JAMII TUSAIDIANE NA SERIKALI KUYAPINGA HAYA.
Watoto wa mitaani Dar wanavyobakwa usiku
Kadiri siku zinavyokwenda mbele, idadi ya watoto wa mitaani inaongezeka
katika Jiji la Dar es Salaam na miji mingine mikubwa kama Arusha, Dodoma,
Mwanza, Mbeya na kwingineko.Ni suala la kawaida kuona watoto wamejipanga kando ya barabara wakiomba wasamaria wema.
Wapo ambao wako peke yao wakifanya kazi hizo, wengine wanafanya kazi hiyo wakiwa na wazazi wao; wazazi hukaa kando kusubiri kuwanyang’anya kile ambacho watoto wanaomba kutoka kwa wasamaria wema.
“Nimetoka Dodoma, huu ni mwaka wa tatu, niko na mama na bibi, wao mara nyingi huwa wanakaa pembeni ya barabara, sisi watoto ambao ni wanne ndio tunaoingia katikati ya barabara kuomba hasa wakati magari yanaposimama,”anasema, John Francis (sio jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 12 akiwa maeneo ya Faya, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Watoto wengi wa mitaani wanaonekana kuteswa mno hasa usiku kwa kubakwa na kulawitiwa na hata kupigwa pale wanapokataa kile ambacho walio wakubwa kwao wanataka ikiwemo kufanyishwa vitendo vya ngono au kutoa fedha walizoomba au walizopata kutokana na kazi mbalimbali zikiwemo kuosha magari.
Huenda ndiyo ‘majambazi’ wa kesho
Hata hivyo kinachoonekana ni kwamba baadhi ya watoto hawa huenda wakawa ni majambazi,kwani kwa mujibu wa Mwanasaikolojia, Modesta Kimonga kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, kitaalamu mtu ambaye anaishi katika hali fulani ngumu ikiwamo kiuchumi, ni rahisi kwake kushawishiwa kufanya lolote.
Wasio na jamaa wako hatarini zaidi
“Kuna kijana aliwahi kutaka kunilawiti, nilikataa, nilimwambia mama alimtukana na kutaka kumpiga.Wanaobakwa na kulawitiwa sana ni wale ambao hawana watu wa kuwasaidia, unakuta wengine wametoka mikoani, wapo hapa Dar es Salaam, hawana ndugu wala jamaa,” anasema Francis.
Usiku ni jehanamu
Katika utafiti ambao mwandishi amefanya katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, yakiwamo Ubungo katika makutano ya barabara ya Mandela, Morogoro na Sam Nujoma, Kariakoo, Posta, Kinondoni, Magomeni, Buguruni, Kawe na Mwenge ambako kunaonekana kuwa na watoto wengi wa mitaani hasa kutokana na kuwa na shughuli nyingi za mbalimbali za kijamii, usiku ni wakati wa hatari zaidi kwa watoto, kwani ndipo huwa wanafanyiwa kila aina ya ukatili, huku wakiwa hawana wa kuwasaidia.
Katika eneo la Magomeni, makutano ya barabara itokayo Kinondoni kwenda Jangwani, jijini Dar es Salaam, kuna watoto ambao wanaosha magari, utafiti unaonyesha baadhi yao wamekuwa wakiingiliwa usiku na baadhi ya watoto wa mitaani walio wakubwa au watu wengine ambao sio ombaomba kwa ahadi za kuwasaidia waondokane na maisha duni yanayowasumbua.
“Ni kweli nimewahi kuingiliwa, siyo kwamba nilipenda, nakumbuka siku hiyo mvua ilinyesha sikuwa na pa kulala, kwani mimi na watoto wenzangu huwa tunalala nje. Kuna jamaa mmoja mtu mzima ambaye naye huwa tunasafisha naye magari na shughuli zingine za mitaani, ana chumba aliniingilia kwa nguvu, alianza polepole, hatimaye alifanikiwa kuniingilia, nililia sana, sikuwa na la kufanya. Baada ya hapo akawa karibu nami kunisaidia mambo mengi yakiwemo kuninunulia chakula ninapokuwa sina fedha,” anasema mtoto mmoja katika eneo la makutano hayo (jina limehifadhiwa).
Katika eneo hilo la makutano ya barabara ya kutoka Kinondoni kwenda Jangwani, kuna mtoto mwingine ambaye muda mwingi huwa anasinzia kumaanisha kwamba huwa amekuwa amelewa, ana umri wa miaka 14, anasisitiza “Ni kweli kuna watoto wengi wanaingiliwa kinyume na maumbile hasa kama mtoto mwenyewe anapenda kula vizuri,” anasema mtoto huyo, aliyeingia jijini akitokea Mwanza kwa kumhonga fedha kidogo kondakta wa basi moja linalotoka Mwanza kuja Dar es Salaam ili kuja kujaribu maisha jijini, kwani kule Mwanza anasema japo wazazi wake wako hai, hawana uwezo.
Katika eneo la Kawe, kwenye bonde ambalo ni mpaka wa Kawe na Mbezi, kuna kundi la watoto linaloitwa Mbwakoko, kwa maana kuwa kwa haraka unaweza kufikiri ni watoto wazembe hivi, lakini ukikaribiana nao usiku utakiona cha moto.
Wana umaarufu katika eneo hilo, kwa matendo yao, kuna wakati wenyeji wanasema huwalazimisha wanaopita eneo hilo kutoa fedha, wanapokataa huwadhuru au hata kuwatishia kwa maneno makali.
“Maisha ni magumu kuliko unavyoweza kufikiri, wakubwa wanatubaka kadri wanavyotaka hasa inapofika usiku, hata ukilia haisaidii kwa sababu hakuna wa kukusaidia,” anasema mtoto mmoja (jina tunalo), huku watoto wa kike wakionekana kuingiliwa na wanaume wengi kwa staili na nyakati tofauti na wanapokataa hupigwa.
“Ni kweli wapo watoto ambao wanatumika katika wizi, wanakuwa kama chambo, wengine wanatumika kuuza dawa za kulevya kwa maana ya kutumwa kupeleka dawa hizo sehemu fulani au kwa mtu fulani au hata kuuza,” anasema mtoto mwingine na kuongeza kuwa yeye hayafurahii maisha haya lakini hana la kufanya kwa sababu wazazi wake wameshakufa na alikuja jijini toka mwaka 2005 akitokea Mwanza, hana mawasiliano na wazazi wake tangu wakati huo wala hajui chochote kwani alikuja akiwa na umri wa miaka 11 baada ya wazazi wake kutalakiana.
Polisi wanajua nini?
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipohojiwa kuhusiana na taarifa hizo aliomba apelekewe maswali ndipo ajibu.
Baadaye mwandishi aliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela ambaye alitoa ushirikiano mzuri kwa kusema kuwa anasikitishwa na taarifa hizo na kwamba anaangalia namna ya kushirikiana na viongozi wengine ili kuona nini wanaweza kufanya.
“Tatizo la watoto wa mitaani ni kubwa, polisi pekee hatuwezi ni lazima Watanzania kwa ujumla tushirikiane kuona namna ya kukomesha tatizo hili la watoto wa mitaani nchini,” anasema Kenyela.
Serikali na mikakati
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto Ummy Mwalimu katika mahojiano na mwandishi wa makala haya anakiri kuwepo kwa tatizo kubwa la watoto wa mitaani na kusema Serikali imeandaa mkakati maalumu kuwasaidia watoto hawa.
Idadi ya watoto wa mitaani Dar
“Ni kweli tatizo ni kubwa, watoto wa mitaani wanaongezeka, miaka kadhaa iliyopita walikuwa 3000 hivi, sasa wako zaidi ya 6000. Kama Serikali tumeunda mkakati dhabiti wa kupambana na hali hii, sasa tumeuwasilisha kwa wataalamu ili kupata ushauri zaidi na kwamba naamini suala la watoto wa mitaani huenda likawa historia,” anasema Ummy.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wanaona hiyo ni kauli tu ambayo haina utekelezaji kwani suala la watoto wa mitaani limekuwapo kwa miaka mingi huku viongozi wakiendelea kutoa ahadi zisizo na utekelezaji.
Kuna taasisi nyingi zisizo za kiserikali ambazo nazo ni kama zilizo nyingi zinaonekana kutofanya jitihada kubwa kupambana na tatizo hili. Hata hivyo Waziri anasisitiza kuwa watoto hawa wa mitaani watasaidiwa kwa vitendo.
Comments
Post a Comment