WITO KWA WAZAZI




OFISA Elimu wa Manispaa ya Iringa anayeshughulikia elimu ya msingi, Angelous Kisiga, amewataka maofisa watendaji wa kata, mitaa na wenyeviti wa vitongoji katika manispaa hiyo, kuendesha msako wa kuwafichua wazazi wenye tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu ili wasipatiwe elimu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, ofisa elimu huyo alisema kuna baadhi ya wazazi wenye tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu badala ya kuwapeleka shuleni, jambo ambalo ni sawa na ubaguzi.

Aliwataka kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kuanza masomo wanapelekwa shule bila kujali kama ni walemavu au siyo walemavu.

Pia aliwataka wakazi wa manispaa hiyo, kusaidiana na Serikali katika kuwafichua wazazi wenye tabia hiyo ya kuwaficha watoto wenye ulemavu, ili wapatiwe elimu kama ilivyo kwa watoto wasiokuwa walemavu.

Kisiga alisema watoto wote bila kujali ulemavu wao, wanayo haki ya msingi ya kupatiwa elimu, jambo ambalo lazima jamii iwafichue wazazi ambao hawapo tayari kuwapeleka shule, ili wakaanze masomo.

“Tatizo lililopo ni kwamba, wazazi wanawaficha watoto wenye ulemavu ili wasianze masomo wakati watoto hao wana haki ya kupewa elimu kama ilivyo kwa watoto wengine.

“Ubaguzi huu lazima jamii iukatae na iwafichue wazazi hawa ili wachukuliwe hatua, ikiwa ni pamoja na kuwapeleka shule watoto hao.

“Jamani ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha mtoto wake anapatiwa elimu ya awali, msingi, sekondari na chuo bila kujali alivyo, kwa kuwa ulemavu siyo kushindwa masomo,” alisema Kisiga.

Kwa upande wao, baadhi ya wazazi wenye watoto walemavu katika Manispaa ya Iringa, waliiomba Serikali kuandaa mazingira mazuri ya kusomea watoto hao kwa kuwa shule nyingi hazina miundombinu inayofaa kwa watu wenye ulemavu.

“Mtoto wangu sijampeleka shule kwa sababu anatambaa japo ana akili ya kuweza kusoma na kama kungekuwa na shule nzuri jirani, ningempeleka.

“Kwa hiyo, Serikali itusaidie, kwani hatupendi kukaa na watoto majumbani, badala yake mazingira ndiyo yanayotulazimisha,” alisema Cresensia Mgimwa, mkazi wa Kihesa, Manispaa ya Iringa.

Comments

  1. yani tunapowaficha watoto haisaidii kitu kwa wazazi zaidi ni kumtenga mtoto na kumyima haki yake ya kujitegemea maishani mwake ambapo atabaki kunyanyasika na kuwa tegemezi kwa familia na pia akijiona yeye ni mzigo kwa familia, Wazazi,ndugu na jamaa msiwafiche watoto walemavu,wapeni nafasi ya kuonyesha vingi walivyojaliwa na Mungu mbali ya ulemavu walonao, Disability ama ulemavu haimaanishi hawawezi,, Give them chance,don't hide them they can do better beyond our expectations.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU