WOTE TUKO SAWA MBELE ZA MUNGU


WATOTO WENYE ULEMAVU WAMEKOSA NINI?

JULIETH MKIRERI
 
 

WADAU mbalimbali wa elimu yakiwemo mashirika binafsi na ya kiserikali, wamekuwa wakitupia lawama kwa wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kwa kushindwa kuwapeleka shuleni.
Wamekuwa wakitoa madai hayo bila ya kuzifanyia kazi changamoto zinazowakwamisha wazazi hao kuwapa watoto hao haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Wengi wa watoto wenye ulemavu toka vijijini wamekuwa wakiishi mazingira magumu kutokana na hali duni za wazazi wao.
Wazazi nao wamekuwa wakisubiri hadi watoto wao walemavu watambuliwe na mashirika au wafadhili ndipo wasaidiwe kupata elimu.
Jambo la kutegemea msaada si rahisi kwa kila mzazi, kwani hata wafadhili hawana fedha za kutosha kuhudumia walemavu wote wa Tanzania.
Hivyo, kuwategemea wafadhili kutasababisha watoto wengi, hasa vijijini kuendelea kuishi bila kupelekwa shuleni.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kongowe, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, Beatus Lingumbuka anasema shule yake ina wanafunzi 1,502; wavulana 789 na wasichana 713.
Anasema katika kitengo cha elimu maalumu kuna wanafunzi 42 wa mtindio wa akili, viziwi, albino na walemavu wa viungo wawili.
Akielezea juu ya wanafunzi ambao wana ulemavu, mwalimu huyo anasema baadhi yao wamekuwa wakikatisha masomo mara kwa mara kutokana na kukosekana kwa watu kutoka katika familia zao kuwahudumia.
Kila mtoto anahitaji mtu wa kumpeleka shule asubuhi na kumchukua ili kurudi nyumbani mara baada ya muda wa masomo kila siku.
Suala hili linaweza likaoneka kama ni jambo rahisi kwa watu wa mijini, lakini ni gumu sana kwa mkulima au mfugaji wa kijijini.
Mwalimu huyo anaendelea kueleza kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo wanafunzi wenye ulemavu ni kushindwa kujitegemea kwa kutembea wenyewe hadi shuleni.
Watoto hao wanahitaji kusindikizwa na anapokosekana msindikizaji ndipo wanapofikia hatua ya kukatisha masomo.
“Katika shule yangu kitengo cha elimu maalum, kilianza miaka kumi iliyopita lakini kikubwa kinachosababisha wanafunzi wenye ulemavu kushindwa kuendelea na masomo yao ni kukosa wasindikizaji,” anasema Lingumbuka.
Pia ukosefu wa chakula shuleni kwa watoto walemavu limekuwa tatizo kubwa kwani wakiona hakuna uji wala chakula hawaendelei kuja shule, wanagoma na kuendelea kubaki nyumbani,” anasema.
Walimu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa mtindio wa akili na kutosikia (Viziwi), Damaris Mkonye na Getrude Kavishe wanasema mbali ya changamoto hizo, huduma muhimu kwa wanafunzi hao ni tatizo.
Wanasema vifaa vya michezo na ziara za kimasomo vinasababisha wanafunzi hao kushindwa kuendelea na masomo.
Mwalimu Kavishe ambaye anafundisha walemavu wenye mtindio wa akili, anasema katika darasa lake anakabiliwa na ukosefu wa vifaa vya kufundishia pamoja na vya michezo.
“Unajua ili hawa watoto wenye ulemavu waendelee kuja shuleni, ni lazima kuwepo na vivutio kama vifaa vya kutosha kwa ajili ya michezo.
“Pia, chakula kiwepo na wapate muda wa kucheza. Kama hakuna vitu hivyo, huwaoni umuhimu wa kuwa shuleni,” Getrude anasema.
Serikali pia haijatenga fungu la kutosha kuwawezesha walimu kuzunguka nyumbani kwa watoto hao kuwafuatilia juu ya masomo wanayofundishwa.
“Unajua katika darasa la walemavu ratiba yao inaelekeza siku nne ni za kuja shuleni kufundishwa lakini siku moja ambayo ni ya tano katika juma tunatakiwa walimu tuwatembelee nyumbani kwao, ili tujue kama tunayowafundisha wanafanya kama inavyotakiwa. Sasa fedha za kutuwezesha kuwafikia hakuna,” anafafanua.
Kwa upande wake mwalimu wa wanafunzi viziwi, Mkonye anaelezea juu ya uelewa mdogo wa wazazi wa watoto wenye ulemavu.
Anasema wazazi wengi wanawanyima haki yao ya msingi kwa kutowapeleka shuleni kupata elimu sawa na wengine.
Mkonye anasema baadhi ya wazazi wa watoto wenye ulemavu wamekuwa na tabia ya kuwaficha watoto wao. Jambo linalosababisha waendelee kuishi bila ya kuwasomesha wakidhani watoto walemavu hawawezi kumudu masomo sawa na wale ambao hawana ulemavu.
Anawataja baadhi ya wanafunzi ambao wameacha masomo kutokana na sababu mbalimbali akiwemo mwanafuzi wa kike aliyekatisha shule mwaka 2010 mkazi wa Miembe Saba.
Anasema wazazi wake hawakuona umuhimu wa kuendelea kumsindikiza shuleni.
Mwalimu huyo anasema wazazi wa binti huyo kiziwi walimkatisha masomo akiwa darasa la tano. Baadae walimpeleka kufanya kazi za ndani jambo waliloona ni muhimu kuliko kusoma.
Wengine waliokatisha masomo ni pamoja na msichana aliyeacha shule akiwa darasa la tatu mwaka 2009 kutokana na kukosa mtu wa kuendelea kumsindikiza shuleni.
“Mvulana mmoja, mkazi wa Mwambisi nae alikatishwa masomo akiwa darasa la pili mwaka 2009 kwa kukosa msindikizaji wa kumfikisha shuleni,” anasema.
Aidha, anasema kuwa mwanafunzi mmoja mkazi wa Visiga nae alishindwa kuanza masomo kutokana na umbali mrefu kutoka nyumbani kwao na kukosekana kwa mtu wa kumsindikiza.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, ameomba serikali iongeze bajeti hasa kwenye vituo vya walemavu ili viweze kununua vifaa na kupika chakula kitakachosaidia kuwavutia walemavu kuendelea na masomo.
Serikali ikiongeza bajeti itawasaidia kwa kuwa wazazi kwa sasa hawachangii kabisa swala la chakula kwa watoto wao. Hivyo, fedha za ruzuku kwa ajili ya maendeleo ya shule zinapoisha hawana sehemu nyingine ya kupata fedha za kununulia chakula kwa wanafunzi hao.
Hivi sasa shule hiyo inapika uji kwa ajili ya watoto wenye ulemavu ili kuendelea kuwavutia kuipenda shule na kuendelea kuhudhuria katika vipindi vya masomo.
Changamoto nyingine ni ya uhaba wa vyumba vya madarasa kwa watoto wenye ulemavu. Kwa sasa wanatumia chumba kimoja kwa madarasa matatu badala ya kila darasa kuwa na chumba chake.
Mwalimu huyo mkuu anawasihi pia wazazi kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wenye ulemavu na kuondokana na dhana potofu ya kudhani kila mtoto anayezaliwa akiwa mlemavu amerogwa.
Hata hivyo, imebainika kuwa baadhi ya wazazi wa watoto wenye ulemavu wamekuwa wakificha taarifa za watoto wao.
Wazazi hao wamedai kuwa wamekuwa wakitembelewa mara nyingi na baadhi ya asasi, lakini hawarudi kuwapatia misaada na hivyo kuwakatisha tamaa.
Katibu wa watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Kisarawe, Pwani, Ibrahim Tully anasema katika maeneo ya vijijini bado kuna muamko mdogo wa wazazi kuwapeleka shule walemavu.
Anasema wazazi wanadai kuwa watoto walemavu hawawezi kufanya chochote.
Tully anasema ipo haja ya serikali kulichukulia umuhimu wa kipekee swala hilo ili kuwezesha kila mtoto mwenye ulemavu kupata haki yake ya elimu.
Anasema serikali iachane na mtindo wa kuzitegemea asasi pekee kuwaibua watoto hao na kuwasaidia.
Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo, mdau wa elimu, aliyetembelea Kijiji cha Chole kusaidia walemavu amezisihi asasi za kiraia kuendelea kutoa misaada ya baiskeli na vifaa vingine.
Anasema vifaa hivyo vitawawezesha watoto wenye ulemavu kufika shule.
Jafo pia anaeleza kuwa baadhi ya watoto wenye ulemavu waishio vijijini wanashindwa kupata haki stahiki kutokana na wazazi wao kuwaficha.
Anadai kuwa kuna mila na desturi, mkoani Pwani ya kudhani mtoto mwenye ulemavu anasababisha mikosi kwenye familia.


Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU