YATIMA ALIYETHUBUTU



David Mangare: Yatima aliyethubutu

Na Dismas Lyassa, Mwananchi   

SHARE THIS STORY
Tajiri maarufu Duniani, Bill Gates wakati fulani amewahi kunukuliwa akisema kinachowasumbua watu wengi kutofanikiwa ni wao wenyewe kutopenda kuthubutu.
Siku moja akiwa kwenye chuo kimoja akitoa nasaha zake, Bill Gates alisema “Mwanafunzi niliyesoma nae ambaye alikuwa akinishinda kwenye mitihani mingi, sasa hivi nimemuajiri, ni fundi wangu, alinishinda elimu darasani, mimi leo namshinda utajiri, amekuwa kati ya maelfu ya wafanyakazi ninaowalipa mshahara”.
Anachosema Bill Gates ni ukweli kuwa kusoma au kutosoma, ama kuzaliwa familia tajiri au maskini, sio tiketi kwamba unaweza kuwa tajiri au la.
Siri ya ushindi
Kinachoweza kumsaidia mtu kuwa na maisha yenye mafanikio ni uwezo wake katika kuthubutu kufanya mambo, hasa pale anapoyafanya kwa ustadi huleta tija zaidi.
Mtafiti wa masuala ya saikolojia, Norman Vincent Peale wa Marekani anasema katika kitabu chake cha Maisha yenye Mafanikio kuwa kujiamini ni silaha nyingine muhimu kama kweli unataka kuwa mwenye mafanikio.
Fahamu kuwa, akili uliyonayo ni nyenzo muhimu ya kukufanya ufanikiwe, kwa kufikiri na kutumia vipaji ulivyo navyo kisha kuvifanyia kazi. Kwa kuwa mafanikio yako yanatokana na akili yako uliyonayo. Endapo utatumia akili, hisia na imani yako kwa busara na kufanyia kazi, ni lazima maisha yako yatakuwa na mabadiliko makubwa ya mafanikio.
Una uhuru wa kuchagua namna unavyofikiri, unavyohisi na unavyoamini ili uweze kusonga mbele, kamwe usikubali kuwa na fikra mgando ambazo hazitakusogeza hapo ulipo.
“Safisha akili yako kwa mawazo mazuri. Siri ya kushinda katika maisha ni kusafisha akili kwa kuondoa tabia zinazokufanya uharibikiwe, kama vile imani potofu, mawazo hasi na badala yake uwe na tabia zenye kukufanya usonge mbele, kuwa na imani na mawazo ya kujenga na si kukubomoa.
Mfano wa yatima David
Kuna mifano mingi ya watu waliothubutu,kati yao ni kijana David Mangare, yatima anayemiliki shule ya muziki aliyoipa jina la Heavenly Vocal & Music School.
“Mimi ni mtoto wa mwisho kati ya watano, ndiye pekee wa kiume. Wengine wote wameolewa. Wazazi walikufa kwa wakati tofauti; Baba mwaka 1999, mama 2000,” anasema David, ambaye anasema wakati huyo alikuwa ana umri wa miaka 11.
Baadae aliishi kwa ndugu ambako alisoma hadi kufikia kidato cha sita, Mbezi High School, matokeo hayakuwa mazuri kutoka na kile alichosema kutoridhishwa na mazingira aliyokuwa akiishi.
“Nililazimika kujitegemea, kwa bahati nzuri wazazi waliiacha nyumba mbili, nikawa na wazo la kufanya kitu, mojawapo ni kuanzisha shule ya muziki kwa vile kanisani nilikuwa nikijifunza muziki na ninajua vema kutumia vyombo mbalimbali,” anasema David aliyezaliwa Aprili 9, 1989.
Kati ya mwaka 2010 na 2011 alijiunga alisomea cheti cha uhasibu katika chuo kikuu cha Stefano (SMMUCO), Moshi na kufanya vizuri, lakini anasema changamoto kubwa inayomsumbua ni ugumu wa kupata ajira.
“Nikaona niimalishe nguvu katika kuendeleza shule yangu hii ya muziki niliyoianzisha mwaka 2010 akiipa jina la Heavenly Vocal & Music School. Fedha za kuanzisha shule hii nilizipata baada ya wakati fulani kufanya kazi ya sensa,” anasema na kuongeza kuwa alilazimika kusomea kwa njia ya posta masomo ya muziki katika chuo kiitwacho Berklee College of Music ambacho hutoa mafunzo bure kwa njia ya posta.
Licha ya kuanzisha shule, anasema mafanikio yamekuw si ya kuridhisha kwa vile hana vitendea kazi vyote muhimu kwa ajili ya mafunzo ikiwemo kufanyia ukarabati jengo analotumia kama shule.
“Ombi langu kwa Watanzania wenye huruma ni kwamba naomba wanisaidie, napatikana kwa 0782985625, nimethubutu kuanzisha mradi huu wenye lengo la kuwafunza watu masuala yote yanayohusiana na muziki kama vile kutumia gitaa,ngoma nk, changamoto kubwa ni fedha za kuifanya shule hii kuwa ya kisasa,” anasema na kuongeza kuwa kwa sasa anaendelea kupokea wanafunzi kwa ajili ya kuwafunza muziki, ambao huwatoza kiasi kidogo kutokana na wengi wa watu anaoshughulika nao wengi wana kipato kidogo.


Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU