WALEZI WATAKIWA KUTOWAKATISHA TAMAA WATOTO WENYE ULEMAVU



 
Na Raya Hamad,
Wazazi na walezi wenye watoto walemavu hasa viziwi wametakiwa  kutowakatisha tamaa watoto wao kwa kuwaacha majumbani na badala yake kuwapeleka katika vituo maalum vinavyotowa elimu ili waweze kujifunza pamoja na kujielewa .
Wito huo umetolewa na Waziri wanchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza Wa Rais Mhe Fatma Abdul habib Ferej pamoja na Waziri wa Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Wanawake na Watoto Mhe Zainab…..wakati walipotembelea kituo cha Maendeleo ya vijana na watoto Viziwi Upendo viziwi  kilichopo Mwanakwerekwe na kuona maendeleo ya watoto hao pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo.
Mhe Fatma amesema ni jukumu la  wazazi  kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata mahitaji yao ya msingi hasa katika suala la malezi kama walivyo watoto wengine jambo ambalo litamfanya mtoto akuwe vizuri.” Mtoto yeyote akilelewa na kutunzwa vyema basi hata ukuwaji wake unakuwa mzuri majirani na watu wengine watampenda kwa vile wazazi wameonesha upendo “ alisisitiza Waziri Fatma .

Waziri Fatma alisema  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inafanya kila jitihada kuona watoto wenye ulemavu wanapata haki na fursa sawa na kupanga mikakati mizuri ya uendeshaji na usimamizi wa masuala ya Watu Wenye Walemavu kupitia Idara ya Watu Wenye Ulemavu
Aidha Mhe Fatma amewaomba wale wote walioahidi kuchangia  mfuko wa watu wenye ulemavu siku ya uzinduzi na ambao hawajatimiza ahadi hio wajitahidi kutimiza ahadi hio kama walivyahidi mbele ya Ras wa Zanzibar ili walengwa waweze kufaidika na mfuko huo kwa vile ni watu maalum wenye mahitaji maalum .
 Mhe Zainab ametowa wito kwa wazazi na walezi kutokwepa majukumu yao ya ulezi na kusubuiri kila kitu kutoka Serikalini ama misaada kutoka kwa wahisani bali wajitahidi kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia na hali za maisha “Mimi naamini kuna mambo mengine yamo ndani ya uwezo wetu basi tujitahidini ili tusibebe dhima kwa Mwenyezi Mungu”
 Nae Katibu wa Kituo cha Upendo bibi Mwanajuma Zahoro ameuleza ujumbe huo matatizo waliyonayo kuwa ni pamoja na Jengo la kudumu,usafiri, uwezo wa kutafuta nyenzo ,uhaba wa vitendea kazi , awali walikuwa wakilipa fedha ndogo lakini bahati mbaya aliyewakodisha nyumba amefariki na hivyo kodi imepanda warithi wanataka kulipwa shilingi Milioni moja na laki moja na arobaini elfu kwa mwaka .
Aidha Mwenyekiti wa Upendo Bi Saada Hamad ameushukuru ujumbe huo na kuwaomba viongozi hao kuwapatia walimu watakaofundisha watoto wao stadi za maisha  zikiwemo Athari za matumizi ya Dawa za Kulevya , Mimba za utotoni, kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, Mazingira na Haki za Watu Wenye Ulemavu .
 Waziri Fatma alikabidhi fedha taslim shilingi laki tatu ambapo Mhe Zainab alikabidhi shilingi laki moja kwa niaba ya Mama Park Raia wa Korea ambae pia alitowa zawadi mbali mbali zilizochangwa na watoto wa Jamhuri ya Watu wa Korea .
Mama Park amehidi kuendelea kusaidia tena  hali inaporuhusu kwani misaada anayoitowa ni   michango wa watoto wa Jamhuri ya Watu wa Korea maalum kwa watoto wenzao hasa wenye mazingira magumu na mahitaji maalum ikiwemo chakula , vifaa vya kuandikia, mikoba, viatu , toys nk. 
Upendo Viziwi hivi sasa inawanafunzi zaidi ya 40 imeanzishwa 2005 wakiwa na watoto watatu wanawake na wanafundisha lugha ya alama kwa vijana na watoto viziwi walio chini ya umri wa miaka 20  pia wanasomesha masomo ya dini , kutengeneza madometi, kufuma, kudarizi pamoja na kufinyanga .
Lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuwafundisha watoto viziwi  lugha ya alama ili wanapoanza elimu ya msingi wawe tayari wanaelewa lugha hio na kuweza  kuwasiliana vizuri wakiwa darasani. 

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU