YOTE YANAWEZEKANA CHINI YA JUA.



                              MUNGU ANABADILI MAISHA.
RACHEL MWANZA, KUTOKA MTOTO WA MITAANI HADI MCHEZA FILAMU NYOTA AFRIKA.








KINSHASA, DRC
MAISHA ya mwigizaji Rachel Mwanza yamebadilika katika miaka ya hivi karibuni. Binti huyo mdogo alikuwa mmoja wa watoto waliozagaa mitaani katika Jiji la Kinshasa nchini DRC, lakini hivi sasa ni mmoja wa wacheza filamu nyota barani Afrika.

Mbali na kuwa mwigizaji nyota, Rachel ameshinda tuzo nyingi na pia kutembelea katika miji mbalimbali mikubwa duniani kwa ajili ya kupokea tuzo.

Binti huyo alikuwa akikatiza katika moja ya mitaa ya Kinshasa wakati nafasi ya kuigiza filamu ya Rabelle (War Witch) ilipomshukia. Waandaaji wa filamu hiyo walibahatika kumuona katika kipindi kimoja cha televisheni cha watoto wa mitaani kilichorushwa nchini DRC na kuvutiwa naye.

Ilikuwa ngekewa kwake, lakini alipatwa na mshtuko mkubwa baada ya kufikishiwa taarifa hizo. Hakuwa akifahamu lolote kuhusu uigizaji wa filamu.

Lakini kutokana na kipaji chake kilichojificha na uelewa aliokuwa nao kuhusu hadithi ya filamu hiyo, aliamua kujitosa katika kazi hiyo.

Kutokana na umri wake, bado ni vigumu kwa Rachel kufikia viwango vya wacheza filamu nyota wa Hollywood, lakini kutokana na maisha aliyoyazoea, alimudu kucheza filamu hiyo kwa umahiri mkubwa.

Kwa sasa, Rachel ana umri wa miaka 16, lakini tayari ameshashinda tuzo kadhaa, ikiwemo ya mwigizaji bora wa kike (Silver Bear) mwaka jana wakati wa Tamasha la Kimataifa la Filamu la Berlin lililofanyika nchini Ujerumani.

Binti huyo kutoka DRC pia alishinda tuzo ya mwigizaji bora wa kike iliyotolewa katika Tamasha la Filamu la Tribeca.

Hivi sasa, Rachel ni mwigizaji mtoto maarufu zaidi barani Afrika. Amekuwa akitembelea sehemu mbalimbali na hivi karibuni alishiriki katika sherehe za utoaji wa tuzo za Oscar, ambako filamu yake ya War Witch ilishinda tuzo ya filamu bora ya lugha ya kigeni.

Japokuwa filamu hiyo ilipigwa kumbo na ile ya Amour, lakini imepata mafanikio na mauzo mazuri na kumwezesha Rachel kuteuliwa kuwania tuzo mbalimbali.

War Witch imeteuliwa kuwania tuzo 12 katika tuzo za Canada, ambapo Rachel alishinda tuzo ya mwigizaji bora wa kike. Filamu hiyo pia imeteuliwa kuwania tuzo nane katika tuzo za Quebec Jutras zitakazotolewa Machi 17 mwaka huu.

Filamu hiyo inaelezea kisa cha mwanajeshi mtoto katika mji mmoja kusini mwa Jangwa la Sahara. Ni filamu iliyochezwa katika mazingira magumu na maeneo ya kutisha, ikiwa inaelezea matukio ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya nchi za kiafrika.

Katika filamu hiyo, Rachel ametumia jina la Kimona. Alitekwa na magaidi akiwa na umri wa miaka 12 na kulazimishwa kushika bunduki aina ya AK 47 na kuua.

Kimona alifanikiwa kuwatoroka magaidi hao kwa msaada wa rafiki yake wa kiume mwenye umri wa miaka 15, ambaye ni mchawi na alikuwa akitaka kumuoa.

Licha ya matukio ya kutisha na vita kila kukicha, Kamona na kijana huyo wanaangukia katika mapenzi. Walidhani wamefanikiwa kukimbia vita, kumbe wanajikuta wakiingia kwenye matatizo mengine mazito.

Ili kujinusuru, Kamona anahitajika kurejea mahali alikotoka na kuyasahau yaliyopita. Wanafanya hivyo huku vita vikiwa vimepamba moto.

Kuwepo kwa Rachel katika tuzo za Oscar zilizotolewa mwaka huu mjini Los Angeles, kumewafanya watayarishaji wengi wa filamu duniani wamtupie macho.

Hata hivyo, kwenda kwake Marekani kulizingirwa na mizengwe mingi, ikiwa ni pamoja na kupata ugumu wa kupewa viza.

Binti huyo amekuwa akipongezwa kutokana na kujitoa katika maisha ya mitaani na kuwa mwigizaji nyota. Amefanya kile ambacho watoto wengi wa aina hiyo wameshindwa kukifanya.

Ilimchukua miaka 10 mtayarishaji filamu wa Canada, Kim Nguyen kuandaa hadithi ya filamu hiyo, lakini umahiri wa Rachel umeifanya iwe na mvuto wa aina yake, utadhani binti huyo amekuwa akiigiza maisha yake yote.

Waandaaji wa filamu hiyo waliweza kumtumia vyema Rachel kwa mbinu, ambazo zilimwezesha kutoa kitu bora japokuwa hakuwa na uwezo wa kusoma na kuandika. Tangu wakati huo, Kim na wenzake wamekuwa wakimfanyia mipango ya kumpeleka shule. Wamedhamiria kumwendeleza kielimu na kimaisha.

Rachel alijikuta akiwa mtoto wa mitaani baada ya wazazi wake kumtelekeza miaka kadhaa iliyopita. Alikwenda kuishi na bibi yake, ambaye baadaye alipoteza kibarua chake na hakuwa na uwezo wa kumtunza.

Baada ya kutelekezwa na bibi yake, Rachel aliamua kujitosa mitaani kwa ajili ya kutafuta riziki ya kuendesha maisha yake, hadi Kim na wenzake, akiwemo Pierre Even na Marie-Claude Poulin walipomuona na kuamua kufanya naye kazi.

Tangu wakati huo, maisha ya Rachel yamebadilika. Licha ya kujiendeleza kielimu, amepangiwa nyumba ya kuishi mjini Kinshasa. Pia amecheza filamu nyingine, inayojulikana kwa jina la Kinshasa Kids, ambayo imeongozwa na Marc-Henri Wajnberg kutoka Ubelgiji.

Comments

  1. Naamini kwa mfano huu, hata hapa kwetu Tanzania inawezekana kwa mtoto wa mitaani kuwa na kipaji zaidi hata ya RACHEL, ila tatizo kubwa ni mitazamo hasi ya jamii juu ya hawa watoto, kwa pamoja tushirikiane kuendeleza vipawa walivyonavyo hawa watoto ili iwe ni jia pekee ya wao kijikimu kimaisha.

    ReplyDelete
  2. Nikweli kabisa,tena kuna watoto ambao hata uwezo wa kufanya vizuri darasani wanao ila kama ulivyosema mitazamo hasi kwa jamii zetu ni kikwazo kwa maendeleo ya hawa watoto.

    ReplyDelete
  3. Wizara husika ingekuwa na taasisi kwa ajili ya maendeleo watoto wa mitaani, au hata wizara ya michezo ingekuwa ina ligi ya watoto wa mitaani ili kuvumbua vipaji vyao, na hata sanaa mbalimbali kama vile uimbaji, uchoraji nk

    ReplyDelete
  4. Mbali na wizara pia mashirika kama vile TBL, VODACOM, AIRTEL, TIGO na watu binafsi wangekuwa na utaratibu wa kudhamini mashindano mbalimbali ya watoto wa mitaani, mimi naamini hapo ndipo tungetambua kila mtu hapa dunia yupo kwa sababu na si kwa bahati mbaya.

    ReplyDelete
  5. Kwa nguvu zetu na uwezo wetu tuwe sauti za hawa watoto.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU