TATIZO LA WATOTO WALEMAVU KUKOSA ELIMU.

Mtoto mwenye ulemavu wa viungo.
“NAPENDA kuwa rubani… lakini baba hajanipeleka shule mpaka leo, ananiambia nitaenda lakini bado nipo nyumbani nashinda nacheza tu.”
Hayo ni maneno ya Farid Shabani (7) Mkazi wa Kongowe, Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, anayasema wakati akizungumza na mwandishi wa makala hii.
Farid ni mlemavu mwenye uono hafifu akitumia jicho moja huku jicho la pili likiwa halioni kabisa. Baba yake ameshindwa kumuanzishia shule kutokana na shule zilizopo karibu na nyumbani kwao kutokuwa na walimu maalumu.
Hivi karibuni iliwekwa bayana kuwa asilimia 86 ya watoto walemavu katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha wameshindwa kupata huduma ya elimu kutokana na kukosekana kwa miundombinu rafiki kwenye baadhi ya shule wilayani humo.
Mtoto huyo mwenye hisia kali za kuwa na maendeleo baadaye anasikitika kwa vile haoni namna ya yeye kuweza kusoma badala ya kuendelea kukaa nyumbani.
Farid anaona kitendo cha kuendelea kukaa nyumbani bila kuanza masomo ni sawa na kunyanyapaliwa. Farid anaishi na wazazi wake wawili, Shaban Salum na Fatuma Omari wote wenye ulemavu wa kusikia.
Mtoto huyo hutumia muda mwingi kuwaangalia usoni wazazi wake kwa mawasiliano ya kila siku, pamoja na pale anapowasisitiza jambo hususan la kupelekwa shule.
Baba yake alipata ulemavu akiwa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Azania iliyopo jijini Dar es Salaam. Ulemavu huo ulisababisha ashindwe kuendelea na masomo.
Shabani anaeleza kuwa mtoto wake huyo alizaliwa akiwa haoni kabisa. Anaongeza kuwa alimpeleka katika Hospitali ya CCBRT ambapo alifanyiwa upasuaji ambao ulimsaidia sana.
Baada ya upasuaji huo jicho moja lilianza kuona na jingine likiwa limepangwa kufanyiwa matibabu baada ya hilo moja kupona.
Shabani anasema baada ya jicho moja kuanza kuona japo kwa uono hafifu alipangiwa kuhudhuria kliniki katika hospitali hiyo mara nne kwa mwaka, jambo lililokuwa gumu kutokana na kukosa fedha za nauli.
Mzazi huyo anaendelea kueleza kuwa alishauriwa na wataalamu wa CCBRT kumpeleka mtoto huyo ili aweze kusafishwa jicho mara nne kwa mwaka. Wataalamu walisema kuwa virusi kutoka katika jicho bovu vinashambulia jicho linaloona.
“Nampenda sana mwanangu lakini nashindwa nitamsaidiaje, sina kazi ya kueleweka ya kuniwezesha kupata fedha niweze kumpeleka akasafishwe jicho lake.
“Hata kumpeleka shule nimeambiwa mpaka nikamuone mtaalamu atanielekeza kutokana na tatizo lake shule gani nimpeleke lakini fedha sina na hakuna msaada ninaopata,” anasema.
Aidha, mtoto huyo amekuwa akimsumbua kuhusu kuanzishwa shule lakini anashindwa pa kumpeleka akasome shule. Aliongeza kuwa shule zilizopo karibu hazina walimu maalumu wenye taaluma hiyo.
Shule anayotakiwa kumpeleka mtoto huyo iko mkoani Tanga, ambayo baba huyo hana uwezo wa kumpeleka. Hivyo, anaendelea kutafuta wafadhili wa kumlipia ada mtoto huyo.
“Najisikia vibaya kwani mara kwa mara mwanangu hupenda kuniambia anataka awe dereva wa ndege na mie ndiyo kwanza naendelea kukaa naye nyumbani bila kumpeleka shule kwa vile uwezo wangu ni mdogo,” anasema.
Wazazi wengi wenye watoto walemavu wamekuwa wakishindwa kuwapatia elimu sawa na watoto wengine. Suala hilo linatokana na sababu mbalimbali zikiwamo za ukosefu wa shule zenye mazingira rafiki kwa walemavu.
Elizabeth Kinwiko, mkazi wa Tanita wilayani Kibaha ni mmoja wa wazazi wenye watoto walemavu. Elizabeth anasema kuwa mtoto wake ameshindwa kupata haki yake ya elimu kutokana na mazingira ya shule zilizopo.
Elizabeth ambaye ana mtoto mlemavu wa macho anasema kuwa alimpeleka mtoto huyo kuanza masomo katika Shule ya Msingi Uhuru Mchangayiko jijini Dar es Salam. Kwa mujibu wa mama huyo, mtoto wake alishindwa kuendelea na masomo kutokana na madai kuwa alikuwa hachangamki akiwa shuleni.
Walimu wa shule hiyo waliwasihi wazazi kumtafutia shule nyingine kwani alikuwa hana raha ya kucheza na wenzake pindi awapo shuleni. Jambo ambalo lilisababisha wazazi kumuachisha shule mtoto wao Maryupendo.
Joyce Mndolwa, mkazi wa Tanita, mwanae, Happy Matagi, ni mmoja wa wazazi wachache sana ambao watoto wao walemavu wamepata elimu.
Anawasihi wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwapatia watoto hao haki sawa na wengine, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka shuleni ili kupata elimu.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu (SHIVYAWATA), Wilaya ya Kibaha Mjini, Daud Kulangwa, anasema tatizo la watoto wenye ulemavu wasiosoma ni kubwa.
Anasema wazazi wanaoshindwa kuwapeleka shule walemavu ni wengi na chama chao hakina uwezo wa kusaidia.
Kulangwa anasema katika halmashauri kuna kitengo cha Elimu Maalumu kinachosimamia elimu ya walemavu. Anashauri wazazi kuwapeleka watoto wao shule jirani kwani walimu wao watakuwa wanatembelea kila shule na kuwafundisha watoto hao.
Katibu wa Shivyawata Kibaha, Happy Matagi, anasema wameshafanya mawasiliano mazuri na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Jenifa Omolo.
Anasema yupo mwalimu mwenye ulemavu wa kuona atakayekuwa na ratiba ya kutembelea katika shule zenye watoto wenye ulemavu huo.
Mipango imewekwa wazi kuwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu wasiwafungie ndani na badala yake wawapeleke shule. Watoto wote watapangwa kutokana na ulemavu walio nao ili waweze kufikiwa na walimu kwenye shule husika ili kupata huduma ya elimu sawa na wengine.
Presia Mwinami ni mdau wa maendeleo hasa kwa watu wenye ulemavu ambaye pia ni mlemavu wa miguu. Mlemavu huyo ambaye ni mkazi wa mailimoja amewasihi wazazi kuwapeleka watoto wenye ulemavu kwenye shule ambazo zina walimu maalumu ili nao wapate elimu.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Shivyawata, Kulangwa, aliweka bayana kuwa asilimia 86 ya watoto walemavu katika Halmashauri ya mji huo wameshindwa kupata huduma ya elimu kutokana na kukosekana kwa miundombinu rafiki kwenye baadhi ya shule wilayani humo.
Kutokana na hali hiyo, mpango mpya wa kitaifa wa elimu jumuishi ambayo inalenga kuwezesha mabadiliko katika mfumo wa elimu unatarajia kuanzishwa hivi karibuni.
Mpango huo utazifikia shule za msingi 265 katika halmashauri za Wilaya ya Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini, Mkuranga na Kisarawe, mkoani Pwani. Lengo ni kuziwezesha shule zote ziweze kusajili watoto wenye ulemavu.
Meneja Mpango huo, Mathew Kawogo, amebainisha kuwa kupitia shule hizo wanatarajia kuwafikia watoto 3,673 wenye ulemavu wa aina mbalimbali kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Meneja Mpango huyo pia ni mwakilishi kutoka Shirika la Watu wenye Ulemavu lenye makao yake makuu nchini Uingereza, Action for Disability Development (ADD).
Mpango huo utatekelezwa kwenye halmashauri hizo nne mkoani Pwani chini ya wadau watatu. Wadau hao ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shirikisho la Watu wenye Ulemavu nchini SHIVYAWATA na Shirika hilo la ADD.
Lengo kuu ni kutekelezwa kwenye wilaya zote nchini ili ifikapo mwaka 2017 idadi kubwa ya watoto wenye ulemavu wawe wamefikiwa na fursa hiyo ya kupata elimu.
Kawogo amefafanua kuwa kupitia mpango huo Wizara ya Elimu nchini imelenga kufikia walau asilimia 80 ya watoto wote wenye ulemavu wenye umri wa kwenda shule kati ya mwaka 2013 hadi 2017.
Msimamizi wa Mpango huo, Shirika la ADD, Vicky Msamba, amewashauri wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalumu kuachana na dhana potofu ya kuwaficha watoto na badala yake wawaandikishe kwenye shule za jirani na makazi yao.
Vicky anasema mpango wa kuelimisha watoto katika madarasa jumuishi ni mpana na gharama ni kubwa.
Anaongeza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha halmashauri zote zinahamasishwa ili majengo ambayo si rafiki kwa walemavu katika shule za msingi sasa yaanze kuboreshwa.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa muongozo na wahandisi wote wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuyajenga ili yawe rafiki kwa watoto walemavu. Pia ramani zimeshasambazwa kwenye kila halmashauri ziweze kutumiwa na wahandisi.
Vicky anasema kuwa Shirika La ADD limepata fedha za mradi huo kutoka Comic Relief la Uingereza na baada ya mradi huo wizara itaendeleza yale yaliyoanzishwa na shirika hilo.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU