WATOTO WA MITAANI BOMU TULILOLIKALIA.

                                         

Watoto wa mitaani bomu tulilolikalia

 Gazeti hili toleo la jana lilichapisha makala maalumu iliyochunguza tatizo la watoto wa mitaani jijini Dar es Salaam. Makala hiyo ilielezea visa vya kusikitisha na kutisha kuhusu namna watoto wanaoishi mitaani wanavyoteseka na maisha, ikiwamo kubakwa nyakati za usiku.

Ni simulizi za kusikitisha zinazotolewa na watoto hao ambazo zinaibua mambo lukuki. Moja ya mambo hayo ni mamlaka zinazohusika na masuala ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu mijini na vijijini kutoonyesha kuguswa na matatizo yanayowasibu watoto hao. Kauli na ahadi za Serikali kuwaondoa watoto hao katika mateso zimekuwa za kinadharia tu badala ya vitendo. Mara nyingi zimekuwa zikitolewa kufikia malengo fulani ya kisiasa.

Ni tatizo ambalo linaelekea kuizidi kimo Serikali. Pamoja na kutunga sheria mbalimbali na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu watoto na ustawi wao katika jamii, Serikali imeonyesha kutokuwa na dira wala dhamira ya kweli ya kuwalinda watoto hao. Ndiyo maana sasa limekuwa jambo la kawaida kuona watoto hao wamesambaa mitaani wakiomba msaada, huku Serikali ikibakia kuwa mtazamaji tu.

Tunasema tatizo hilo ni kubwa na linaelekea kuielemea Serikali kwa sababu ya idadi ya watoto hao, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni inakua kwa kasi ya ajabu nchi nzima. Serikali imekiri kuhusu ukubwa wa tatizo, ambapo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, Ummi Mwalimu amesema katika mahojiano na gazeti hili kwamba Serikali iko mbioni kuandaa mkakati maalumu ili kupambana na tatizo la watoto wa mitaani.

Hayo ni maneno matamu na ya kutia moyo. Hata hivyo, wakosoaji wa Serikali kuhusu jinsi inavyoshughulikia tatizo hilo wanasema kauli kama hizo zimekuwa zikitolewa bila kufuatiwa na vitendo, kwani tatizo la watoto wa mitaani limekuwapo kwa muda mrefu na limeendelea kukua kwa kasi ya ajabu. Wanasema jambo linalokwaza katika juhudi za kupambana na tatizo hilo ni ukosefu wa utashi wa kisiasa.

Jiji la Dar es Salaam pekee lina watoto wa mitaani zaidi ya 6,000 wakati idadi yao ilikuwa 3,000 miaka michache tu iliyopita. Mamlaka za masuala ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu, zikiwamo taasisi zisizo za kiserikali zinasema takwimu za nchi nzima, hasa katika miji mikubwa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na mingine zinabadilika mara kwa mara kutokana na kukua kwa tatizo hilo kila kukicha.

Watoto wa mitaani waliohojiwa jijini Dar es Salaam wamesema kwa uchungu kwamba wanateseka mno, hasa nyakati za usiku kwa kubakwa na kulawitiwa na hata kupigwa pale wanapojaribu kukataa matakwa ya watesaji wao.

Hata hivyo, kinachoonekana hapa ni kwamba mateso hayo taratibu yanawajengea watoto hao usugu wa aina fulani na wataalamu wa masuala ya kijamii wanasema usugu huo unawatayarisha kuingia katika maisha ya uhalifu katika siku za usoni. Imeelezwa kwamba katika baadhi ya vitongoji vya Jiji la Dar es Salaam vikundi vya watoto wa mitaani vinavyojiita ‘Mbwakoko’ tayari vinafanya vitendo vya kihalifu.

Jamii imewanyima watoto hao upendo na matokeo yake wamekata tamaa na kulazimika kuishi kwa uhalifu. Lazima tutambue kwamba watoto hao ni bomu tulilolikalia kwa muda mrefu na sasa limefika wakati wake wa kutulipukia.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU