AJIRA KWA WATOTO NI ZAO LA UBEPARI.
Tarehe 12 Juni ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira kwa Watoto. Katika maadhimisho haya hufanyika makongamano na hafla mbalimbali kujaribu kupiga kampeni dhidi ya ajira za watoto. Tanzania ni miongoni mwa nchi 174 zilizoridhia azimio namba 182 la kukomesha utumikishaji watoto chini ya umri wa miaka 18.
Hakuna anayepinga juu ya kuwepo ajira
za watoto kila mahala. Kwa mfano, kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti la
Mwananchi kupitia mradi wa kupambana na ajira ngumu kwa watoto
Zanzibar, zaidi ya watoto 15,000 ndani ya Zanzibar wanajishughulisha
na ajira tena zile ngumu.
Aidha, kuna vilio kama hivyo vya ajira
za watoto pia Tanzania Bara hususan katika maeneo ya machimbo ya
migodini yakiwemo Mererani mkoani Manyara, maarufu kwa uchimbaji wa
madini aina tanzanite.
Suala msingi hapa ni kiini cha jambo
hili. Ukija hapa kwenye chanzo ndio utaona dhihirisho la kuchanganyikiwa
wanademokrasia na mfumo wao wa kibepari. Kwanza kabisa, mfumo huu
umeshindwa kutambua ni nani hasa mtoto. Kwa mfano, kifungu cha 4 cha
Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka, 2004 kinamuelezea mtoto
kama mtu mwenye umri chini ya miaka 14. Lakini kwa sheria hiyo hiyo kwa
ajira zilizo katika sekta hatarishi, mtoto maana yake ni mtu mwenye
umri wa chini ya miaka 18. Kwa hivyo, upande mmoja ni miaka 14 na upande
wa pili ni chini ya miaka 18.
Aidha, mfumo huu huzuiya binti
aliyebaleghe asiolewe kwa kigezo kwamba ni mtoto/mwanafunzi ilhali
hakuna makosa binti huyo kuziniwa. Kinachozuiliwa ni kuwa asiolewe tu.
Mfumo huu unajifanya kupaza sauti juu
dhidi ya suala la ajira kwa watoto hususan ajira hatarishi kama za
uvuvi, migodini, viwandani nk. ila hauna namna ya kuwahakikishia raia
jumla sio watoto tu, hali nzuri ya maisha. Bali mfumo huu kwa sera zake
za kinyonyaji, makodi na dhulma ya kiuchumi ndio unapelekea wazazi na
kila wanyonge kushindwa kujimudu kimaisha na badala yake huhitaji wapate
msaada wa watoto wao, hata bado wakiwa wadogo. Huku mfumo huu
unadanganya kwa kauli mbiu ya uwongo ati kusoma shule ni haki ya msingi
ya mtoto. Vipi mtoto huyu ataweza kwenda shule bila ya kudhamini maisha
yake na maisha ya wazazi wake ? Tafiti zote kuhusu ajira kwa watoto
zinaonesha chanzo kikuu ni umasikini.
Baadhi ya watoto huwa kwenye mazingira
magumu ambayo huwafanya ni lazima watafute shughuli ya kufanya ili
kujipatia riziki yao. Ubepari umeshindwa kudhamini maisha ya watoto wa
kawaida na mayatima katika kuhakikishia ustawi wao. Matokeo yake baadhi
yao wamekuwa hawana jinsi amma wawe ombaomba au hulazimika kufanya kazi
ngumu ili wajipatie kipato cha kujikimu wao na familia zao.
Mfumo wa kidemokrasia na wanaojiita
wanaharakati wake wamezingirwa na upofu wa makusudi wa kujitakia,
matokeo yake wamekuwa hawatoi masuluhisho kamili na ya uhakika juu ya
suala hili na mengineyo kwa jamii.
Ukweli wa mambo ni kuwa mfumo wa
kibepari ndio tatizo kwani kupitia kipimo chake cha maslahi umekuwa
unawanyonya watu wote na sio watoto tu kwani tunaona maisha ya raia
jumla wawe watoto, vijana au wazee yamo katika hali mbaya.
Suala hili pia linadhihirisha unafiki
mkubwa kwa mfumo huu wa kidemokrasia/kibepari. Kwa kuwa tunaona
wanaojishughulisha kwenye tasnia zinazoitwa za burudani, kama vile
muziki na filamu huwa wao kamwe hawatajwi kama ni watoto ambao wapo
kwenye ajira haramu. Imekuwa maarufu kushuhudia watoto wadogo hata wa
chini ya miaka 14 wakishughulishwa kwenye ajira za filamu na miziki. Kwa
mfano, wasanii kama Britney Spears, Lil bow wow, Lil Wayne, Mr Blue,
nk. walianza kuvuma kwenye fani za muziki wakiwa chini ya umri wa miaka
15. Pia tumeshuhudia wasanii kama vile Macaulay Culkin, Lulu nk.
walianza kuvuma kwenye tasnia ya filamu za maigizo ilhali wakiwa
wadogo bado.
Kwa hakika ni wazi kwamba mfumo wa
kibepari na nidhamu yake ya kisiasa ya kidemokrasia imefeli
kuwahakikishia wanadamu maisha salama. Wawe watoto au watu wazima. Na
wanachojaribu ni kujificha mgongo wazi.
Comments
Post a Comment