HII NI KWA JAMII NZIMA.




Maisha ya hapa dunia ni ya kupita tu, mali na vyote vionekanavyo ni mapito pia. Ila upendo na kuthaminiana bila kujali tofauti zetu ni hazina kubwa sana hapa duniani. 


Jamii inasikitisha sana yawezekana ni kwa kujua au kutokujua, lakini kweli inasikitisha sana, JANA nimeonekana mtu wa ajabu baada ya kukaa na watoto wa mitaani maeneo ya Bunda stand mpya, Mzee mmoja msomi na mwenye heshima kubwa hapa wilayani alinifuata na kuniambia kwanini nimekaa na watoto wahuni wa mitaani, akaenda mbali zaidi na kusema hawa ndio majambazi wa wilaya hii. Akatokea Dereva mmoja ambaye yeye hata hakutaka kujua nilikuwa naongea nini na wale watoto yeye akawafukuza kwenye viti, mbaya zaidi akawapiga na kuwatupia matusi mazito. Baada ya hapo huyo dereva akaniambia nilikuwa nakuheshimu sana ila leo nimekuchukulia tofauti kabisa, akasema "nilidhani umeenda shule umeelimika kumbe shule haijakusaidia" utakaaje na watoto wachafu namna hii, hawa ni vibaka wa stand wewe unakaa nao.

Kweli iliniumiza sana.. Mpaka sana bado siamini kama kweli wale watu walikuwa wanajua walitendalo na kama walijua walitendalo jamii inaelekea wapi? Kwanza wale watoto umri wao ni kati ya miaka mitano na saba, walikuwa watoto wawili ambao kwa maelezo yao ni ndugu ambao hawawajui wazazi wao tangu wamezaliwa. Nilijiuliza maswali mengi sana ila nikaona ni vema jamii tukakumbushana haya, 
Kwanza wale ni watoto kama watoto wengine, pili wao hawakupenda kuishi katika hayo mazingira na tatu wao sio sehemu ya tatizo, wamejikuta wapo katika mazingira hayo. 

Ni kweli watoto wa mitaani wana tabia ambazo sio nzuri ila ni wewe na mimi tunaweza tukawakosoa na kuwaelekeza njia sahihi za maisha hata kama hatuna pesa wala msaada wowote kwao ila sio kwa kuwaona ni watu wasiofaa kabisa katika jamii, mpaka tunadiriki kuwapiga na kuwabebesha matusi mazito. 

Tabia hii ya udokozi na udanganyifu kwa watoto wa mitaani inatokana na mazingira magumu wanayoishi, lakini kama taasisi mbalimbali na mashirika binafsi yakijitokeza kusaidia hili kundi, na pia nguvu ya serikali ikaimarishwa katika kuwasaidia hawa watoto naamini hizo tabia zitafutika zenyewe. Na hilo suala la kuwasaidia ili lizae matunda ni lazima lifanyike kipindi chote sio wakati wa sikukuu pekee, hapo ndio utasikia makumpuni yametoa msaada kwa watoto yatima, watoto wa mitaani au watoto wenye ulemavu.

Tubadilike kwa kulielewa jambo hili, kuwahurumia watoto wa mitaani haitawasaidia ila ili tuwasaidie kwa moyo wote ni vema tukavaa uhalisia wa matatizo yao, tujihisi maumivu kwa shida na taabu wanazopata katika maisha yao, kwa kuguswa na mateso yao hapo tutaoweza kuwasaidia iwe kwa mawazo au hata kuwa nao karibu kwa kuwapenda na kuwachukulia kuwa na wao ni sehemu ya jamii.



Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU