NI JUKUMU LA JAMII NZIMA KUPAMBANA NA UKATILI DHIDI YA WATOTO WALEMAVU.

UNICEF kupambana na ukatili dhidi ya watoto walemavu..

Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, limeripoti watoto wenye ulemavu ulimwenguni ni waathiriwa wakubwa wa mateso, ubakaji na wengi wao hawasajiliwi baada ya kuzaliwa ikilinganishwa na wasiokuwa na ulemavu.
                       Mdau wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu watoto UNICEF

Kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF iliyotolewa jana katika mkutano wake mjini Da Nang, Vietnam, watoto wenye ulemavu wanabaguliwa na kutengwa katika jamii kwa sababu wazazi hawatoi uangalizi wa kutosha kwa watoto hao, likiwemo la kutowaandikisha wanapozaliwa.
Mkugenzi Mkuu wa UNICEF, Anthony Lake, amesema ukosefu wa takwimu za watoto walemavu katika nchi nyingi duniani, umewafanya watoto hao kutokujuilikana na kutambuliwa. UNICEF inakadiria kuwa kila penye watoto 20 wenye umri wa miaka 14, mmoja wao ni mlemavu wa moja kwa moja au anaishi na aina fulani ya ulemavu.
Lake amesema hali inayowakabili watoto wenye ulemavu duniani ni ya kutisha, na kutowasajili kumechangia sana mateso na idhilali juu yao, huku wengi wao wakikosa msukumo wowote wa kuwaendeleza kama watoto.

Haja ya kujua  idadi ya walemavu duniani ni muhimu
                                            Kijana mwenye ulemavu wa miguu

Mkurugenzi huyo ameongeza kusema na hapa namnukuu: "Kama hatutakuwa na mfumo wa kujua idadi ya watoto wenye ulemavu, hatutaona umuhimu wao."
Miongoni mwa unyanyasaji unaowakabili watoto hao ni ule unaohusiana na ngono. Kutokupewa elimu ya mahusiano na madhara ya magonjwa ya zinaa kunawaweka watoto hao katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya magonjwa hayo.
Kwa kukosa kwao mafungamano ya kawaida ya kibinaadamu, watoto wengi wenye ulemavu wanakuwa wakimya na wanashindwa kujua mipaka katika mahusiano yao na wengine.

Pamoja na mengine, ripoti hiyo ya UNICEF inagusia vitendo vya kuwawinda na kuwakata viungo watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania kwa imani za kishirikina, ikiitaka jamii kubadili mtazamo wake kuhusu watoto wenye ulemavu, kwa kuwapatia huduma za kijamii, ikiwemo elimu na afya
Ripoti hiyo imetaka msisitizo mkubwa uwekwe katika kile ambacho watoto wenye ulemavu wanaweza kufanya kulikoni kuangalia tu katika kile wasichoweza kufanya watoto hao.
''Mara nyingi nimeona katika televisheni watoto wenye ulemavu hawapati fursa ya kwenda shule, kutokana na mtazamo wa watu kuhusu watoto walemavu, ambao sio sahihi,'' amesema Nguyen Phoung Anh mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16 kutoka Vietnam.
Phoung Anh mwenye maradhi ya mifupa, amekuwa mtu mashuhuri sana nchini Vietnam, baada ya kuonesha kipaji chake katika televisheni ya nchi hiyo akiimba na kucheza akiwa katika kiti chake. Anasema licha ya kila mtu kujua kuwa ni kosa kuwatenga watu wenye ulemavu, bado watu wanawachukulia vibaya watu wenye ulemavu kama vile sio binadamu wa kawaida.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mtoto wa kike mwenye ulemavu yuko kwenye hatari kubwa zaidi kuliko mwenzake wa kiume, na amekuwa akiachwa nyuma sana katika kila jambo.

UNICEF imeitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza nguvu zaidi katika kupambana na matatizo yanayowakabili watoto wenye ulemavu, kwani dola milioni 100 zilizotolewa na wafadhili ni  theluthi moja  tu ya zile zinazohijitaka kuwasaidia watoto hao.

Suala hili ni kubwa zaidi katika nchi za kiafrika  kama vile Tanzania, kwa utafiti uliofanywa na timu nzima ya HEAR MY VOICE umebaini watoto wengi walio na ulemavu hawathaminiwi katika jamii na matokeo yake wanafichwa ndani na wengine kuuawa kabisa, kutokana na mtazamo uliopo katika jamii kuwa ulemavu ni MKOSI AU LAANA, hivyo familia yenye mtoto mlemavu hutengwa na jamii kwa kuhusisha ulemavu na imani za kishirikina au laana katika familia.

Ushauri wangu kwa jamii: Imani potofu na mitazamo hasi kuhusu ulemavu ni vitu vinavyoturudisha nyuma katika juhudi za kuwa na jamii yenye upendo kwa kila mtu bila kujali tofauti tulizonazo, iwe ni ulemavu au hata umasikini na rangi. Kwa suala la ulemavu sisi sote ni kazi ya mikono ya Mungu, tofauti iliyopo kati yetu ni mapenzi yake. Tukiweza kuyazingatia hayo naamini kila mmoja katika jamii ataifurahia dunia tunayoishi na hata walemavu wataona dunia ni sehemu nzuri ya kuishi.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU