavu.
“Baada ya kujifungua mume wangu
alitoroka nyumbani na akaniacha nikiwa peke yangu katika hali ngumu
kimaisha,” anasema Zeana.
Alijifungua mtoto mwenye ulemavu
wa kutoona, kutotembea, kutosikia na kutozungumza.
“Mume wangu alimwona mwanangu kama
mkosi ndani ya familia, alinikimbia mtoto akiwa na mwezi mmoja,” anasema.
Anaongeza kwamba tangu mumewe
amkimbie ni miaka 11 imepita sasa, jambo linaloendelea kufanya maisha yake na
mtoto wake kuwa magumu zaidi.
Zeana anasema ili kukidhi mahitaji
yake na mtoto wake kwa siku, analazimika kumuacha mwanaye huyo kwa majirani
aweze kutafuta fedha za kujikimu. Changamoto iliyopo ni kwamba muda mwingi
mtoto huyo hufungiwa ndani wakati wote ambao mama yake hutoka kwenda kutafuta
riziki.
JAMHURI pia inakutana na mtoto anayetajwa kwa jina moja la
Terezia (6) mwenye ulemavu anayeishi na bibi yake. Taarifa zinasema baba
mzazi wa mtoto huyu aliondoka nyumbani hapo baada ya kuona mtoto wake ni
mlemavu.
Wakati baba akiwa amemtoroka
mwanaye, mtoto huyu anatajwa kuwa katika mazingira magumu zaidi kwani hata
mama yake naye hulazimika kuondoka nyumbani na kumuacha akiwa peke yake.
“Mtoto huyu alizaliwa akiwa mzima,
baada ya miezi saba hali yake ilianza kubadilika akawa haoni wala kusikia
ndipo baba mzazi alipoamua kuondoka nyumbani.
“Mama mzazi naye alianza kumficha
ndani kwa madai kuwa anaogopa watu kumsema amezaa mtoto mlemavu.
“Baada ya majirani kugundua tatizo
hilo waliamua kwenda kumtoa ndani kwa nguvu na kuanza kumshindisha nje kama
watu wengine,” anasema bibi wa Terezia bila kutaja jina lake.
Kutokana na changamoto
zinazowakabili wanawake wenye watoto walemavu kijijini hapo, hatimaye
wamebuni mbinu za kulea watoto wa watu (yaya) ili wapate kipato cha kuendesha
maisha yao.
Mwalimu wa kituo cha kulelea
watoto wenye ulamavu katika Shule ya Msingi Moivaro wilayani Arumeru, Leah
Ndaga, anataja changamoto zinazowakabili katika kazi hiyo. Mwalimu Leah
anasema kwamba kwa muda mrefu sasa wananchi wamekuwa wakibeza aina ya kazi
wanayoifanya kwa madai kuwa wanapoteza muda kukaa na watoto wenye ulemavu.
“Tunatoa elimu kwa jamii na maeneo
yanayotuzunguka kuwa watoto hawa ni sehemu ya jamii yetu. Tunaiomba jamii
iwachukulie kama sehemu yao isiwatenge badala yake iwasaidie wanapohitaji
msaada ukiwamo wa kwenda shuleni,” anasema.
Wakati wakiendelea na juhudi za
kusaidia miundombinu ya kwenda eneo moja hadi jingine, kituo hicho kina
watoto 47. Kati ya hao, watoto watatu wana ulemavu wa macho huku wengine
wakiwa na ulemavu wa kutosikia, kutoongea na kutotembea.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha
Msovero, Sioni Mathayo, akizungumzia changamoto hiyo anasema imekuwa vigumu
kuwasaidia watoto hao kutokana na kutokuwa na kipato cha kutosheleza
mahitaji.
“Serikali ya kitongoji hatuna
mafungu ya kusaidia watoto walemavu. Tunaomba viongozi wajaribu kuangalia
upya jinsi ya kuziwezesha serikali za vitongoji ambazo zipo na wananchi,’’
anasema Mathayo.
Pamoja na kutokuwa na bajeti,
Mwenyekiti huyo anabainisha kuwa kama kiongozi alichukua jukumu la kupeleka
matatizo hayo kwenye uongozi wa juu ili kupata msaada wa namna ya kuwabana
wanaume hao wasizikimbie familia zao.
Anasema juhudi nyingine
zinazofanywa ni za kuwapatia msaada kupitia Kituo cha Aston Vision kilichopo
kijijini hapo, ambacho hutoa elimu kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira
magumu.
Mwasisi wa kituo hicho, Aston
Simoni, anasema lengo la kuanzisha kituo hicho lilitokana na kijiji hicho
kuwa na watoto wengi wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
“Hapa tunapata msaada kutoka kwa
wadau wa nje na ndani ya nchi ambao hutusaidia chakula, magodoro na dawa za
kuongeza vitamini kwa watoto yatima na wale wenye walemavu.
|
Comments
Post a Comment