UNYANYAPAA UNAVYOTUMIKA KUWANYIMA FURSA WATU WENYE ULEMAVU.


Na Francis ole Rikanga.

TAFSIRI ya neno ulemavu hutofautiana kutoka kwa mtaalam moja hadi mwingine, kutokana na mazingira ambamo tafsiri hiyo hutumika.

Baadhi ya wataalam hutafsiri kuwa ulemavu ni ukosefu wa viungo muhimu katika mwili wa binadamu na wengine husema ulemavu ni ukosevu wa fikra.


Pamoja na watalaam na watu mbalimbali katika jamii kutofautiana, Bw.Fredy Msigallah ambaye ni Afisa mtetezi wa Haki za watu wenye Ulemavu kutoka CCBRT anasema ulemavu ni kukosekana au kuwepo kwa ukomo fursa ya kushiriki katika maisha ya kijamii kwa kiwango sawa na watu wengine kwa sababu za kimaumbile, kiakili na kijamii.

Kwakwe ulemavu si ukosefu wa viungo bali ni ukosefu wa fursa ya kushiriki katika maisha ya jamii kunakosababishwa na vikwazo vya mazingira, kimtizamo na mfumo uliopo ndani ya jamii.

Ni ukweli usiopingika kuwa licha ya kuwepo kwa vikwazo bado kuna watu wenye ulemavu waliodhihirisha kuwa ulemavu sio viungo. Ipo mifano hai ya watu wenye ulemavu iwe ya viungo, kuona, kusikia au ngozi (Albino) ambao wamewezeshwa na sasa wanatoa mchango mkubwa katika jamaii bila kujali ulemavu walionao.

Baadhi ya watu wenye ulemavu walioidhihirishia jamii kuwa ulemavu sio viungo ni Mwalimu Khalid Sadick ambaye ni mlemavu wa macho kwa sasa anafundisha katika shule ya Msingi Ndugumbi iliyopo Magomeni jiji Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani  nchini  bw. Jotram Kabatere ambaye ni Mlemavu wa miguu ameonyesha uwezo wa walemavu baada ya kugundua na kutengeneza alama za barabarani kwa  watu wenye ulemavu ‘Disabilities Road Sign’ ambayo hadi sasa havijaanza kutumika bila ya kutolewa sababu za msingi.

Bw.Msigallah ni mlemavu wa miguu lakini msomo mwenye shahada ya uzamili katika masuala ya utawala na sera za umma aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Manchester  iliyopo Uingireza.

Mbunge wa Lindi Mjini Salum Baru’ani ni jibu lingine kwa wale wenye mtizamo hasi juu ya watu wenye ulemavu hususan wa ngozi “Albino”. Baada ya mauaji wa kupindukia kwa watu wenye ulemavu wa ngozi wananchi wa Jimbo la Lindi Mjini waliudhihirishia umma wa watanzania kuwa wana imani na watu wenye ulemavu wa ngozi na kumpa ridhaa kuwa mwakilishi wao katika chombo muhimu cha kutunga sheria.

Kwa kuzingatia mifano hiyo ni muhimu jamii ikubali kuwa ulemavu sio viungo na wapo watu wenye viungo vyote, rangi sawa, akili sawa, elimu kubwa lakini hawajaonyesha mchango wowote katika jamii na hawana ulemavu wowote.

Hali hii inadhihirisha kuwa ulemavu ni mtazamo hasi ndani ya jamii na sio upungufu wa viungo unaomfanya awe au asiwe na mchango katika jamii .

Kama ulemavu ni ukosefu wa viungo ni vizuri kila mtu katika jamii aelewe kuwa ni mlemavu mtarajiwa aidha kwa ugonjwa au kwa usafiri ambapo ajali imekuwa ikizalisha walemavu wa viungo ambao pengine ni kati ya wale waliokuwa na kiburi isiyo na kifani ya kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu.

Ni ukweli usiofichika kuwa kundi hilo limesahaulika na jamii na hata serikali, na kusababisha kukosa huduma muhimu za kijamiia, kisiasa na kiuchumi kwa kiwango kikubwa.

Taarifa za utafiti wa walemavu Tanzania uliofanywa na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) mwaka 2008 unaonyesha kuwa walemavu ni asilimia 7.8 kiasi sawa kwa wanaume na wanawake.

Kundi hili si kubwa kiasi cha serikali kushindwa kulihudumia na kulipa mahitaji yanayostahili. Lakini kutokana na ufisadi na ubinafsi uliojaa katika taasisi husika watu hawa hujikuta wakikumbukwa pale tu, linapotokea tukio au janga kama vile mauaji ya maalbino.

Ukosefu wa huduma mbalimbali za jamii kwa watu wenye ulemavu, kunawafanya waathirike kisaikolojia na wengi wao kukata tamaa.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linakadiria katika nchi nyingi duniani kiwango cha ulemavu ni kati ya asilimia 10 hadi 12.16

Agalabu utafiti wa NBS  mwaka 2008 ulionyesha kuwa aina na idadi ya walemavu kwa asilimia ni macho milioni 1.2 sawa na asilimia 4, matatizo ya kutembea 956,669 (3) uziwi 600,000 (2) albino 8,193 kiasi ambacho kinawezekana ikawa ni zaidi ya hiyo kwa sasa.

Pia, utafiti ulionesha kuwa, watoto walio na umri wa chini ya miaka 15, ni asilimia 50 kati ya hao walizaliwa na ulemavu au waliupata kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja.

Kwa watu wazima asilimia 12 walisema walizaliwa na ulemavu huo na asilimia 14 walitaja baridi yabisi kama chanzo cha ulemavu walionao huku asilimia sita wanaamini kuwa uchawi ndiyo chanzo cha ulemavu walionao, wakati ulemavu mwingine ambao utafiti huo haukutaja unasababishwa na ukatili majumbani ‘Domestic violence’ ambayo hufanywa aidha na wanaume au wanamke.

Pia, visiwani Bi. Asha Alfani ambaye ni mlemavu wa macho aliupata kutokana na kipigo kwa mumewe  ambacho pia kilisababisha mtoto wake kufia tumboni kutokana na kuvunjika mbavu na kuzaliwa akiwa amekufa.

Matokeo mengine ya utafiti yanaonyesha kuwa viwango vya ulemavu ni vikubwa  kwa maeneo ya vijijini kwa asilimia 9.4 sawa na watu milioni 2.9 ukilinganishia na maeneo ya mijini ambao ni asilimia 7.3 sawa na watu 560,000 huku kiwango cha ulemavu ni kikubwa kwa Tanzania bara kwa asilimia tisa sawa na watu milioni 4.4 kuliko Tanzania Zanzibar asilimia 7 sawa na watu 55,355.17.

Aidha tafiti kadhaa zilizofanywa katika baadhi ya Tanzania bara na Tanzania Zanzibar, zilibaini kuwa watu wenye ulemavu hawapati fursa sawa katika kupata haki ya elimu kutokana na mila na fikra potofu kuwa kuwasomesha watoto wenye ulemavu ni uharibifu wa rasilimali.

Tafiti hizo zinaonyesha kuwepo uhaba mkubwa wa vifaa vya kufundishia katika shule za walemavu, mintarafu watafiti waliotembelea shule ya watoto wasiona ya Kilakala mkoani Morogoro walibaini uhaba mkubwa wa vitabu na vivaa vingine vya kufundishia watu wasiona, na vifaa rafiki kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Matokeo ya utafiti kuhusu watu wenye ulemavu Tanzania ya mwaka 2008, yanaonyesha kuwa ni watoto 4 tu kati ya 10 wenye umri kati ya miaka 7 na 13 ndio wanaopata elimu ya msingi na wanaopata elimu ya sekondari ni asilimia 5.

Kwa mujibu wa matokeo hayo waliopata elimu ya juu ni chini ya asilimia moja na asilimia 48 ya watu wenye ulemavu hawajui kusoma wala kuandika ukilinganisha na asilimia 25 ya wale wasiokuwa na ulemavu.

Uchunguzi umebaini kuwa, baadhi ya sababu zinazofanya watoto wenye ulemavu wakose elimu bi pamoja na wazazi kuwaficha watoto hao nyumbani, miundombinu isiyorafiki katika shule

Katika masuala ya ajira watu wenye ulemavu wanaendelea kunyanyapaliwa na kufanya wabaki nyuma licha ya  katiba kutoa fursa ya wao kupata haki ya kufanya kazi sawa na watu wengine.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya watu wenye ulemavu (2010) Sera ya Taifa ya Watu wenye Ulemavu (2004), na mkataba wa Kimataifa wa Haki za watu wenye ulemavu (ambao Tanzania umeuridhia) vinasisitiza haki sawa ya ajira kwa watu wenye ulemavu.

Pamoja na kuwepo kwa sheria, mikataba hizo, bado hali ya ajira kwa watu wenye ulemavu iko duni. Kwa mfano matokeo ya utafiti uliofanywa na CCBRT kwa kushirikiana na Radar Development mwaka 2010 kwa Dar es salaam tu, inaonyesha viwanda 125 vyenye wafanya kazi wasiopungua 25,000 asilimia 0.7 ni walemavu.

Ikumbukwe kuwa kwa mujibu ya sheria ya watu wenye ulemavu (2010), kila mwajiri mwenye wafanyakazi 20 au zaidi inapaswa kuhakikisha kuwa asilimia 3 ya wafanyakazi hao ni watu wenye ulemavu lakini sheria hiyo aidha haijulikani kwa waajiri au inavunjwa makusudi.

Ibara ya 9 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu na ambao Tanzania umeridhia unaeleza kuwa pamoja na mambo mengine, miundombinu ya majengo inatakiwa kuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kufanya kazi na kupata huduma katika ofisi mbalimbali.

Lakini pamoja na sheria hiyo kuwepo bado miundombinu katika ofisi, shule na  vyombo vya usafiri nchini sio rafiki kwa watu wenye ulemavu na kwa sababu ya miundombinu hiyo hasa katika elimu watu hawa hujikuta wakikata tamaa ya kuendelea na masomo.

Kutokana na adha wanaopata wanaposubiri usafiri wa daladala katika barabara zetu ambazo hakuna alama wala miundombinu inayoweza kutumika na watu wenye ulemavu, hususan vituo vya watu wenye ulemavu wa aina fulani, mintarafu wasiosikia hujuukuta wakikaa vituoni kwa muda mrefu bila kupata msaada, lakini pia wanapoingia madarasani na hata wanapojisikia kutumia vyoo shuleni bado huwa wanateseka.

Majengo mengi ya ghorofa ‘Ofisi za serikali na mashirika ya umma a watu binafsi’ hayana miundombinu mahsusi ya kuhudumia watu wenye ulemavu.

Suala hili huwaathiri walemavu katika shughuli zao ya kila siku ni vyema likaangaliwa upya ili kupunguza usumbufu wanaopata.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU