MIUNDOMBINU SHULENI KIKWAZO KWA WATOTO WALEMAVU

MPANGO wa Umoja wa Mataifa (UN) unaozitaka nchi wanachama kuhakikisha elimu inatolewa kwa kila mtoto bila kujali tofauti za jinsia na kimaumbile unaonekana kupata vikwazo kadha wa kadha baada ya shule nyingi hapa nchini kutokuwa na miundombinu ya kuwawezesha watoto wenye ulemavu kupata elimu bila tatizo lolote.
Mkakati huo unaosimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), unalenga kuimarisha mpango wa elimu kwa wote katika ngazi ya kitaifa na kimataifa kwa watoto wote, vijana na watu wazima ifikapo mwaka 2015.
Hapa nchini, mpango huo unaonekana kupewa kisogo na wenye mamlaka kutokana na kundi la watu wenye ulemavu wa maumbile au viungo vya mwili kutotendewa haki kutokana na shule nyingi za msingi na sekondari kutokuwa na miundombinu rafiki kwa wanafunzi hao.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni katika Wilaya ya Musoma mkoani Mara, umeonesha kuwa shule nyingi ama hazina miundombinu wala mipango ya muda mfupi na mrefu wa kuwasaidia walemavu hao kupata haki zao stahili.
Kukosekana kwa miundombinu hiyo, kunakiuka moja kwa moja haki za walemavu kama zilivyoanishwa katika mkataba wa kimataifa juu watu wenye ulemavu wa mwaka 2006, sanjari na tamko la Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu (UNDHR) la mwaka 1948 ibara ya 26.
Utafiti huo umeonesha kwamba kukosekana kwa miundo mbinu kumewafanya baadhi ya wazazi wenye watoto wa aina hiyo kufanya maamuzi magumu ya kutowapeleka shule watoto wao wenye ulemavu kwa kile wanachodhani ni sawa na kuwaadhibu.
“Sidhani kwamba ni haki kumpeleka mtoto kama huyu wa kwangu shuleni wakati najua wazi kuwa hakihitaji hata tu kujisaidia haja ndogo na kubwa hatoweza kupata msaada wa haraka. Naona ni sawa na kumtesa mwanangu, ni heri nibaki naye hapa nyumbani nihangaike naye mwenyewe,” alisikika akisema mama mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Kauli ya mama huyo inaungwa mkono na Wekesa Nyamarwa mkazi wa Kijiji cha Nyakanga ambaye anasema hata yeye ana mtoto mwenye ulemavu aliyefikia umri wa kwenda shule, lakini kutokana na hali halisi ya mazingira ya shule za hapa nchini haoni sababu na umuhimu wa kufanya hivyo.
Mnyamarwa anakiri kuwa kijana wake anapenda kusoma na ana moyo wa kukabiliana na mazingira magumu ya shule. Hata hivyo, anadai kwamba moyo huo wa mwanae ni wa muda tu kwani ana uhakika kuwa baada ya muda atachoka na kukata tama na hivyo kuacha shule.
“Mfano ni shule yetu ya msingi Nyakanga iliyopo hapa kijijini, nadhani mmeiona hata nyie haina miundombinu rafiki ya kuwawezesha watoto na wanafunzi walemavu kufurahia maisha ya shule kama walivyo wanafunzi wengine wasio walemavu.
“Shule haina ngazi za kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu kuingia darasani na zaidi hata namna ya kuingia chooni. Sasa hebu niambie unategemea nini kwa mtoto kama wangu anawezaje kuyafurahia mazingira hayo ndiyo maana nikaona ni sawa na kumpa adhabu,” alisema.
Anadai kwamba, wapo wanafunzi walemavu wengi walioko katika jamii hususani maeneo ya vijijini ambao wameshindwa kwenda shule kutokana na mazingira mabovu yanayotokana na shule karibu zote kujengwa bila kuzingatia haki za walemavu.
Wekesa anasema hali halisi iliyopo sasa inapingana na haki ya upatikanaji elimu kwa watoto wenye ulemavu inayoainisha wazi kwamba kuwa mtoto mlemavu haimaanishi kukosa haki ya kupata elimu huku akisisitiza hata mtoto mlemavu anaweza kufaulu vizuri kielimu ili mradi aandaliwe vizuri.
Anasema, serikali inatakiwa kutoa ushawishi na msaada wa kiufundi kwa kuandaa, kutoa fedha na kutekeleza kwa vitendo mipango ya kitaifa ya elimu na kuhakikisha inaisimamia ili kutoa kujenga miundo mbinu itakayokuwa rafiki kwa walemavu, hivyo kupunguza pengo lililopo.
Rajabu Josephat (16) mwanafunzi wa shule ya msingi ya Nyankanga ambaye ni mlemavu anasema ameamua kuendelea na masomo licha ya kukabiliana na mazingira magumu ya kupata elimu yake.
Rajabu anasema miundo mbinu iliyopo katika shule nyingi hapa nchini ni changamoto kubwa inayowakabili wanafunzi walemavu na kusababisha wengi wao kuamua kutokwenda shule kabisa.
Anakiri kuwa hata yeye alichelewa kujiunga na elimu ya msingi kutokana na ama hali ya umasikini wa familia anayotoka au kuhofia miundo mbinu iliyopo shuleni hapo.
“Moja ya changamoto ninayokabiliana nayo ni namna ya kwenda maliwatoni ninapokuwa shuleni na huwa inafikia mahali nashindwa kwenda na kulazimika kujibana mpaka nirudi nyumbani kwa kuwa inanilazimu niingie taratibu kwa kuhofia usalama wangu sanjari na kuambukizwa magonjwa ya mlipuko.
“Mara chache ninapobanwa na haja ndogo ama kubwa na nikashindwa kuvumilia zaidi, inanilazimu kukimbia vichakani kwenda kujisaidia, jambo ambalo ni hatari kubwa kwa vile naweza kung’atwa na nyoka au wanyama wengine hatari ambao ni adui wa biadamu na nikapoteza maisha, “ anasema.
Alphaxard Ngelegele ni Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyankanga ambaye anakiri wazi kwamba shule yake haina mazingira mazuri ya kuwawezesha watoto wenye ulemavu kupata elimu na hakuna mipango yoyote ya kukabiliana na hali hiyo.
Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kemoramba, Mayala Moses anasema licha ya ukweli kuwa shule hiyo imejengwa mwaka 2005 tu, bado haina miundombinu yoyote kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu.
Tatizo kama hili haliko katika shule za Nyankanga na Kemoramba tu zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Musoma Vijijini bali hata katika Shule ya Msingi ya Mmahare iliyopo Kata ya Etaro wilayani humo ambapo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mariam Nsoro, anasema ingawa shule haina mtoto mwenye ulemavu lakini hakuna miundo mbinu yoyote kwa ajili ya kundi hilo.
Katiba ya nchi ya mwaka 1977 ibara ya 12 kifungu kidogo cha 4 na 5, Sera ya Maendeleo ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2005, Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 1995, Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi awamu ya pili ya mwaka 2007-2011 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari wa mwaka 2005-2010 vyote vinahimiza umuhimu wa elimu kwa watu wenye ulemavu.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU