TATIZO SUGU
MAZINGIRA MAGUMU YA KUJIFUNZIA NI CHANZO CHA UTORO KWA
WANAFUNZI WENYE WALEMAVU WILAYANI NAMTUMBO.
Mwalimu wa kitengo maalumu cha shule ya msingi Namtumbo Bw Lezile Kampango amesema changamoto kubwa katika kituo hicho pekee cha wanafunzi wenye ulemavu wa akili wilayani namtumbo ni ukosefu wa chakula,vifaa vya kufundishia, madarasa na walimu.
“Watoto kama hawa hawawezi kusoma
bila chakula, kwani mwanafunzi akihisi njaa tu anatoka nje na kurudi kwao
bila hata ya kuuliza, gari ikipita wote wanatoka na kulikimbilia, ukiwa
mwalimu inabidi uhakikishe kuna vivutio vya kutosha kuwafanya wafike shule na
kukaa madarasani,” alisema Kampango.
|
Wilaya ya namtumbo ina kitengo
kimoja tu cha watoto wenye mahitaji maalumu kilichopo katika shule ya msingi
Namtumbo kinachohudumia wanafunzi wenye ulemavu wa hakili tu.Kitengo hiki kina
mwalimu mmoja na wanafunzi watano wanaohudhuria kati ya 26 walioandikishwa.
Kitengo hicho akilianzishwa mwaka
1997 na ndicho kitengo pekee kinachoshughulia kutoa elimu kwa watoto wenye
ulemavu katika wilaya nzima ya Namtumbo kwa kuwa hakuna kitengo wala shule
ambayo inatoa elimu maalum katika makundi mengine ya wenye ulemavu kama
wasioona na wasiosikia.
Takwimu za mwaka 2011 zinaonesha
kuwa, wilaya ya Namtumbo ina jumla ya walemavu 252, kati yao wanafunzi 181 ndio
wanaosoma shule mbalimbali katika elimu jumuishi wakiwemo wenye ulemavu wa
akiri 34,wasioona 18,wasiosikia 11,walemavu wa viungo 109 na wenye ulemavu wa
ngozi tisa.
Wanafunzi 71 waliokuwa na umri wa
kwenda shule hawajaandikishwa na hawapo mashuleni wakiwemo wenye ulemavu wa
akiri 21,asiyeona mmoja, wasiosikia 11,wenye ulemavu wa viungo 35 na wenye
ulemavu wa ngozi watatu.
Takwimu za shirika la umoja wa
mataifa la kuhudumia watoto ulimwenguni(UNICEF) za mwaka 2002 zilionesha kuwa
asilimia 98 ya watoto wenye ulemavu katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania
hawapatiwi kabisa elimu jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wao.
Imeelezwa kuwa asilimia hii ndogo
inasababishwa na kuwepo kwa shule chache maalum hapa nchini kwa ajili ya watu
wenye ulemavu, ukosefu wa wataalamu,sera na sheria nyingi za nchi
hizo hazitaji moja kwa moja au kutoa utaratibu mzuri wa kutoa elimu
kuhusu wenye ulemavu, ukosefu wa vifaa maalum na muhimu vya kuwawezesha kusoma
pamoja na miundombinu duni isiyokidhi mahitaji ya watu
wenye ulemavu.
ANGALIZO.
Hili tatizo si kwa wilaya
ya Namtumbo pekee yake, hili ni tatizo kwa taifa zima kwa ujumla. Wadau wa
elimu ni vema wakalitazama suala hili kwa jicho la pekee, kwa sababu hawa
watoto wana haki sawa ya kupata elimu kama ilivyo kwa watoto wasio na ulemavu.
Comments
Post a Comment