MKATABA WA KIMATAIFA WA HAKI ZA WATU WENYE ULEMAVU
MKATABA WA KIMATAIFA WA HAKI ZA WATU
WENYE ULEMAVU
&
MKATABA WA NYONGEZA (2006)
TAFSIRI ISIYO RASMI
UMOJA WA MATAIFA (NEW YORK-)
Dibaji
Walioridhia
Mkataba huu, kwa
(a) Kukumbuka kanuni zilizobainishwa
ndani ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa ambao unatambua hadhi ya asili, thamani,
usawa na haki zisizopokonyeka za watu wote ambao ni wa jamii ya binadamu kama uhuru
wa msingi, haki na amani duniani;
(b) Kutambua kwamba Umoja
wa Mataifa, katika Tamko la Dunia la Haki za Binadamu na Mikataba ya Kimataifa
ya Haki za Binadamu, umetangaza na kukubali kwamba kila mmoja ana stahili
kupata haki zote na uhuru kama zinavyoelezwa humo, bila tofauti ya aina yoyote;
(c) Kuthibitisha kwa
msisitizo hali ya kuwahusu watu wote, kutogawanyika, kutegemeana, na kuhusiana
kwa haki zote za binadamu na uhuru wa msingi na uhitaji wa watu wenye ulemavu
kuhakikishiwa kunufaika kwao kikamilifu bila ubaguzi;
(d)
Kukumbuka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi,
Kijamii na Kiutamaduni, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na za Kisiasa;
Mkataba wa Kimataifa wa kuondosha aina zote za Ubaguzi wa Rangi; Mkataba wa
Kimataifa wa Kukomesha aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake; Mkataba Dhidi ya
Mateso na Adhabu au Matendo Mengine ya Kikatili, yasiyo ya Kibinadamu au ya
Kiudhalilishaji; Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, na Mkataba wa Kimataifa
wa Ulinzi wa Haki za Wafanyakazi wote Wahamiaji na Familia zao;
e)
Kutambua kuwa
ulemavu ni dhana inayobadilika na kwamba ulemavu hutokea kutokana na
mchangamano baina ya watu wenye ulemavu na mitizamo na vikwazo vya kimazingira,
ambavyo huzuia ushiriki wao kamili na unaofaa kwa jamii katika hali iliyo sawa
na wengine;
(f)
Kutambua umuhimu
wa kanuni na miongozo ya kisera iliyomo ndani ya Mpango Kazi wa Dunia kuhusu
Watu wenye Ulemavu na kwenye Kanuni Sanifu za kuweka Usawa wa Fursa kwa Watu wenye
Ulemavu katika kushawishi uendelezaji, utungaji na utathmini wa sera, mipango,
programu, na hatua mbali mbali katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa
ili kutoa fursa sawa kwa watu wenye ulemavu,
(g)
Kutilia mkazo
umuhimu wa kujumuisha masuala ya ulemavu kama sehemu ya lazima ya mikakati
inayohusiana na maendeleo endelevu,
(h)
Kutambua pia
kuwa ubaguzi dhidi ya mtu yeyote kwa msingi wa ulemavu ni uvunjaji wa hadhi ya
asili na thamani ya nafsi ya binadamu;
(i)
Kutambua
zaidi uanuwai miongoni mwa watu wenye ulemavu;
(j)
Kutambua haja ya
kukuza na kulinda haki za binadamu za watu wote wenye ulemavu, wakiwemo wale
wanaohitaji msaada maalum wa ziada;
(k)
Kuguswa kwamba, licha ya kuwepo kwa mikataba na
kuchukuliwa kwa hatua mbali mbali, bado watu wenye ulemavu wameendelea
kukabiliwa na vikwazo katika ushiriki wao kama wanajamii walio sawa na wengine
na haki zao za kibinadamu huvunjwa duniani kote,
(l)
Kutambua umuhimu
wa ushirikiano wa kimataifa katika kuboresha hali za maisha ya watu wenye
ulemavu katika kila nchi, hususan zile zinazoendelea,
(m)
Kutambua thamani
ya mchango unaotolewa na unaoweza kutolewa na watu wenye ulemavu katika
maendeleo ya jumla ya binadamu na uanuwai uliopo katika jumuiya zao, na kwamba
kwa kuhamasisha kunufaika kikamilifu na haki zao za binadamu, Uhuru wa msingi,
na ushiriki wao kikamilifu, kutawawezesha kujihisi kuwa sehemu ya jamii na kwa
kiwango kikubwa kuelekea kwenye hatua za maendeleo ya kibinadamu, kijamii na
kiuchumi na katika kutokomeza umaskini;
(n)
Kutambua umuhimu
wa watu wenye ulemavu kwa kila mmoja kujiamulia mambo mwenyewe binafsi na
kujitegemea ikiwa ni pamoja na uhuru wa kuchagua mwenyewe yale
anayoyataka;
(o)
Kuzingatia kwamba
watu wenye ulemavu wanapaswa kupata fursa ya kushirikishwa kikamilifu katika
michakato ya kufanya maamuzi yahusuyo sera na mipango mingine, ikiwa ni pamoja
na ile inayowahusu wao moja kwa moja;
(p)
Kuguswa na hali
mgumu wanazowakabili watu wenye ulemavu ambao wamekuwa waathirika wa aina mbali
mbali au zilizokithiri za ubaguzi kwa
misingi ya koo, rangi, jinsi, lugha, dini, siasa au itikadi nyinginezo, utaifa,
uzawa au sehemu atokayo mhusika, ukwasi, umri au hali nyinginezo;
(q)
Kutambua kuwa
wanawake na wasichana wenye ulemavu wanapokuwa nyumbani au nje ya nyumbani kila
wakati wako katika hatari kubwa zaidi ya kufanyiwa ukatili, kujeruhiwa au kudhalilishwa,
kutelekezwa au kuhudumiwa kizembe, kutendewa vibaya au kudhulumiwa;
(r)
Kutambua kuwa
watoto wenye ulemavu wanapaswa kunufaika kikamilifu na haki zote za binadamu na
uhuru wa msingi kwa kuzingatia usawa na watoto wengine, na kwa kukumbuka wajibu
wa jinsi hiyo uliochukuliwa na nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki
za Mtoto;
(s)
Kusisitiza
hitaji la kujumuisha
mtazamo wa jinsia katika jitihada zote za kuendeleza unufaikaji kamili wa haki
za binadamu na haki za msingi kwa watu wenye ulemavu;
(t)
Kuonyesha ukweli
kwamba watu wengi wenye ulemavu huishi katika hali ya umasikini, na kwa maana
hiyo, kutambua uhitaji mahususi wa kushughulikia athari mbaya za umaskini
kwa watu wenye ulemavu;
(u)
Kutafakari kwamba
hali ya amani na usalama unaozingatia kuheshimu kikamilifu madhumuni na kanuni
zilizoainishwa kwenye Hati ya Umoja wa Mataifa na uzingatiaji wa mikataba mbalimbali
ya haki za binadamu iliyopo kuwa ni ya lazima katika kuwalinda watu wenye
ulemavu, hususan, wakati wa mapambano ya silaha na kuvamiwa kimabavu na wageni;
(v)
Kutambua umuhimu
wa kuyafikia mazingira yanayoonekana, ya kijamii, ya kiuchumi na yale ya
kiutamaduni, kuifikia miundombinu ya kiafya na kielimu, na kuweza kupata habari
na mawasiliano, ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kunufaika kikamilifu na haki
zote za binadamu na Uhuru wa misingi;
(w)
Kutambua kuwa
kila mmoja, anao wajibu kwa wenzake na kwa jamii anamotoka anakabiliwa na
jukumu la kujibiidiisha kwa ajili ya kuendeleza na kutekeleza uzingatiaji wa
haki zinazotambuliwa kwenye Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu;
(x)
Kusadiki
kuwa familia ni kundi la kiasili, la msingi katika jamii na lenye
haki ya kulindwa na jamii na dola, na kwamba watu wenye ulemavu na familia zao
wanapaswa kupata ulinzi na msaada unaohitajika ili kuziwezesha (familia)
kuchangia kwa ukamilifu na kwa usawa katika unufaukaji na haki za watu wenye
ulemavu;
(y)
Kusadiki kuwa Mkataba wa Kimataifa wenye upeo mpana na
uliotengemaa wa kuendeleza na kulinda haki na hadhi ya watu wenye ulemavu
utatoa mchango wa maana katika kurekebisha mapungufu yanayowakabili watu wenye
ulemavu na kupanua ushiriki wao wa fursa sawa katika nyanja za kiraia, kisiasa,
kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, katika nchi zote zinazoendelea na
zilizoendelea,
Wamekubaliana kama ifuatavyo:
Ibara ya
1
Azma
Azma ya
Mkataba huu ni kuendeleza, kulinda na kuhakikisha upatikanaji mkamilifu na sawa
wa haki zote za binadamu na uhuru wa asili kwa
watu wote wenye ulemavu, na kukuza uheshimikaji wa hadhi yao ya asili.
Watu
wenye ulemavu ni pamoja na wale wenye udhoofu wa muda mrefu wa maumbile, akili
au fahamu ambao ukichangamana na vikwazo mbalimbali, vinaweza kuzuia ushiriki
wao kikamilifu na kimanufaa katika jamii kwa misingi ya usawa na watu wengine.
Ibara ya
2
Fasili
Kwa
madhumuni ya Mkataba huu:
“Mawasiliano”-Ni
neno lenye kujumuisha lugha mbalimbali, maonyesho ya matini, maandishi ya nukta
nundu, lugha ya kupapasa, maandishi yenye herufi nene, vyombo mbalimbali vya
habari vinavyopatikana, hali kadhalika na maandishi, sauti, lugha nyepesi, ving’amuzi
vya vitendo, teknolojia za kukuza mawimbi ya sauti na namna, njia na mitindo
mbadala ya kimawasiliano, ikijumuisha upatikanaji wa taarifa na teknolojia ya
mawasiliano.
“Lugha”- Ni neno linalojumuisha
lugha ya mazungumzo na lugha ya alama na aina nyingine za lugha zisizo za matamshi.
“Ubaguzi kwa misingi ya
ulemavu”-Ni neno linalomaanisha kutofautishwa kokote, kutengwa au kuzuiwa
kwa kwa sababu ya ulemavu ambako kuna azma
ya kudhoofisha au kubatilisha utambulisho, ufurahiaji au utekelezwaji wa haki
zote za kibinadamu na uhuru wa asili kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni,
kiraia au eneo lolote lile kwa misingi ya usawa na watu wengine. Ubaguzi ni
pamoja na aina zote za ubaguzi, ikijumuisha na kunyimwa marekebisho
stahili.
“Marekebisho
stahili”-Ni neno
linalomaanisha mabadilisho na marekebisho ya lazima na yafaayo bila kusababisha
taabu isiyowiana au isiyovumilika, pale yanapohitajika kutokana na hali fulani,
ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanafurahia au kutumia haki zote za
binadamu na uhuru wa msingi kwa kiwango sawa na wengine.
“Usanifu
kwa ajili ya wote”-Ni neno linalomaanisha
ubunifu wa bidhaa, mazingira, mipango na utoaji huduma unaoweza kutumiwa na watu
wote, kwa kiasi kikubwa kadri inavyowezekana, bila ya kuwepo haja ya kufanya
marekebisho au matengenezo maalum. “Usanifu kwa ajili ya wote” hauondoi umuhimu
wa kuwepo kwa nyenzo saidizi kwa ajili ya makundi maalum ya watu wenye ulemavu
pale ambapo zinahitajika.
Ibara ya 3
Kanuni za
Jumla:
Kanuni za a jumla za Mkataba huu zitakuwa ni:
(a)
Kuheshimu
hadhi ya asili, uhuru wa mtu binafsi ikiwa ni
pamoja na uhuru wa kufanya maamuzi yake mwenyewe, na
kujitegemea kwa watu;
(b)
Kutokubaguwa;
(c)
Ushiriki kamili na wa maana na ujumuishwaji katika jamii;
(d)
Kuheshimu tofauti na kuwakubali watu wenye ulemavu kuwa ni sehemu
ya tofauti miongoni mwa binadamu na ubinadamu
(e)
Usawa wa fursa;
(f)
Ufikikaji;
(g)
Usawa kati ya wanaume na wanawake;
(h)
Kuheshimu uwezo wa watoto wenye ulemavu unaokua na kuheshimu haki
za watoto wenye ulemavu na kuhifadhi utambulisho wao.
Ibara ya
4
Wajibu
wa Jumla
1.
Nchi Wanachama zinakubali kuhakikisha na kuendeleza upatikanaji
kamilifu wa haki zote za binadamu na uhuru wa msingi kwa watu wote wenye
ulemavu bila ubaguzi wa namna yoyote ile kwa misingi ya ulemavu. Ili kufikia azma hii, Nchi Wanachama zinakubali:
(a)
Kuchukua hatua zote zinazohitajika za kutunga sheria,
kiutawala na nyinginezo katika kutekeleza haki zilizotambuliwa
ndani ya Mkataba huu;
(b) Zitachukua hatua
zote zinazohitajika, zikiwemo za kisheria, kurekebisha au kufuta sheria
zilizopo, kanuni, mila na desturi ambazo zinaendekeza ubaguzi
dhidi ya watu wenye ulemavu;
(c) Zitazingatia ulinzi na uendelezaji wa haki
za binadamu kwa watu wenye ulemavu katika sera zote na mipango yote;
(d) Zitajizuia kujiingiza katika jambo lolote
lile linaloenda kinyume na Mkataba huu na kuhakikisha kuwa mamlaka na taasisi
za umma zinafanya kazi zao kwa kuzingatia Mkataba huu;
(e) Zitachukua hatua zote zinazofaa ili kuondoa
ubaguzi wa aina yoyote unaoweza kufanywa kwa misingi ya ulemavu na mtu yoyote,
jumuiya au kampuni binafsi;
(f) Zitafanya au kuendeleza tafiti na maendeleo
ya bidhaa, huduma, vifaa na nyenzo zilizosanifiwa kwa ajili ya wote kwa mujibu wa ibara ya 2 ya
Mkataba huu, ambavyo vitahitaji marekebisho madogo kadri invyowezekana na kwa
gharama nafuu ili kukidhi mahitaji maalum ya mtu mwenye ulemavu, kuhimiza
upatikanaji na matumizi yake, na kuhimiza usanifu kwa ajili ya wote wakati wa kuendeleza viwango
na miongozo.
(g) Zitafanya au kuendeleza tafiti, na kutengeneza
au kukuza upatikanaji na matumizi ya teknolojia mpya, ikiwa ni pamoja na
teknolojia ya habari na mawasiliano, zana za ujongeaji, nyenzo na teknolojia
saidizi, zinazowafaa watu wenye ulemavu, kwa kuzipa kipaumbele teknolojia zenye
gharama nafuu;
(h) Zitawajibika kutoa habari kwa watu wenye
ulemavu juu ya upatikanaji wa nyenzo za kujimudu kujongea, nyenzo na teknolojia
saidizi, ikijumuisha teknolojia mpya, pamoja na namna nyingine za usaidizi,
huduma za usaidizi na vifaa;
(i) Zitakuza mafunzo ya wataalam na watumishi
wanaoshughulika na watu wenye ulemavu juu ya haki zinazotambuliwa kwenye
Mkataba huu ili kuboresha utoaji misaada na huduma zinazohakikishwa na haki
hizo;
2. Kuhusu haki za kiuchumi, kijamii na
kiutamaduni, kila nchi iliyoridhia Mkataba huu itachukua hatua za kiwango cha
juu kwa kadri rasilimali zake zinavyoruhusu, na pale inapobidi, kufanya hivyo
katika mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, ili hatua kwa hatua kufanikisha
upatikanaji wa haki hizi kikamilifu, bila kuathiri wajibu uliopo ndani ya
Mkataba huu bila kupuuzia utekelezaji wa majukumu yaliyoainishwa na Mkataba huu
ambayo yanaanza kutumika mara moja kwa mujubu wa sheria za kimataifa.
3. Katika mchakato wa kutunga na kutekeleza
sheria na sera za kutekeleza Mkataba huu, na katika michakato mingine ya
kufanya maamuzi yanayohusu watu wenye ulemavu, waliouridhia
Mkataba huu watashauriana kwa karibu na kuwashirikisha watu wenye ulemavu,
ikiwa ni pamoja na watoto wenye ulemavu, kupitia jumuiya zinazowawakilisha.
4. Hapana jambo lolote ndani ya Mkataba huu
litakaloathiri ibara yoyote ambayo inachangia zaidi katika kufikia upatikanaji
wa haki za watu wenye ulemavu na ambayo imo katika sheria za waliouridhia
Mkataba huu au Sheria ya Kimataifa inayotumika katika nchi hiyo. Hapatakuwepo
vizuizi au kudharauliwa kwa haki zozote za binadamu na misingi ya uhuru ilizopo
kwa mujibu wa sheria, mikataba ya kimataifa au desturi katika nchi
yoyote ile iliyoridhia Mkataba kwa kisingizio kwamba Mkataba huu hautambui haki au uhuru
huo au kwamba zinatambuliwa kwa kiwango cha chini.
5. Masharti ya Mkataba huu yatatumika katika
maeneo yote ya nchi zenye mfumo wa shirikisho bila ya kuwepo mipaka au baadhi
ya vipengele kuachwa.
Ibara ya
5
Usawa na kutokubagua
1. Waliouridhia Mkataba huu wanatambua
kwamba watu wote ni sawa mbele na chini ya sheria na wanastahili kulindwa na
kunufaishwa na sheria kwa usawa bila ubaguzi wowote.
2. Waliouridhia Mkataba huu watapiga
marufuku aina zote za ubaguzi kwa misingi ya ulemavu na kubeba dhamana ya
kuhakikisha kwamba, watu wenye ulemavu wanapewa ulinzi sawa na imara wa
kisheria dhidi ya ubaguzi katika hali yoyote ile.
3. Ili kukuza usawa na kuondoa ubaguzi, waliouridhia
Mkataba huu watachukua hatua zinazohitajika ili kuhakikisha kuwa marekebisho
yanayostahili yanafanyika.
4. Hatua mahsusi ambazo ni za lazima katika
kuharakisha au kufanikisha kwa vitendo usawa kwa watu wenye ulemavu,
hazitochukuliwa kuwa ni ubaguzi chini ya masharti ya Mkataba huu.
Ibara ya
6
Wanawake wenye ulemavu
1. Waliouriudhia Mkataba huu wanatambua
kuwa wanawake na wasichana wenye ulemavu wanakabiliwa na aina nyingi za
ubaguzi, na kwa maana hiyo, zitachukua hatua ili kuhakikisha kuwa wananufaika
kikamilifu na haki zote za binadamu na uhuru wa msingi.
2. Nchi Wanachama zitachukua hatua zote
zinazofaa kuhakikisha maendeleo kamili, uendelezaji na uwezeshaji wa wanawake,
kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba wanapata na kufurahia haki za binadamu na
uhuru wa asili zilizoorodheshwa ndani ya Mkataba huu.
Ibara ya
7
Watoto wenye ulemavu
1. Waliouridhia Mkataba huu watachukua
hatua zote za lazima katika kuhakikisha kwamba watoto wenye ulemavu wananufaika
kikamilifu na haki zote za binadamu na uhuru wa msingi kwa kiwango sawa na
watoto wengine.
2. Katika matendo yote yanayowahusu watoto
wenye ulemavu, maslahi bora ya mtoto ndiyo yatakayozingatiwa.
3. Waliouridhia Mkataba huu watahakikisha
kwamba watoto wenye ulemavu wanayo haki ya kutoa maoni yao kwa uhuru juu ya
mambo yote yanayowahusu, mawazo yao yakipewa uzito unaostahiki kwa mujibu wa
umri na upevu wao, kwa misingi sawa na watoto wengine, na wapatiwe visaidizi
kwa kuzingatia aina ya ulemavu na umri wao ili kuipata haki hiyo.
Ibara ya
8
Kukuza Ufahamu
1. Waliouridhia Mkataba huu wamekubali
kuchukua hatua za haraka, madhubuti na zinazofaa katika:
(a) Kukuza ufahamu katika
jamii yote, ikiwemo ndani ya familia kuhusu watu wenye ulemavu, na kuendeleza
heshima, haki na hadhi ya watu wenye ulemavu;
(b) Kupambana dhidi ya
mazoea yaliyo ndani ya jamii, dharau, kinyongo na mienendo yenye madhara dhidi
ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na ile yenye kuegemea jinsi na umri
katika nyanja zote za maisha.
(c) Kuendeleza ufahamu
kuhusu uwezo na michango ya watu wenye ulemavu.
2. Hatua za
kufikia lengo hili ni pamoja na:
a) Kuanzisha na kuendeleza kampeni imara za
ufahamu wa umma zinazolenga:
(i) Kuhakikisha
haki za watu wenye ulemavu zinatambulika;
(ii) Kuendeleza elimu ya mapokeo ya haki za watu
wenye ulemavu;
(iii) Kukuza
utambuzi wa ujuzi, stahili na uwezo wa watu wenye ulemavu na mchango wao mahali
pa kazi na katika soko la ajira.
(b) Kuendeleza
katika ngazi zote za mfumo wa elimu, kadhalika miongoni mwa watoto wote tokea
wakiwa na umri mdogo, tabia ya kuheshimu haki za watu wenye ulemavu;
(c) Kuvihimiza
vyombo vyote vya habari kutangaza taswira ya watu wenye ulemavu kwa njia
zinazokubaliana na makusudio ya Mkataba huu;
(d) Kuhamasisha
uwepo wa programu za utambuzi kuwahusu watu wenye ulemavu na haki zao;
Ibara ya 9
Ufikikaji na upatikanaji
1. Katika kuwawezesha watu wenye ulemavu
waishi kwa
kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika nyanja zote za
maisha, waliouridhia Mkataba huu watachukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha kwamba watu
wenye ulemavu, sawa na watu wengine wanafika kwenye mazingira yaliyosanifiwa,
mfumo wa usafiri, habari na mawasiliano ikiwa ni pamoja na mifumo na teknolojia
ya habari, vifaa na huduma nyinginezo zilizo wazi na zitolewazo kwa umma mijini
na vijijini. Pamoja na mambo mengine, hatua hizi, zitajumuisha uainishaji na
uondoshaji wa mikingamo dhidi ya ufikikaji na utumikaji wa :
(a) Majengo, barabara, usafiri na vifaa vingine
nje na ndani ya shule, majengo ya umma miundombinu ya afya na mahali pa kazi;
(b) Habari, mawasiliano na huduma nyingine
ikijumuisha huduma za kielektoniki na zile za dharura;
2. Waliouridhia Mkataba huu pia watachukua hatua zinazofaa ili:
(a) Kuendeleza, kueneza na kufuatilia
utekelezaji wa viwango vya kawaida na miongozo kuhusu upatikanaji wa huduma kwa
ajili umma;
(b) Kuhakikisha kuwa taasisi zote binafsi
zinazotoa vifaa na huduma kwa ajili ya umma zinazingatia kuwa huduma zao
zinawafikia watu wenye ulemavu;
(c) Kutoa mafunzo kwa wadau juu ya matatizo ya
watu wenye ulemavu katika upatikanaji wa huduma;
(d) Kuweka ndani ya majengo na sehemu nyingine
zinazohudumia umma alama kwa maandishi ya Nukta Nundu na kwa njia nyingine
zinazosomeka na kueleweka kirahisi;
(e) Kutoa visaidizi halisi na wasaidizi, ikiwa
ni pamoja na waongozaji, wasomaji na wakalimani mabingwa wa lugha ya alama ili
kuwawezesha watu wenye ulemavu kuyafikia na kuyatumia majengo na huduma
nyinginezo kwa ajili ya umma;
(f) Kuhamasisha njia nyingine sadifu za usaidizi
ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata habari/taarifa;
(g) Kuhamasisha upatikanaji wa aina mpya za
teknolojia na mifumo ya habari na mawasiliano, ikiwa ni pamoja na intaneti kwa
ajili ya watu wenye ulemavu
(h) Kuhamasisha usanifu, uendelezaji, uzalishaji
na usambazaji wa teknolojia na mifumo ya habari na mawasiliano ili zipatikane
kwa gharama nafuu.
Ibara ya 10
Haki ya Kuishi
Waliouridhia Mkataba huu wanasisitiza kuwa kila binadamu anayo haki ya
asili ya kuishi na zitachukua hatua za makusudi ili kuhakikisha kwamba haki
hiyo inafurahiwa kwa ukamilifu na watu wenye ulemavu kwa misingi iliyo sawa na
watu wengine.
Ibara ya 11
Hali za hatari na dharura
Waliouridhia Mkataba huu watachukua hatua za makusudi, kulingana na wajibu
unaobainishwa chini ya Sheria ya Kimataifa, ikijumuisha Sheria ya Kimataifa ya
Misaada ya Kibinadamu na Sheria ya Kimataifa ya Haki za Binadamu katika
kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watu wenye ulemavu wakati wa hali ya hatari,
ikiwa ni pamoja na mazingira ya mapigano ya silaha, dharura za kibinadamu na
matukio ya majanga ya asili.
Ibara ya 12
Kutambuliwa kwa usawa mbele ya Sheria
1. Waliouridhia
Mkataba huu wanasisitiza kwamba watu wenye ulemavu wana
haki ya kutambuliwa mahali popote kama watu mbele ya sheria.
2. Waliouridhia
Mkataba huu watatambua kwamba watu wenye ulemavu
wanafurahia kuwa na uwezo wa kisheria kwa misingi ya usawa na watu wengine
katika nyanja zote za kimaisha.
3. Waliouridhia
Mkataba huu watachukua hatua zinazofaa ili kuwawezesha
watu wenye ulemavu kupata msaada wa kisheria watakaouhitaji katika kutekeleza
uhalali wao wa kisheria.
4. Waliouridhia Mkataba huu watahakikisha kwamba hatua zote zinazohusiana na uhalali
wa kutenda kisheria zina kinga zinazofaa kuzuia matumizi mabaya kwa mujibu wa
sheria ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Kinga za aina hii zitahakikisha
kuwa hatua zinazohusiana na uhalali wa kutenda kisheria zinaheshimu haki,
utashi na upendeleo wa mtu, hazina mgongano wa kimaslahi na ushawishi
usiostahili, zinawiana na kuendana na hali ya mhusika, zinatumika katika muda
mfupi kadri inavyowezekana na zinapitiwa mara kwa mara na mamlaka
zinazojitegemea, zenye uwezo na adili au chombo cha kimahakama. Kinga hizo
zitawiana na kiwango ambacho hatua hizo huathiri haki na maslahi ya mhusika.
5. Kwa mujibu wa masharti ya ibara hii, Waliouridhia
Mkataba huu watachukua hatua zote zinazofaa na madhubuti katika kuhakikisha
kwamba watu wenye ulemavu wana haki sawa ya kumiliki au kurithi mali, kusimamia
mambo yao ya kifedha na haki sawa ya kupata mikopo ya kibenki, uwekaji rehani
na njia nyinginezo za mikopo, na zitahakikisha kwamba watu wenye ulemavu
hawanyang’anywi mali zao kiholela.
Ibara ya 13
Upatikanaji wa haki:
1. Waliouridhia Mkataba watahakikisha
upatikanaji wa haki stahiki kwa watu wenye ulemavu katika misingi ya usawa na watu wengine, ikijumuisha
marekebesho ya vipengele vya utaratibu wa kiuendeshaji yanayozingatia umri, ili
kufanikisha jukumu lao kama washiriki wa moja kwa moja au wasiyo wa moja kwa
moja na kuwa mashahidi katika mienendo yote ya kesi na katika hatua za
upelelezi na hatua nyingine za awali.
2. Ili kusaidia kuhakikisha upatikanaji wa
haki kwa watu wenye ulemavu, Waliouridhia
Mkataba huu watatoa mafunzo kwa wale wanofanya kazi
katika tasnia ya utoaji haki wakiwemo polisi na wafanyakazi wa magereza.
Ibara ya 14
Uhuru na Usalama wa mtu
1. Waliouridhia Mkataba watahakikisha kuwa, katika misingi ya usawa na wengine,
wale wenye ulemavu nao:
(a) Wanafurahia haki ya uhuru na usalama wa mtu;
(b) Hawapokonywi
uhuru wao kinyume cha sheria au kiholela, na kwamba ikibidi kupokonywa uhuru
wao, basi iwe ni kwa mujibu wa sheria, na kwamba kuwa na ulemavu kwa namna
yoyote ile hakutohalalisha kupokonywa kwa uhuru.
2. Waliouridhia
Mkataba huu watahakikisha kwamba, ikiwa watu wenye
ulemavu kwa njia yoyote ile wamepokonywa uhuru wao, basi kwa msingi sawa na
wengine, wana haki ya kuhakikishiwa uhuru wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa
za haki za binadamu na watatendewa kwa mujibu wa malengo na misingi ya Mkataba
huu, ikijumuisha na kipengele cha marekebisho yanayostahili.
Ibara ya 15
Uhuru wa
kutoteswa, au kudhalilishwa
1. Hapana mtu atakayewekwa katika hali ya
mateso au udhalimu, kutendewa au kuadhibiwa kinyume cha ubinadamu,
kiudhalilishaji au kikatili. Kwa namna yoyote ile, hakuna mtu atakayefanyiwa
majaribio ya kitabibu au kisayansi bila yeye kuridhia kwa uhuru.
2. Nchi Wanachama zitachukua hatua
madhubuti za kisheria, kiutawala, kijamii, kielimu na hatua nyingine ili
kuwalinda watu wenye ulemavu katika misingi ya usawa na watu wengine, ili
wasiteswe, wasifanyiwe udhalimu, kudhalilishwa kinyume cha ubinadamu.
Ibara ya 16
Kutonyonywa,
kutofanyiwa ukatili na kutodhalilishwa
1. Waliouridhia
Mkataba huu watachukua hatua stahiki za kisheria,
kiutawala, kijamii, kielimu na hatua nyingine ili kuwalinda watu wenye ulemavu
nje na ndani ya familia zao dhidi ya vitendo vya kinyonyaji, kikatili na
kidhalilishaji, ikiwa ni pamoja na upendeleo wa kijinsia.
2. Waliouridhia
Mkataba huu pia watachukua hatua madhubuti ili kuzuia
aina zote za unyonyaji, ukatili na udhalilishaji kwa kuhakikisha pamoja na mambo
megine kuwepo kwa mifumo stahiki ya usaidizi inayozingatia jinsia na makundi
rika ya watu wenye ulemavu, familia na
walezi wao, ikijumuisha utoaji habari na elimu kuhusu mbinu za uzuiaji,
kutambua na kuyatolea taarifa matendo ya kinyonyaji, kikatili na
kidhalilishaji. Waliouridhia Mkataba huu watahakikisha kwamba huduma za kinga zinatilia maanani
unyeti wa masuala ya umri, jinsia, na ulemavu.
3. Ili kuzuia
aina zozote za kinyonyaji, kikatili, na kidhalilishaji, Waliouridhia Mkataba huu, watahakikisha kwamba nyenzo na mipango ambayo inalenga
kuwahudumia watu wenye ulemavu, inasimamiwa kimadhubuti na mamlaka zilizo huru.
4. Waliouridhia
Mkataba huu, watachukua hatua madhubuti kuendeleza watu
wenye ulemavu walioathiriwa kwa namna yoyote ile kutokana na kunyonywa,,
kufanyiwa ukatili au kudhalilishwa, kwa kuwapatia ahueni kimwili, kiakili na
kisaikolojia kwa njia ya kuwatengemaza na kuwarejesha kwenye jamii na hata kwa
njia ya huduma za kinga. Ahueni hiyo na urejeshaji katika hali ya kawaida
utafanyika katika mazingira yatakayoimarisha afya, ustawi, heshima, hadhi na
uhuru wa mtu na utazingatia mahitaji ya kijinsia na ya makundi rika.
5. Waliouridhia
Mkataba huu watatunga sheria na sera madhubuti,
ikijumuisha sheria na sera zenye kuwalenga wanawake na watoto ili kuhakikisha
matukio ya kinyonyaji, kikatili na kidhalilishaji dhidi ya watu wenye ulemavu
yanabainishwa, yanafanyiwa upelelezi na, inapobidi, kuyafungulia mashtaka.
Ibara ya 17
Kuheshimu tofauti za kimaumbile
Kila mtu mwenye ulemavu anayo haki ya kuheshimiwa kwa ukamilifu
wake kimwili na kiakili kwa misingi ya usawa na watu wengine.
Ibara ya 18
Uhuru wa mtu kwenda atakapo na kuwa na utaifa
1. Waliouridhia
Mkataba huu wanatambua haki za watu wenye ulemavu za kuwa
huru kwenda popote watakapo, uhuru wa kuchagua makazi yao na utaifa kwa misingi
iliyo sawa na watu wengine, ikijumuisha kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu:
(a) Wanayo
haki ya kapata na kubadili utaifa na kutopokonywa utaifa wao kiholela au kwa
misingi ya ulemavu wao;
(b) Hawanyimwi,
kwa misingi ya ulemavu walio nao, uwezo wa kupata, kumiliki na kutumia hati za
utaifa wao au hati nyingine za utambulisho, au kutumia michakatao stahiki kama vile
taratibu za uhamiaji, kwa kadri zinavyoweza kuhitajika ili kuwawezesha kutumia
haki yao ya uhuru wa kwenda watakapo.
(c) Wapo
huru kuihama nchi yoyote ile, hii ikiwa ni pamoja na nchi yao ya asili;
(d) Hawanyimwi,
kiholela au kwa msingi wa ulemavu walio nao, haki ya kuingia/kurudi kwenye nchi
yao ya asili .
2. Watoto wenye
ulemavu watasajiliwa mara baada ya kuzaliwa na watakuwa na haki, toka
wanapozaliwa ya kupewa jina, haki ya kupata utaifa na kwa kadri itavyowezekana,
haki ya kuwatambua na kulelewa na wazazi wao.
Ibara ya 19
Kuishi kwa kujitegemea na Kujumuishwa katika jamii
Waliouridhia Mkataba wanatambua haki sawa kwa watu wote wenye ulemavu kuishi
katika jamii, wakiwa na maamuzi sawa na watu wengine, na zitachukua hatua za
makusudi katika kuwawezesha kufurahia haki hii kikamilifu, kujumuishwa na kushiriki
kikamilifu katika shughuli za kijamii, ikiwa ni pamoja na na kuhakikisha
kwamba:
(a) Watu wenye
ulemavu wanapata fursa ya kuchagua makazi yao, wataishi wapi na wataishi na
nani kwa misingi iliyo sawa na watu wengine na hawalazimiki kuishi katika mfumo
maalum ulioandaliwa;
(b) Watu wenye
ulemavu wanapata huduma za aina mbalimbali nyumbani, kwenye eneo wanapoishi na
huduma nyinginezo za kijamii zikijumuisha misaada binafsi ambayo ni ya lazima katika
kuwawezesha kuishi na kujumuika kwenye jamii, na kuishi bila kutengwa au kubaguliwa
na jamii inayowazunguka;
(c) Huduma za
kijamii na miundombinu kwa ajili ya umma, inapatikana kwa watu wenye ulemavu
kwa misingi ya usawa na inaendana na mahitaji yao.
Ibara ya 20
Matembezi binafsi
Waliouridhia Mkataba huu watachukua hatua madhubuti za kuhakikisha kuwa watu
wenye ulemavu wanajitegemea kwa kadri inavyowezekana katika kumudu kutembea
ikiwa ni pamoja na:
(a) Kumwezesha
mtu binafsi mwenye ulemavu kutembea kwa namna na wakati anaotaka mwenyewe na
kwa gharama atakayoimudu;
(b) Kuwawezesha
watu wenye ulemavu kupata nyenzo bora za kujimudu, vifaa na teknolojia saidizi
na aina nyingine ya usaidizi wa viumbe hai (wanadamu na wanyama) na vijumbe,
ikijumuisha kuwezesha upatikanaji wake kwa gharama watakayoimudu;
(c) Kutoa mafunzo
ya stadi za kutembea kwa watu wenye ulemavu na kwa watalaam wanaofanya kazi na
watu wenye ulemavu;
(d) Kuzihimiza
asasi zinazotengeneza nyenzo za kutembelea, vifaa na teknolojia saidizi
kuzingatia vipengele vyote vya watu wenye ulemavu kumudu kutembea.
Ibara ya 21
Uhuru wa kujieleza, kutoa maoni na kupata habari
Waliouridhia Mkataba huu watachukua hatua zinazofaa katika kuhakikisha kwamba watu
wenye ulemavu wanatumia haki ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, ikijumuisha
uhuru wa kutafuta, kupata na kutoa habari na mawazo yao kwa misingi iliyo sawa
na watu wengine na kwa kutumia aina zote za mawasiliano wanazozichagua, kama
ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 2 ya Mkataba huu, ikiwa ni pamoja na:
(a) Habari
zinazoulenga umma kuwafikia watu wenye ulemavu kwa njia wanazoweza kupokelea
taarifa na teknolojia sadifu kwa aina mbalimbali za ulemavu bila kuchelewa wala
kuingia gharama za ziada;
(b) Kurasimisha
na kuwezesha matumizi ya lugha ya alama, maandishi ya nukta nundu, nyenzo za
kukuza mawimbi ya sauti na mawasiliano mbadala na aina nyinginezo zinazofikika,
mifumo na aina za mawasiliano watakayoamua kutumia watu wenye ulemavu katika
mawasiliano rasmi;
(c) Kuzihimiza
taasisi binafsi zinazohudumia umma, ikijumuisha njia za intaneti, kutoa habari
na huduma kwa njia na mifumo itayowawezesha watu wenye ulemavu kuzifikia na kuzitumia
huduma hizo;
(d) Kuvihimiza
vyombo vya habari, ikijumuisha na wanaosambaza habari kupitia intaneti,
kuzifanya huduma zao kuweza kufikiwa na watu wenye ulemavu;
(e) Kutambua na
kuendeleza matumizi ya lugha za alama.
Ibara ya 22
Kuheshimu
faragha
1. Hapana mtu
mwenye ulemavu, bila kujali sehemu anayoishi au mpangilio wa makazi, ambaye
faragha, familia, nyumba, maandishi yake ama aina nyingine za mawasiliano, vitaingiliwa
kiholela au kinyume cha sheria ambapo hadhi na sifa zake vitajeruhiwa. Watu
wenye ulemavu wana haki ya kulindwa kisheria dhidi ya kuingiliwa kwa aina ile
au kushambuliwa kinyume cha sheria.
2. Waliouridhia
Mkataba huu watalinda faragha ya taarifa binafsi, afya
na marekebisho ya watu wenye ulemavu kwa misingi ya usawa na watu wengine.
Ibara ya
23
Kuheshimu
maisha ya kifamilia na familia
1. Nchi zilizoridhia Mkataba huu, zitachukua
hatua madhubuti ili kukomesha ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu katika
masuala yote ya ndoa, familia, uzazi na mahusiano ya kimapenzi kwa misingi ya usawa
na wengine na kuhakikisha kwamba:
(a) Haki
ya watu wote wenye ulemavu waliofikia umri wa kufunga ndoa, na kuanzisha
familia kwa misingi huru na ridhaa ya wahusika inatambuliwa;
(b) Haki za watu wenye ulemavu kuamua kwa uhuru
na kiuwajibikaji, idadi na mpangilio wa uzazi na kupata taarifa zinazowafaa
wanarika, elimu ya uzazi na mpango wa uzazi inatambuliwa, na njia muhimu za
kuwawezesha kuzitumia haki hizi zinatolewa;
(c) Watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na
watoto, wanabaki na kizazi kwa misingi iliyo sawa na watu wengine.
2. Waliouridhia Mkataba
huu watahakikisha kuwa, haki na dhamana za watu wenye
ulemavu kuhusiana na masuala ya ulezi, ulinzi, udhamini, kuasili watoto na hali
kama hizo, au taasisi kama hizo, ambapo maudhui kama
haya yamo kwenye sheria za nchi, kwa vyovyote vile maslahi ya mtoto ndiyo
yatakayopewa umuhimu. Waliouridhia Mkataba watatoa
msaada unaofaa kwa watu wenye ulemavu katika kutekeleza jukumu lao la kulea
watoto wao.
3. Waliouridhia Mkataba huu watahakikisha
kwamba watoto wenye ulemavu wanakuwa na haki sawa kuhusu maisha ya kifamilia. Ili kuzipata haki hizi, na kuzuia ufichaji, utupaji
utelekezaji na ubaguzi wa watoto wenye ulemavu, Waliouridhia Mkataba
huu watatoa taarifa mapema na kwa ukamilifu, kuhusu huduma na msaada
kwa watoto wenye ulemavu na familia zao.
4. Waliouridhia Mkataba huu watahakikisha
kwamba mtoto hataondoshwa kwa wazazi wake bila ya ridhaa yake, isipokuwa pale
ambapo mamlaka yenye dhamana ya kufanya hivyo kwa kupitia chombo cha mahakama,
itakapoamua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa, kwamba kuondoshwa
huko ni kwa lazima na ni kwa maslahi ya mtoto. Kwa vyovyote vile, mtoto
hataondoshwa kwa wazazi wake kwa misingi ya ulemavu, uwe wa mtoto mwenyewe,
mmoja kati ya wazazi wake au wazazi wote wawili.
5. Waliouridhia Mkataba huu watafanya
kila jitihada, endapo famlia haiwezi kumlea mtoto mwenye ulemavu, kumpatia
malezi mbadala ndani ya familia pana, na hilo
likishindikana, basi ndani ya jamii katika mazingira ya kifamilia.
Ibara ya
24
Elimu
1. Waliouridhia Mkataba huu, wanatambua
haki za watu wenye ulemavu kupata elimu. Ili haki hii ipatikane bila ya ubaguzi
na kwa misingi ya usawa wa fursa, Waliouridhia Mkataba, watahakikisha
kuwepo kwa mfumo wa elimu jumuishi katika ngazi zote na mfumo wa ujifunzaji kwa
maisha yote ukijielekeza kwenye:
(a) Uendelezaji kamili wa uwezo wa binadamu na
uzingatiaji wa hadhi na kujithamini, kuimarisha hali ya kuheshimu haki za
binadamu, uhuru wa kujiamulia na uanuwai miongoni mwa binadamu.
(b) Watu wenye ulemavu kujiendeleza kadri
wawezavyo kihaiba, kivipawa na kiubunifu, kadhalika na uwezo wao kiakili na
kimwili;
(c)
Kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki ipasavyo katika jamii iliyo huru.
2. Ili haki
hii ipatikane, Waliouridhia Mkataba huu watahakisha kwamba:
(a) Mfumo wa elimu
hauwatengi watu wenye ulemavu na
kwamba
watoto wenye ulemavu hawabaguliwi kwenye elimu ya msingi ambayo ni ya lazima au
ile ya sekondari kwa misingi ya ulemavu;
(b) Watu wenye ulemavu
wanaweza kuipata elimu ya msingi na ya sekondari katika mfumo jumuishi, bora na
bila ya malipo kwa misingi ya usawa na wengine katika jamii waishimo.
(c) Marekebisho stahili
yanafanyika kulingana na mahitaji binafsi;
(d) Watu wenye ulemavu
wanapata usaidizi unaohitajika ndani ya mfumo wa elimu, ili kuwawezesha
kuelimika vilivyo;
(e) Hatua za makusudi za
kumuwezesha mtu binafsi mwenye ulemavu zinachukuliwa katika mazingira
yanayomuwezesha kufikia upeo wa maendeleo ya kitaaluma na kijamii kama lilivyo lengo la ujumuishaji kamilifu;
3. Nchi zilzoridhia
Mkataba huu, zitawawezesha watu wenye ulemavu kujifunza maishani na stadi za
kimaendeleo katika jamii ili kurahisisha ushiriki wao ulio kamilifu katika nyanja
ya elimu na kama wanajamii wengine. Ili kufikia lengo hili, Waliouridhia Mkataba
huu watachukua hatua zinazofaa, zikijumuisha:
a) Kuwezesha mafunzo
ya maandishi ya nukta nundu, maandishi mbadala na njia za kukuza mawimbi
ya sauti na nyinginezo za kuboresha mawasiliano, mbinu kabilifu za ujongeaji,
na kuwezesha huduma za makundi rika na ushauri;
b) Kuwezesha mafunzo ya
lugha ya alama na kukuza utambulisho wa kiisimu wa jamii ya viziwi;
c) Kuhakikisha kwamba
elimu kwa watu wenye ulemavu, hususan watoto wasioona, viziwi au viziwi
wasioona, inatolewa kwa lugha, mfumo na njia sadifu za kimawasiliano, na katika
mazingira yatakayotoa nafasi kubwa ya maendeleo kitaaluma na kijamii.
4. Ili
kusaidia katika kuhakikisha upatikanaji wa haki hii, Waliouridhia
Mkataba huu watachukua hatua madhubuti katika, kuajiri walimu, wakiwemo
walimu wenye ulemavu, walio na utaalamu wa lugha ya alama na/au nukta nundu na
pia kuwafundisha wataalamu na watumishi katika ngazi zote za elimu. Mafunzo
kama hayo yatajumuisha mwamko kuhusu ulemavu na kutumia njia za kukuzia mawimbi
ya sauti na zile mbadala kimawasiliano, mbinu na vifaa vya kimafunzo
vitakavyowasaidia watu wenye ulemavu.
5 Waliouridhia Mkataba huu, watahakikisha
kwamba watu wenye ulemavu wanapata elimu ya juu, mafunzo ya ufundi, elimu ya
watu wazima na mafunzo wakati wote wa maisha yao bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kuipata
kwa misingi sawa na watu wengine. Ili kufikia hatua hii, Waliouridhia
Mkataba huu watahakikisha kwamba marekebisho stahiki yanafanyika kwa ajili ya
watu wenye ulemavu.
Ibara ya
25
Afya
Waliouridhia
Mkataba huu wanatambua kwamba watu wenye ulemavu wanayo haki ya kunufaika kwa
kiwango cha juu cha huduma za afya kinachoweza kupatikana bila ya ubaguzi
wowote kwa misingi ya ulemavu. Nchi Wanachama zitachukua hatua zote
zinazostahiki katika kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata huduma za
afya zenye kuzingatia jinsia, ikiwa ni pamoja na zinazohusiana na
utengamanisho. Kwa makusudi kabisa Nchi Wanachama:
(a) Zitawapatia watu wenye ulemavu matibabu ya
aina, ubora na viwango vile vile vya huduma na mipango ya afya isiyo na/au
yenye gharama nafuu kama zinavyotolewa kwa watu wengine, zikijumuisha maeneo ya
afya ya uzazi na ile iliyojikita kwenye idadi ya watu na mipango ya elimu ya
afya kwa umma.
(b) Zitatoa huduma za afya zinazohitajika kwa
watu wenye ulemavu hasa kutokana na ulemavu wao, ikijumuisha utambuzi wa mapema
na kuanzisha afua stahiki na huduma zenye lengo la kupunguza na kuzuia ulemavu
zaidi miongoni mwa watoto na watu wazima.
(c) Zitatoa huduma hizo katika maeneo ya karibu
na jamii za watu kadri inavyowezekana, yakiwemo maeneo ya vijijini;
(d) Zitawataka wataalamu wa afya kutoa huduma za
kiwango sawa kwa watu wenye ulemavu kama zinavyotolewa kwa watu wengine, ikiwa
ni pamoja na misingi ya kutoa ridhaa kwa uhuru na ufahamu wa kutosha kadhalika
na kuongeza ufahamu wa masuala ya haki za binadamu, hadhi, uhuru na mahitaji ya
watu wenye ulemavu kwa njia ya mafunzo na kutangaza viwango vya maadili ya
kitabibu kwa taasisi za umma na za binafsi.
(e) Zitakataza ubaguzi dhidi ya watu wenye
ulemavu katika utoaji wa bima za afya, na bima za maisha pale ambapo bima kama hizo zinaruhusiwa kisheria katika nchi husika;
ambapo zitatolewa kwa misingi ya haki na namna inayofaa.
(f) Zitazuia kumkatalia mtu matibabu na huduma
za kiafya kibaguzi au kumnyima chakula na vinywaji kwa misingi ya ulemavu.
Ibara ya
26
Marekebisho
na utengamao
1. Waliouridhia Mkataba huu watachukua
hatua madhubuti na sadifu ikiwa ni pamoja na kwa njia ya wanarika kusaidiana,
kumuwezesha mtu mwenye ulemavu kufikia na kuendeleza hali ya kujitegemea,
kupata uwezo wa kimwili, kiakili, kijamii na kiufundi, pia na kujumuika katika
masuala yote ya maisha. Ili kufikia lengo
hili, Waliouridhia Mkataba huu wataandaa, kuimarisha na kupanua
huduma za marekebesho na utengamao hususani katika nyanja za afya, ajira, elimu
na huduma za kijamii kiasi kwamba huduma na programu:
a) Zianze katika hatua za awali kadri
itavyowezekana, na zipanue wigo wa upimaji ili kugusa mahitaji na uwezo wa
mhusika binafsi;
b) Zinasaidia ushiriki na ujumuishwaji wa
wahusika katika jamii na kwenye masuala yote ya jamii, ni za hiari na kwa`kadri
inavyowezekana, zinawafikia watu wenye ulemavu katika maeneo yaliyo karibu na
jamii zao, ikiwa ni pamoja na maeneo ya vijijini;
2. Nchi Wanachama zitakuza maendeleo ya awali
na kuendelea kutoa mafunzo kwa ajili ya wataalamu na watumishi wanaofanyakazi
katika fani za marekebisho na utengamao;
3. Nchi Wanachama zitakuza upatikanaji maarifa
na matumizi ya vifaa saidizi na teknolojia vilivyosanifiwa kwa ajili ya watu
wenye ulemavu kwa kadri vinavyohusiana na marekebisho na utengamanisho.
Ibara ya
27
Kazi na
Ajira
Waliouridhia
Mkataba huu, wanatambua haki ya watu wenye ulemavu kuajiriwa na kufanya kazi
kwa misingi sawa na wengine. Hii inajumuisha haki ya fursa ya kujipatia riziki
kwa kufanya kazi walizozichagua au kuzikubali wao wenyewe katika soko la ajira,
na mazingira yaliyo wazi, jumuishi na yanayofikika kwa watu wenye ulemavu. Waliouridhia
Mkataba huu watalinda na kukuza ufanikishaji wa haki ya kufanya kazi,
ikijumuisha wale wanaopata ulemavu wakiwa kazini, kwa kuchukua hatua zinazofaa,
ikiwa ni pamoja na sheria ili kuweza:
(a) Kukataza ubaguzi kwa msingi wa ulemavu
katika mambo yote yanayohusu aina zote za kazi, ikijumuisha masharti ya
kuajiri, uajiri na ajira, kudumu kazini, kupandishwa daraja na mazingira ya
kazi yaliyo salama kiafya.
(b) Kulinda haki za watu wenye ulemavu, kwa
misingi ya usawa na wengine, masharti ya kazi yaliyo adilifu na ya kufaa,
ikijumuisha fursa sawa na malipo sawa kwa kazi iliyo na uzito ule ule,
mazingira ya kufanyia kazi yaliyo salama kiafya ikiwa ni pamoja na kulindwa
dhidi ya manyanyaso, na kusuluhisha migogoro;
(c) Kuhakikisha kwamba
watu wenye ulemavu wanaweza kutumia haki zao mahali pa kazi na vyama huru vya
wafanyakazi kwa misingi sawa na wengine.
(d) Kwa namna inayofaa, watu wenye ulemavu
kunufaishwa na programu zinazohusiana na teknolojia ya jumla na ushauri wa
kiufundi, huduma za mafunzo kazini, na ya kiufundi na mengineyo endelevu.
(e) Kuongeza fursa za ajira na kupandishwa
madaraja kwa watu wenye ulemavu katika soko la ajira, pamoja na kusaidiwa,
kupata, kudumishwa na kurejeshwa kazini.
(f) Kuimarisha na kukuza fursa za watu wenye
ulemavu kujiajiri wenyewe, kuanzisha na kuendesha shughuli za ujasiriamali,
kuanzisha vyama vya ushirika na mtu binafsi kujianzishia biashara zake;
(g) Kuajiri watu
wenye ulemavu katika sekta ya umma;
(h) Kukuza hali
ya watu wenye ulemavu kuajiriwa katika sekta binafsi kwa kuwa na sera na
mipango mingine inayofaa ikiwa ni pamoja na ile sera ikibali, utoaji motisha na
afua nyinginezo;
(i) Kuhakikisha
kwamba marekebisho stahiki yanafanyika mahali pa kazi kwa ajili ya watu wenye
ulemavu;
(j) Kukuza
upatikanaji wa uzoefu wa watu wenye ulemavu katika soko wazi la ajira;
(k) Kukuza
mafunzo ya kitaaluma na stadi za kiufundi, kudumu kazini na mipango maalum ya
watu wenye ulemavu kurudishwa kazini.
2. Waliouridhia Mkataba huu, watahakikisha kwamba watu wenye ulemavu hawafanywi
watumwa au watwana na wanalindwa kwa misingi ya usawa na watu wengine dhidi ya
ajira za kushurutishwa au za lazima.
Ibara ya
28
Ubora wa
maisha na hifadhi ya kijamii
1. Waliouridhia Mkataba huu wanatambua
haki ya watu wenye ulemavu ya kupata maisha bora wao wenyewe na familia zao,
ikiwa ni pamoja na chakula , mavazi na makazi, na muendelezo wa hali bora ya
maisha, na zitachukua hatua mathubuti kulinda na kuendeleza upatikanaji wa haki
hii bila ya ubaguzi kwa misingi ya ulemavu.
2. Waliouridhia
Mkataba huu wanatambua haki ya watu wenye ulemavu kupata hifadhi ya kijamii
na kufaidika na haki hiyo bila ya ubaguzi kwa msingi wa ulemavu, na zitachukua
hatua stahiki katika kulinda na kukuza haki hiyo ikijumuisha hatua kama vile:
(a) Kuhakikisha kwamba huduma za maji safi, na kuhakikisha
kwamba huduma zinazofaa na zenye gharama nafuu, visaidizi na usaidizi mwingine
unaohusiana na mahitaji ya ulemavu zinawafikia watu wenye ulemavu kwa misingi
ya usawa;
(b) Kuhakikisha kwamba mipango ya hifadhi ya
jamii na ile ya kupunguza umasikini inawafikia watu wenye ulemavu, hususan,
wanawake, wasichana na wazee wenye ulemavu;
(c) Kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu na
familia zao wanaoishi katika hali ya umasikini wanapata huduma moja kwa moja
kutoka serikalini, ikiwa ni pamoja na gharama zinazohusiana na ulemavu kama
vile mafunzo ya kutosha, ushauri nasaha, ruzuku na matunzo wakati wa fadhaa zinazotokana
na ulemavu, maumivu na msendeko.
(d) Kuhakikisha kwamba
programu za umma za makazi zinawafikia watu wenye ulemavu;
(e) Kuhakikisha kwamba
programu za mafao ya uzeeni zinawafikia watu wenye ulemavu katika misingi ya
usawa.
Ibara ya 29
Kushiriki katika Siasa na Kuhudumia Umma
Waliouridhia Mkataba huu wanawahakikishia watu wenye ulemavu haki za kisiasa na
fursa ya kunufaika na haki hizo kwa misingi ya usawa na watu wengine, na
zitachukua hatua za:
(a) Kutoa hakikisho kuwa watu wenye ulemavu
wanaweza kushiriki kwa ukamilifu katika medani ya siasa na huduma kwa umma kwa
misingi iliyo sawa na wengine moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi
waliochaguliwa kwa misingi huru, ikiwa ni pamoja na fursa ya watu wenye ulemavu
kupiga kura na kuchaguliwa, pamoja na mengine kwa:
(i) Kuhakikisha kwmba utaratibu wa kupiga kura,
vifaa na nyenzo ni sadifu, vinafikika, na vinaeleweka na kutumika kwa urahisi;.
(ii) Kulinda
haki ya watu wenye ulemavu kupiga kura kwa siri wakati wa uchaguzi na bila kudhalilishwa, na
kugombea, kuchukua dhamana za uongozi na kutekeleza masuala yote ya umma katika
ngazi zote za serikali, kuwezesha matumizi ya visaidizi na teknolojia mpya kama
itavyoonekana inafaa;
(iii) Kutoa
hakikisho la uhuru wa maoni kwa watu wenye ulemavu kama wapiga kura, na katika
kulifanya hili liwezekane pale inapobidi, mhusika ataomba, na kuruhusiwa
kusaidiwa kupiga kura yake na mtu aliyemteua mwenyewe;
(b) Kukuza
mazingira ambamo watu wenye ulemavu wanaweza kushiriki kikamilifu katika
masuala ya umma bila ya ubaguzi, na kwa misingi ya usawa na wengine, na
kuhimiza ushiriki wao katika mambo ya umma, ikijumuisha:
(i) Kushiriki
katika asasi za kiraia na zile zinazojihusisha na masuala ya umma na siasa za
nchi, na katika shughuli na uongozi wa vyama vya siasa;
(ii) Kuunda
na kujiunga na vyama vya watu wenye ulemavu ili kuwawakilisha katika ngazi za
kimataifa, kitaifa, kikanda na kimitaa.
Ibara ya 30
Kushiriki katika masuala ya kitamaduni, mapumziko,
burdani na michezo
1. Waliouridhia Mkataba huu wanatambua haki ya watu wenye ulemavu kushiriki kwa
msingi wa usawa na watu wengine katika mambo ya kitamaduni, na zitachukua hatua
zinazofaa ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu:
(a) Wanafaidika
na fursa za kupata vifaa vya kitamaduni kwa njia zinazofikika;
(b) Wanafaidika
na vipindi vya televisheni, filamu, michezo ya kuigiza na shughuli nyingine za
kitamaduni kwa njia anuwai zinazowafaa.
(c) Wanafaidika
bila vikwazo, sehemu zinapofanyikia shughuli au huduma za kitamaduni kama vile
kumbi za maonyesho, makumbusho, sinema, maktaba na huduma za kitalii, na kadri
inavyowezekana, kuyafikia majengo ya kihistoria, na sehemu nyingine umuhimu kwa
utamaduni wa jamii.
2. Waliouridhia Mkataba huu watachukua hatua zinazofaa kuwawezesha watu wenye ulemavu
kuwa na fursa ya kujiendeleza na kutumia ubunifu, usanii na uwezo wao kiakili,
siyo tu kwa manufaa yao, bali pia kwa ustawishaji wa jamii .
3. Waliouridhia Mkataba huu watachukua
hatua madhubuti, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, katika kuhakikisha kuwa
sheria zinazolinda haki za ubunifu, haziweki vikwazo au kuwabagua watu wenye
ulemavu katika kupata vifaa vya kitamaduni.
4. Watu wenye ulemavu wanakuwa na haki, kwa
msingi wa usawa na watu wengine, kutambuliwa na kuunga mkono masuala yao
mahususi ya kitamaduni na utambulisho kiisimu; ikijumuisha lugha ya alama na
utamaduni wa viziwi.
5. Ili
kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kwa msingi wa usawa na watu wengine
katika mapumziko, shughuli za burudani na michezo, Waliouridhia
Mkataba huu watachukua hatua zifaazo:
(a) Kuhimiza na kuendeleza watu wenye ulemavu
katika kushiriki, kwa kadri iwezekanavyo, kwenye michezo ngazi zote;
(b) Kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu
wanakuwa na fursa ya kuandaa, kuendeleza na kushiriki kwenye riadha na burudani
ambavyo ni mahsusi kwa watu wenye ulemavu. Hali hii itafikiwa kwa kushajiisha
uwekaji masharti ya mafunzo, ufundishaji na rasilimali zinazofaa kwa msingi wa
usawa na watu wengine;
(c) Kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanaweza
kufika maeneo ambapo michezo, burudani na shughuli za kitalii vinakofanyikia,
(d) Kuhakikisha kuwa watoto wenye ulemavu
wanapata nafasi sawa na wenzao ya kushiriki katika michezo, mapumziko na
burdani, na shughuli zote za michezo ikijumuisha ile iliyo kwenye mfumo wa
kishule;
(e) Kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata
huduma kutoka kwa wale wanaoandaa shughuli za mapumziko, utalii, burudani na
michezo.
Ibara ya
31
Takwimu
na Ukusanyaji wa taarifa
1. Nchi Wanachama zinaahidi kukusanya taarifa
muhimu, ikiwa ni pamoja na takwimu na taarifa zilizofanyiwa utafiti ili
kuziwezesha kuandaa na kutekeleza sera, kwa nia ya kukidhi matakwa ya Mkataba
huu. Mchakato wa kukusanya na kuzihifadhi taarifa utahusisha:
a) Kuzingatia kinga
zilizowekwa kisheria ikijumuisha sheria ya kuhifadhi taarifa, katika
kuhakikisha usiri na kuheshimu faragha ya watu wenye ulemavu;
b) Kuzingatia kanuni
zinazokubalika kimataifa za kulinda haki za binadamu na uhuru wa msingi na
maadili yanayotumika katika ukusanyaji na utumiaji takwimu.
2. Taarifa zilizokusanywa kwa mujibu wa ibara
hii, zitachambuliwa kwa kadri inavyofaa na zitatumiwa kufanyia tathmini ya
utekelezaji wa majukumu ya nchi zilizouridhia Mkataba huu na kutambua na
kushughulikia vikwazo vinavyowakabili watu wenye ulemavu katika kutumia haki
zao.
3. Waliouridhia Mkataba huu watabeba
dhamana ya kusambaza takwimu hizi na kuhakikisha kuwa zinapatikana bila vikwazo
kwa watu wenye ulemavu na wengineo.
Ibara ya 32
Ushirikiano wa kimataifa
1. Waliouridhia
Mkataba huu wanatambua umuhimu wa ushirikiano wa
kimataifa na uendelezaji wake katika kuunga mkono juhudi za kitaifa za
kuyafikia makusudio na malengo ya Mkataba huu, na zitachukua hatua madhubuti
kwa minajili hii, baina na miongoni mwa mataifa na kwa kadri inavyofaa kwa ubia
na jumuiya za kimataifa na za kikanda na zile za kiraia, hususan, vyama/asasi
za watu wenye ulemavu. Hatua za aina hiyo zinaweza kujumuisha:
(a) Kuhakikisha
kwamba ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo mipango ya maendeleo ya kimataifa inawajumuisha
na kuwafikia watu wenye ulemavu;
(b) Kuwezesha na
kuunga mkono mipango ya kujenga uwezo, ikiwa ni pamoja na kubadilishana
taarifa, uzoefu, mipango ya mafunzo na mazoea mema yanayofaa kuigwa;
(c) Kuwezesha
ushirikiano wa kitafiti na ufikiwaji wa taarifa za kisayansi na kiteknolojia;
(d) Kutoa, kwa
kadri inavyofaa, msaada wa kiufundi na kiuchumi, ikijumuisha kuwezesha ufikiaji
na ushirikishanaji wa teknolojia saidizi iliyopo kwa njia ya na uhawilishaji wa
teknolojia.
2. Vipengele vya
ibara hii haviathiri utekelezaji wa majukumu ya Mkataba huu kwa kila nchi iliyouridhia.
Ibara ya 33
Utekelezaji na ufuatiliaji ngazi ya Kitaifa
1. Kwa mujibu wa
muundo wa kila nchi iliyoridhia Mkataba huu zitajipangia eneo moja au zaidi
ambayo ni mahususi kwa ajili ya masuala yanayohusiana na utekelezaji wa Mkataba
huu ndani ya serikali na itazingatia uanzishaji wa mfumo wa kuratibu hatua zinazohusu
utekelezaji wa kisekta katika ngazi mbalimbali serikalini .
2. Kwa mujibu wa
miundo ya kisheria na kiutawala, Waliouridhia Mkataba huu, watadumisha, wataimarisha, watadhihirisha, au kuanzisha
nchini, muundo mmoja au zaidi, ulio huru kwa kadri inavyofaa ili kuendeleza,
kulinda na kufuatilia utekelezaji wa Mkataba huu. Wakati wa kuanzisha muundo
huo, waliouridhia Mkataba huu, watazingatia kanuni zinazohusiana na hali ya utendaji
kazi wa taasisi za kitaifa katika kulinda na kukuza haki za binadamu.
3. Asasi za
kiraia, hususan zile za watu wenye ulemavu na vyama vinavyowawakilisha vitashirikishwa
na kushiriki kwa ukamilifu kwenye mchakato wa ufuatiliaji.
Ibara ya 34
Kamati kwa ajili ya Haki za Watu wenye Ulemavu
1. Itaanzishwa
Kamati ya Kimataifa kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu (halafu itajulikana kama
“Kamati”) itakayofanya kazi zitakazofafanuliwa.
2. Wakati wa
kurasmisha Mkataba huu, itakuwepo Kamati yenye wataalamu kumi na wawili. Pale nchi
sitini au zaidi zitakapouridhia au kuukubali Mkataba huu, Kamati hii
itapanuliwa kwa kuongezewa wajumbe wengine sita na hivyo, kufikia ukomo wa
wajumbe kumi na wanane.
3. Wajumbe wa
Kamati wataitumikia wakiwa na dhamana binafsi na ni wale ambao wametukuka
kiuadilifu, kiubingwa na kiuzoefu katika masuala yaliyomo kwenye Mkataba huu.
Nchi Wanachama zitateua wagombea wao kwenye kamati hii kwa kuzingatia matakwa yaliyomo
katika Ibara ya 4, aya ya 3 ya Mkatabu huu.
4. Wajumbe wa
Kamati watachaguliwa na Nchi zilizoridhia Mkataba huu kwa kutilia maanani
uwiano wa mgawanyo kijiografia, uwakilishi wa aina tofauti za ustaarabu na
mifumo mikuu ya kisheria, mizania ya kijinsia na ushiriki wa mabingwa wenye
ulemavu.
5. Wajumbe wa Kamati hii watachaguliwa kwa
kura ya siri kutokana na orodha ya wajumbe waliopendekezwa na mikutanao ya jumuiko
la Waliouridhia Mkataba huu Katika majumuiko hayo ambayo
akidi yake ni theluthi mbili ya Waliouridhia Mkataba huu, watu
watakaochaguliwa kuwa wanakamati watakuwa ni wale waliopata idadi kubwa zaidi
ya kura zilizopigwa kwa uhuru kabisa na wengi wa wawakilishi wa Waliouridhia
Mkataba huu waliohudhuria na kushiriki uchaguzi.
6. Uchaguzi wa awali utafanyika si zaidi ya
miezi sita baada ya Mkataba huu kuanza kufanya kazi rasmi. Angalau miezi minne
kabla ya tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi wowote ule, Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, ataziandikia barua Waliouridhia Mkataba huu
akikaribisha mapendekezo ya majina ambayo yatawasilishwa kwake katika kipindi
cha miezi miwili baada ya taarifa. Kisha, Katibu Mkuu ataandaa orodha ya watu
wote walioteuliwa katika mfumo wa kialfabeti, na akiainisha nchi
zilizowapendekeza na kuiwasilisha mbele ya Waliouridhia Mkataba huu.
7. Wanakamati watachaguliwa kwa vipindi vya
miaka minne minne. Wanaweza kuchaguliwa tena kwa muhula mwingine mmoja tu. Hata
hivyo, dhamana ya wanakamati sita waliochaguliwa katika uchaguzi wa mwanzo,
utakoma kufuatia uchaguzi utakaofanyika baada ya kipindi cha miaka miwili tangu
ule wa mwanzo. Mara baada ya uchaguzi wa kwanza, majina ya wanakamati hao sita
yatachaguliwa kwa njia ya kubahatisha na Mwenyekiti wa jumuiko lililozungumziwa
katika aya ya tano ya ibara hii.
8. Uchaguzi wa wanakamati sita wa ziada utafanyika
wakati wa uchaguzi wa kawaida, kwa mujibu wa vifungu husika kwenye Ibara hii.
9. Endapo mwanakamati atafariki dunia au
kujiuzulu au atatamka mwenyewe kwamba kwa sababu fulani fulani hawezi tena
kuendelea kutekeleza majukumu yake, Nchi iliyoridhia Mkataba huu ambayo
ilimpendekeza kwa mara ya kwanza, itamteua bingwa mwingine mwenye sifa na
kutosheleza vigezo vilivyobainishwa na vifungu husika vya ibara hii, ili
atumikie muda uliobakia.
10. Kamati
itatayarisha utaratibu wake wa kazi.
11. Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa atatoa wafanyakazi na vifaa vinavyotakiwa katika kutekeleza
kiufanisi kazi za kamati chini ya Mkataba huu, na mkutano wa kuizindua Kamati
atauitisha yeye.
12. Kwa idhini ya
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, wajumbe wa Kamati iliyoundwa chini ya Mkataba
huu, watapata ujira kutokana na rasilimali za Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa matakwa na masharti yanayoweza
kuamuliwa na Baraza Kuu likitilia maanani umuhimu wa majukumu ya Kamati;
13. Wajumbe wa
Kamati watakuwa na haki ya kupata vitendea kazi, marupurupu na kinga kama
ilivyo kwa mabingwa wengine kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa kama
inavyofafanuliwa kwenye vifungu husika vya Mkataba wa marupurupu na kinga za
Umoja wa Mataifa.
Ibara ya 35
Taarifa za Waliouridhia Mkataba huu
1. Kupitia kwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kila aliyeuridhia Mkataba huu atawasilisha
mbele ya Kamati, taarifa ya kina ya hatua zilizochukuliwa katika kutimiza
wajibu wake chini ya Mkataba huu na maendeleo yaliyopatikana kutokana na
utekelezaji huo ndani ya muda wa miaka miwili baada ya kuanza kutumika rasmi
katika kila aliyeuridhia.
2. Kuanzia hapo,
kila aliyeuridhia Mkataba huu, atawasilisha taarifa zake walau kila baada ya miaka
minne au zaidi kwa kadri Kamati itavyoitaka.
3. Kamati itaamua,
aina ya miongozo itakayotumika kwenye maudhui ya taarifa.
4. Kila
aliyeuridhia Mkataba huu aliyewasilisha taarifa yake ya kina mbele ya Kamati,
hatakuwa na haja ya kurudia mambo yale yaliyokwisha taarifiwa awali. Katika kutayarisha
taarifa kwa ajili ya Kamati Waliouridhia
Mkataba huu wanatakiwa kuzingatia kufanya hivyo kwa kutumia
mchakato wenye uwazi na kutilia maanani matakwa yaliyomo katika Ibara ya 4, aya
ya 3 ya Mkataba huu.
5. Ripoti
zinaweza kubainisha sababu na changamoto zinazoathiri kiwango cha utekelezaji
wa majukumu chini ya Mkataba huu.
Ibara ya 36
Kujadili taarifa
1. Kamati,
itazingatia kila taarifa na itatoa ushauri na mapendekezo ya jumla kuhusu
taarifa yenyewe kama itakavyoona inafaa na kuiwasilisha kwa mhusika. Mhusika anaweza
kujibu kwa kutoa maelezo yoyote kwa Kamati. Pia Kamati inaweza kutaka maelezo
ya ziada yanayohusiana na utekelezaji wa Mkataba huu kutoka kwa mhusika.
2. Ikiwa aliyeridhia
Mkataba huu atakawia sana kuwasilisha taarifa yake, Kamati inaweza kumuarifu
juu ya umuhimu wa kukagua hali ya utekelezaji wa Mkataba huu kwa mujibu wa
maelezo ya kuaminika yaliyoifikia Kamati. Ikiwa taarifa inayotakiwa, haitawasilishwa
ndani ya miezi mitatu baada ya kukumbushiwa, Kamati itamwalika mhusika
kushiriki katika uchunguzi huo. Ikiwa mhusika hatajibu kwa kuwasilisha taarifa
inayohitajika na matakwa ya aya ya 1 ya ibara hii yatatumika.
3. Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa atasambaza taarifa hizi kwa wote waliouridhia Mkataba huu.
4. Waliouridhia Mkataba huu, watausambazia umma taarifa zake zinazohusu nchi yao
kadhalika na ushauri na mapendekezo ya jumla kuhusiana na taarifa yenyewe.
5. Kamati itazituma,
fedha na programu za Umoja wa Mataifa kwa wakala maalum na jumuiya nyingine kwa
kadri itakavyoona inafaa, ili zikashughulikie ombi au dalili za haja ya ushauri
wa kiufundi au msaada, pamoja na ushauri wa Kamati na mapendekezo, kama yapo,
juu ya maombi hayo au dalili hizo.
Ibara ya
37
Ushirikiano baina ya Waliouridhia Mkataba huu na Kamati
1. Kila
aliyeuridhia Mkataba huu huu itashirikiana na Kamati na kuwasaidia wajumbe wake
kutekeleza wajibu wao.
2. Katika
uhusiano wake na Waliouridhia Mkataba huu, Kamati itazingatia njia na mbinu za kuendeleza uwezo wa
kila aliyeuridhia katika kutekeleza Mkataba huu, ikiwa ni pamoja na kwa njia za
ushirikiano wa kimataifa.
Ibara ya
38
Uhusiano wa Kamati na vyombo vingine
Katika kuendeleza utekelezaji mzuri wa Mkataba huu na
kushajiisha ushirikiano wa kimataifa katika maeneo yaliyoainishwa ndani ya
Mkataba huu:
a) Wakala za Umoja
wa Mataifa zitakuwa na haki ya kuwakilishwa wakati wa kupangilia utekelezaji wa
matakwa ya Mkataba yanayoangukia kwenye mamlaka zao. Kamati inaweza kuzialika
wakala maalum na vyombo vingine vya kitaalamu kadri itakavyoona inafaa ili
vitoe ushauri wa kitaalamu juu ya utekelezaji wa Mkataba huu katika maeneo yanayoangukia
kwenye mamlaka zao. Kamati inaweza kuzikaribisha wakala maalum na vyombo
vingine vya Umoja wa Mataifa kuwasilisha taarifa zao juu ya utekelezaji wa
Mkataba huu katika maeneo yanayoangukia kwenye mamlaka zao;
b) Katika
kutekeleza mamlaka iliyonayo, Kamati, kwa kadri itakavyoona inafaa,
itashauriana na vyombo vingine vinavyoanzishwa kwa mikataba ya haki za binadamu
kwa lengo la kuhakikisha uthabiti wa mfumo wa miongozo ya kutayarisha taarifa
husika, maoni na mapendekezo ya jumla na hivyo kujiepusha na marudio na
kuingiliana katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ibara ya 39
Taarifa ya Kamati
Kamati itatoa taarifa ya shughuli zake kila baada ya
miaka miwili mbele ya Baraza Kuu na kwa Halmashauri ya masuala ya kiuchumi na
kijamii na inaweza kushauri na kutoa mapendekezo ya jumla kutokana na uchunguzi
na taarifa ilizozipokea kutoka kwa waliouridhia Mkataba huu. Ushauri huo na
mapendekezo ya jumla yataingizwa katika taarifa ya Kamati pamoja na maoni, kama
yapo, kutoka kwa waliouridhia.
Ibara ya
40
Kikao cha Waliouridhia
Mkataba huu
1. Waliouridhia Mkataba huu, watakutana mara kwa mara katika vikao rasmi, ili
kushughulikia jambo lolote kuhusu utekelezaji wake.
2. Kabla ya miezi sita kupita tokea Mkataba huu
kuanza kutumika rasmi, kikao cha Waliouridhia
Mkataba huu kitaitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa. Mikutano itayofuata itaitishwa na Katibu Mkuu kila baada ya miaka
miwilimiwili au kwa kutakiwa kufanya hivyo kutokana na maamuzi ya kikao cha Waliouridhia Mkataba huu.
Ibara ya 41
Utunzaji
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atakuwa ndiye mtunzaji
mkuu wa Mkataba huu.
Ibara ya 42
Saini
Mkataba huu utawekwa wazi Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa
New York, kuanzia Machi 30, 2007 kwa ajili ya kusainiwa na Nchi zote na Jumuiya
za Kikanda.
Ibara ya 43
Hiari ya kuwajibika
Mkataba huu utatakiwa kuridhiwa na Nchi zilizotia saini
na kuthibitishwa rasmi kwa saini. Jumuiya za kikanda pia zinaweza kuuridhia
Mkataba huu. Mkataba huu utakuwa wazi kupata ridhaa ya nchi yoyote au Jumuiya
ya Kikanda ambayo haijasaini Mkataba huu.
Ibara ya 44
Jumuiya za
kikanda
1. “Jumuiya ya Kikanda”
itamaanisha taasisi iliyoundwa na Nchi huru katika eneo fulani ambapo Nchi
wanachama wamekabidhi uwezo wa kisheria wa masuala yanayolindwa na Mkataba huu.
Taasisi za aina hii zitatangaza kwenye vyombo vyake kuthibitisha au kukubali na
kufafanua ukomo wake kisheria kuhusiana na mambo yanayolindwa na Mkataba huu.
Halafu zitamuarifu Mtunzaji juu ya mabadiliko yoyote ya msingi yanayohusu uwezo
wa kisheria.
2. Pale
panapotamkwa “Waliouridhia Mkataba huu” patahusisha pia Jumuiya za aina hii kwa
kadri ya ukomo wa uwezo wake kisheria.
3. Kwa madhumuni
ya Ibara ya 45, aya ya 1 na ibara ya 47 aya ya 2 na 3 ya Mkataba huu, hati za
kuridhia au mapendekezo ya marekebisho toka kwenye Jumuiya za Kikanda
hayatazingatiwa.
4. Kulingana na
ukomo wa uwezo wa kisheria zilizonao Jumuiya za Kikanda, zinaweza kutumia haki
yake ya kupiga kura katika vikao vya Waliouridhia Mkataba huu kwa idadi sawa ya
kura na zile Nchi zinazounda Jumuiya husika. Jumuiya hizo hazitatumia haki ya
kupiga kura ikiwa mmoja wa Nchi mwanachama wake ametumia haki yake ya kupiga
kura, au vinginevyo.
Ibara ya 45
Kuanza kutumika rasmi
1. Mkataba huu
utaanza kutumika rasmi siku ya thelathini baada ya kupokelewa kwa hati ya
ishirini ya kuuridhia au kuukubali.
2. Kwa kila Nchi
au Jumuiya ya Kikanda iliyoridhia na kuuthibitisha rasmi au kuukubali Mkataba
huu baada ya kuwasilishwa kwa hati ya ishirini, Mkataba huu utaanza kutumika
siku ya thelathini baada ya kuwasilishwa kwa hati yake yenyewe.
Ibara ya 46
Shaka
1. Shaka lolote
lisiloendana na lengo au makusudio ya Mkataba huu halitaruhusiwa.
2. Shaka
linaweza kuondolewa wakati wowote.
Ibara ya 47
Marekebisho
1. Nchi yoyote
iliyoridhia Mkataba huu inaweza kupendekeza marekebisho kwenye Mkataba huu na
kuyawasilisha kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Katibu Mkuu atawasilisha
mapendekezo ya marekebisho yoyote kwa Nchi zilizouridhia Mkataba huu pamoja na
ombi la kuzitaka zimjulishe kama zinapendelea kuitishwa kwa jumuiko la Nchi zilizoridhia
kwa madhumuni ya kufikiria na kuamua juu ya mapendekezo hayo. Itakapotokea
kwamba ndani ya miezi minne tokea tarehe ya mawasiliano hayo angalau theluthi
moja ya Nchi zilizoridhia zimependelea kuitishwa kwa kikao, basi Katibu Mkuu
atakiitisha chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa. Marekebisho yoyote
yatakayopitishwa kwa wingi wa theluthi mbili ya kura za Nchi zilizohudhuria na
kupiga kura, yatawasilishwa na Katibu Mkuu mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa kwa kuidhinishwa na baadaye kwa Nchi zote zilizoridhia ili ziyakubali.
2. Marekebisho
yaliyopitishwa na kuthibitishwa kwa mujibu wa aya ya 1 ya ibara hii, yataanza
kutumika siku ya thelathini baada ya hati za kuyakubali zilizowasilishwa
kufikia theluthi mbili ya Nchi zilizoridhia siku ya kupitishwa kwa marekebisho.
Kisha, marekebisho yataanza kutumika kwa Nchi yoyote siku ya thelathini kufuatia
ilipoweka hati yake yenyewe ya kuyakubali. Ni Nchi zile tu zilizoridhia ambazo
zimeyakubali marekebisho ndizo zitakazobanwa na marekebisho hayo.
3. Ikiwa itaamuliwa
kwa pamoja na kikao cha Nchi zilizoridhia marekebisho yaliyofanywa na
kuthibitishwa kwa mujibu wa aya ya 1 ya ibara hii ambayo yanahusiana, hususan,
na ibara ya 34, 38, 39 na 40, yataanza kutumika kwa Nchi zote zilizoridhia siku
ya thelathini baada ya hati za kuyakubali kufikia theluthi mbili ya idadi ya
Nchi zilizoridhia siku ile
yalipopitishwa .
Ibara ya 48
Kujitoa
Nchi iliyoridhia Mkataba huu inaweza kujitoa katika
utekelezaji wake kwa kumpelekea Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa taarifa ya
maandishi kuhusu kujitoa kwake. Kujitoa huko kutatekelezeka mwaka mmoja baada
ya tarehe ambayo Katibu Mkuu alipokea taarifa hiyo.
Ibara ya 49
Njia rahisi ya kupatikana
Mkataba huu utaweza kupatikana katika hali zinazofikika.
Ibara ya 50
Mkataba Halisi
Nakala za Mkataba huu kwa lugha za Kiarabu, Kichina,
Kiingereza, Kifaransa, Kirusi na Kihispania zitakuwa na uhalisia ule ule.
KWA
KUSHUHUDIWA na wajumbe wenye mamlaka kamili waliosaini hapo chini kwa kuidhinishwa na na Serikali
husika wametia saini Mkataba huu.
Mkataba wa Nyongeza kwa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu
Walioridhia Mkataba wa Nyongeza wamekubaliana kama ifuatavyo:
Ibara ya 1
1. Walioridhia
Mkataba huu wa Nyongeza wanatambua uwezo wa Kamati ya Haki za Watu wenye Ulemavu
(Kamati) wa kupokea na kutafakari taarifa kwa mujibu wa mamlaka yake kutoka kwa
au kwa niaba ya watu binafsi au makundi ya watu ambao wanadai kuwa ni waathirika
wa ukiukwaji wa masharti ya Mkataba huu wa Kimataifa ulioridhiwa na mamlaka
husika.
2. Hakuna
taarifa itakayopokelewa na Kamati ikiwa inaihusu Nchi iliyoridhia Mkataba wa kimataifa
wa haki za watu wenye ulemavu lakini ambayo bado haikuiridhia Mkataba wa
Nyongeza.
Ibara ya 2
Kamati itaichukulia taarifa fulani kwamba haipaswi
kushughulikiwa ikiwa:
(a) Taarifa
haitambuliki ilikotoka.
(b) Taarifa
hiyo itakuwa inakiuka haki ya kuwasilisha taarifa za aina
hiyo au haikubaliani na vipengele vya
Mkataba;
(c) Suala
hilo tayari limeshachunguzwa na Kamati, au
linachunguzwa chini ya utaratibu mwingine wa
upelelezi au usuluhishi
wa kimataifa;
(d) Kabla ya
kuzipitia njia zote za kulipatia ufumbuzi tatizo hilo ndani ya Nchi husika.
Kipengele hiki hakitokuwa na uzito endapo utatuzi wa tatizo utaonekana kuchukua
muda mrefu bila sababu za msingi au kutoelekea kuleta faraja inayofaa;
(e) Taarifa haitakuwa
na ithibati au maelezo yenye kujitosheleza, au endapo
(f) Tatizo
ambalo ni chanzo cha taarifa litakuwa lilitokea kabla ya Mkataba huu wa
Nyongeza kuanza kutumika kwa Nchi iliyoridhia, isipokuwa kama tatizo hilo liliendelea
baada ya hapo.
Ibara ya 3
Kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 2 ya Mkatatba wa
Nyongeza, Kamati itawasilisha tuhuma iliyoipokea kwa njia ya siri kwa Nchi
iliyoiridhia na inayotuhumiwa. Ndani ya kipindi cha miezi sita, Nchi iliyoridhia
itawasilisha mbele ya Kamati maelezo, kwa maandishi au maelezo ya ana kwa ana,
ikifafanua jambo linalolalamikiwa na hatua za utatuzi wake, ambazo zimechukuliwa
na Nchi husika, kama zipo.
Ibara ya 4
1. Wakati wowote
baada ya kupokea taarifa na kabla ya kufikia uamuzi kwa hoja, Kamati inaweza kuipelekea
Nchi iliyoridhia ombi kuchukuliwa kwa hatua za muda mfupi kadri itakavyokuwa ni
lazima ili kuepuka athari isiyoweza kurekebishika inayoweza kumpata muathirika
au waathirika wa ukiukwaji tuhumiwa.
2. Pale Kamati
itakapoamua kutumia mamlaka yake chini ya aya ya kwanza ya ibara hii, haimaanishi
kuwa imetoa uamuzi wa kuikubali taarifa au juu ya ustahili wa malalamiko
yaliyowasilishwa.
Ibara ya 5
Katika kujadili malalamiko chini ya Mkataba wa Nyongeza, Kamati
itafanya mikutano ya faragha. Baada ya kuchunguza taarifa, Kamati itapeleka
ushauri na mapendekezo yake, kama yapo, kwa Nchi husika iliyoridhia na kwa
mlalamikaji.
Ibara ya 6
1. Ikiwa Kamati
itapokea taarifa ya kuaminika kwamba Nchi iliyoridhia inafanya ukiukaji mkubwa
au ina mfumo unaokiuka haki zilizotamkwa ndani ya Mkataba, Kamati itaitaka Nchi
husika kushirikiana nayo katika kuchunguza taarifa, na kwa ajili hiyo,
kuwasilisha maoni kuhusu taarifa husika.
2. Kwa
kuzingatia maoni yoyote ambayo yamewasilishwa na Nchi husika iliyoridhia pamoja
na taarifa nyingine yoyote ya kuaminika iliyopatikana, Kamati inaweza kuteua
mjumbe wake mmoja au zaidi kufanya uchunguzi na kutoa taarifa ya haraka kwa
Kamati. Endapo itaruhusiwa na kwa ridhaa ya Nchi iliyoridhia, uchunguzi unaweza
kujumuisha ziara ndani ya Nchi inayolalamikiwa.
3. Baada ya
uchambuzi, Kamati itawasilisha yaliyogunduliwa kwenye uchunguzi huo, mbele ya
Nchi husika ikiwa ni pamoja na maoni na mapendekezo yoyote kama yapo.
4. Nchi inayohusika
itatakiwa kutoa maoni na mapendekezo kwa Kamati ndani ya kipindi cha miezi sita
tokea kupokea taarifa ya uchunguzi;
5. Uchunguzi wa
aina hiyo utafanywa kwa siri na kwa kuomba ushirikiano na Nchi husika katika
hatua zote za uchunguzi.
Ibara ya 7
1. Kamati
inaweza kuitaka Nchi husika kujumuisha kwenye ripoti yake chini ya Ibara ya 35
ya Mkataba huu, maelezo ya hatua zilizochukuliwa mintarfu uchunguzi uliofanywa
chini ya Ibara ya sita ya Mkataba wa Nyongeza.
2. Baada ya
kipindi cha miezi sita kilichotajwa katika Ibara ya 6, aya ya 4 kupita ikibidi,
Kamati inaweza kuitaka Nchi husika iliyoridhia kuiarifu juu ya hatua
ilizochukua kuhusiana na uchunguzi kama huo.
Ibara ya 8
Kila Nchi iliyoridhia inaweza wakati wa kutia saini au kuridhia,
au kuukubali Mkataba wa Nyongeza, kutangaza kuwa haitambui uwezo wa Kamati hii
ulioelezwa katika Ibara ya 6 na 7.
Ibara ya 9
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atakuwa ndiye Mhifadhi wa
Itifaki hii ya Hiari.
Ibara ya 10
Mkataba wa Nyongeza utakuwa wazi kwa kutiwa saini na Nchi
zilizoridhia na jumuiya za muungano wa kikanda za Mkataba huu wa Kimataifa
katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, kuanzia tarehe 30 Machi,
2007.
Ibara ya 11
Kuanza kutumika rasmi kwa Mkataba huu wa Nyongeza
kutategemeana na kusainiwa na Nchi (zilizotia saini) ambazo zimeridhia au kuukubali
Mkataba. Itatakiwa kuthibitishwa rasmi kwa kusaniwa na Jumuiya za Muungano wa Kikanda
zilizotia saini mkataba wa Nyongeza ambazo zimethibitisha rasmi au kuukubali
Mkataba. Utakuwa wazi kukubaliwa na Nchi au Jumuiya ya Muungano wa Kikanda yoyote
ambayo imeridhia, imethibitisha rasmi au kuukubali Mkataba na ambayo haijatia
saini mkataba wa Nyongeza.
Ibara ya 12
1. “Jumuiya za Muungano
wa Kikanda” zitamaanisha jumuiya zilizoundwa na Nchi huru za eneo fulani la
kijiografia ambapo wanajumuiya (nchi zinazoiunda) zitakasimu mamlaka
yanayotawaliwa na Mkataba huu kadhalika na Mkataba wa Nyongeza. Jumuiya za aina
hii zitatamka kupitia hati rasmi za uthibitishaji au ukubalifu kiwango cha
mamlaka kuhusiana na mambo yanayoongozwa na Mkataba na Mkataba wa Nyongeza kadhalika.
Halafu zitamuarifu Mhifadhi pale yatakapotokea mabadiliko yoyote ya msingi
yanayohusu uwezo wake;
2. Kwa mujibu wa
Mkataba huu wa Nyongeza Jumuiya kama hizo zitatajwa kama “Nchi zilizoridhia” kulingana
na mipaka yake ya kiuwezo;
3. Kwa madhumuni
ya ibara ya 13, aya ya 1 na ibara ya 15 aya ya 2 ya Mkataba huu wa Nyongeza,
hati yoyote itakayowasilishwa na Jumuiya ya Muungano wa Kikanda haitohesabiwa;
4. Kwa masuala
yaliyomo ndani ya mamlaka zao, Jumuiya za Muungano wa Kikanda zinaweza kutumia haki
yao ya kupiga kura katika mikutano ya Nchi zilizoridhia kwa idadi sawa ya kura
na ile ya Nchi wanachama wao ambao zimeiridhia Mkataba huu wa Nyongeza. Hata
hivyo, Jumuiya hizo hazitotumia haki ya kupiga kura ikiwa mmoja wa Nchi
mwanachama wake ametumia haki yake ya kupiga kura, na kadhalika.
Ibara ya 13
1. Kwa kutegemeana
na ni lini Mkataba huu wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu utaanza kazi,
Mkataba wa Nyongeza utaanza kutumika siku ya thelathini baada ya kuwasilishwa
kwa hati ya kumi ya kuiridhia au kuikubali;
2. Baada ya
kuwasilishwa kwa hati ya kumi na Nchi au Jumuiya ya Muungano wa Kikanda
iliyoridhia, kuthibitisha rasmi au kuukubali Mkataba huu wa Nyongeza ndipo
itakapoanza kutumika rasmi. Nchi husika itaanza kubanwa na Itifaki hii ya Hiari
siku ya thelathini tangu ilipowasilisha hati yake kuridhia.
Ibara ya 14
1. Shaka lolote
linalopingana na lengo au makusudio ya Itifaki ya Hiari halitoruhusiwa.
2. Shaka
linaweza kuondolewa wakati wowote.
Ibara ya 15
1. Nchi yoyote
iliyoridhia inaweza kushauri marekebisho ya Mkataba wa Nyongeza na
kuyawasilisha kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Katibu Mkuu atawasilisha
marekebisho yoyote yanayopendekezwa na Nchi zilizoridhia pamoja na ombi la kuzitaka
zimjulishe iwapo zinakubali kuitishwa kwa mkutano wa Nchi zilizoridhia kwa
madhumuni ya kuzingatia na kufanya maamuzi juu ya mapendekezo yaliyowasilishwa.
Itapotokea kwamba ndani ya miezi minne tokea tarehe ya mawasiliano hayo angalau
theluthi moja ya Nchi zilizoridhia zimekubali kuitishwa mkutano, Katibu Mkuu
ataitisha mkutano chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Marekebisho yoyote
yatakayopitishwa kwa wingi wa theluthi mbili ya kura za Nchi zilizohudhuria na
kupinga kura, yatawasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Katibu
Mkuu kwa kuidhinishwa na kisha kwa Nchi zote zilizoridhia ili yakubaliwe.
2. Marekebisho
yaliyopitishwa na kuthibitishwa kwa mujibu wa aya ya 1 ya ibara hii, yataanza
kutumika siku ya thelathini baada ya hati za kuyakubali zilizowasilishwa
kufikia theluthi mbili ya Nchi zilizoridhia siku ya kupitishwa kwa marekebisho
husika. Baadae marekebisho yataanza kutumika kwa Nchi yoyote siku ya thelathini
kufuatia kuweka hati yake ya kuyakubali. Marekebisho hayo yatazibana zile Nchi
zilizoridhia ambazo zimeyakubali.
Ibara ya 16
Nchi iliyoridhia inaweza kujitoa katika utekelezaji wa
Itifaki ya Hiari kwa kumpelekea Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa taarifa ya
maandishi kuhusu kujitoa kwake. Kujitoa huko kutakuwa na nguvu mwaka mmoja
baada ya tarehe ambayo Katibu Mkuu alipokea taarifa hiyo.
Ibara ya 17
Mkataba wa Nyongeza utaweza kupatikana kwa njia ambayo
watu wataipata kwa wepesi.
Ibara ya 18
Nakala za Mkataba wa Nyongeza katika lugha za Kiarabu,
Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kirusi na Kihispania zitakuwa sawa sawa na ni
nakala rasmi.
MBELE YA
MASHAHIDI, wanadiplomasia wenye dhamana za Serikali
zetu, tumetia saini Mkataba huu wa Nyongeza.
Comments
Post a Comment