CHANZO CHA WATOTO WA MITAANI

WAKATI  nchi za Afrika zilipofanya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Juni 16 ikiwa ni njia mojawapo ya kuwakumbuka na kuwaenzi watoto wa Afrika Kusini ambao walifanyanyaswa na kubaguliwa na hata kuuawa wakati wa ubaguzi wa rangi, Tanzania inaelezwa kuwa haina takwimu sahihi za watoto wa mitaani.

Kukosekana kwa takwimu hizo kumeelezwa kuwa kunatokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuongezeka siku hadi siku kila sehemu kwa watoto hao, hali ambayo inawafanya watendaji wa Serikali wakose takwimu hizo.Pia, inaelezwa kwamba watoto wengine wanaishi katika mazingira magumu  na hatarishi kwa afya zao, lakini bila kutambuliwa.

Wakiwa mitaani huko, watoto hao wamekuwa wakikumbana na mambo mbalimbali yakiwamo kubakwa, kunyanyaswa, kudhalilishwa kijinsia, vitendo wanavyofanyiwa na watu mbalimbali wakiwamo watoto wenzao na hata watu wazima.

Ugomvi wa wazazi kwenye familia,kutowajibika ipasavyo na umaskini ni  sababu mojawapo ya zinazofanya watoto hao kutoroka na kuingia mitaani na kuishi katika mazingira magumu, hali ambayo inaonyesha wazi kuwa, jamii imeshindwa kuwajibika ipasavyo.Watoto hao ambao wanategemewa kuwa viongozi wa baadaye, lakini wanaonekana kuwa na maisha magumu yanayosababisha kukosa elimu, malezi bora jambo ambalo linawafanya waishi katika mazingira hatarishi.

Ili kutatua tatizo hilo, Serikali, jamii na wadau mbalimbali zikiwamo taasisi za kiraia zina wajibu wa kushirikiana  kwa pamoja na ili kuhakikisha kuwa, wanatoa elimu kuhusu suala hilo.Mbali na wadau hao, walimu pia wana nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi kupiga vita suala la kutupwa watoto,unyanyasaji, ubebaji wa mimba bila ya kujiandaa jambo ambalo linaweza kupunguza kama si kumaliza  tatizo hilo.


Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU