TULITAFAKARI HILI


Ni Watoto wa Mitaani sawa, lakini Vipaji vyao vyaweza kuleta Manufaa au Kuangamiza Taifa hili

(1500)
Views

Ukipita katika viunga vya miji mikubwa ya Tanzania, kuanzia Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Morogoro na kadhalika, hushangai kukuta watoto wakizurura mitaani huku wakati wa usiku wakiwa wamejilaza katika vibaraza vya maduka na katika maeneo ya wazi kama kwenye viwanja vya michezo. Kwao mvua ni yao, baridi ni yao na jua pia ni lao.
Watoto hao wanaishi katika mazingira hatarishi yanayowaweka katika vishawishi vya kufanya uhalifu, kama vile uporaji na kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na biashara nyigine yoyote ile haramu. 
Katika hali ya kukosa chakula, malazi na mavazi kama mahitaji muhimu ya mwanadamu, watoto hawa wamekuwa wakisukumwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu kama njia ya kujipatia riziki.
Wanapokuwa katika mazingira hayo, wanaweza kuja kuwa watu hatari na tishio kwa taifa hili, hivyo kuigeukia jamii ambayo awali ilikuwa ikiwanyooshea vidole bila kuwapatia msaada wowote. 
Watoto hawa wanafanana na shamba zuri lenye rutuba tayari, ambalo likipandwa mbegu njema zinazaa mazao mema. Hawa wanahitaji kuwa na maarifa na maadili mema, lakini wanayakosa kwa kuwa hawana mtu wa kuwasaidia.
Jamii ya Watanzania imekuwa na tabia ya kuwanyooshea vidole watoto hawa wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwabatiza majina ya ajabu pamoja na kuwanyanyapaa kana kwamba walipenda kuishi maisha hayo. Kama taifa, tunajisahau kwamba hata wao ni sehemu ya jamii hii, ni sehemu ya taifa hili. 
Watoto wengi hao wamegeuka na kuwa ombaomba katika migawaha, sehemu zenye mikusanyiko ya watu, ndani ya vilabu vya pombe, vituo vya mabasi ya abiria na wakati mwingine hujibanza pembezoni mwa barabara wakiomba msaada kwa wasamaria wema. 
Tabia ya kuombaomba inaweza kujenga ulemavu kwenye akili hadi kwenye mwili hata kama ana miguu na mikono, na ana umri wa kufanya kazi, lakini bado ataendelea kuwa kuombaomba kwa kuwa ameshalemaa na kujiona kuwa hiyo ndiyo njia nzuri ya kuishi bila kutoa jasho.
Kwa mtzamo wa makala haya ya FikraPevu, haitoshi tu kuwapa watoto hao msaada wa Sh 100, 200, 500, 1000 kama kweli mtu ana nia ya kuwasaidia, bali yatupasa kama taifa kutafuta suluhisho la kudumu la kutatua tatizo hilo sugu la kuwa na watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika mitaa ya miji yetu mikubwa. 
Ni hatari watoto hawa kuendelea kuelea tu bila kuwa na usimamizi mzuri kwa kuwa siku moja tunaweza tukajikuta kama taifa, wakitumiwa vibaya na makundi yasiyolitakia mema taifa hili, kwa mfano kundi la magaidi.
Mifano ya hili ipo mingi katika nchi za wenzetu. Wengi wa watoto hao ndio waliokusanywa na kukabidhiwa silaha na vikundi vya waasi katika nchi hizo.
Kwa upande mwingine, watoto hawa wengi wao wanavyo vipaji mbalimbali vya ubunifu, ambavyo kama wangepata msaada wa kuviendeleza vipaji vyao hivyo, wangekuwa ni watu wa kulifaa taifa lao.
Vipaji vyao hivyo vikiendelzwa vinaweza vikawa rasilimali muhimu ya kuwawezesha kujiajiri wenyewe na hivyo kujitegemea kiuchumi badala ya kusubiri kuajiriwa.
Mkurugenzi wa taasisi binafsi ya mjini Arusha, inayojulikana kwa jina la Gola, ambayo imekuwa akijihusisha na masuala ya watoto hawa wanaoishi katika mazingira magumu, huku pia ikiwa inamiliki Kituo cha Malezi ya Watoto wa aina hiyo, Elisha Maghembe, anasema pamoja na mambo mengine kwamba vipaji kwa vijana si vitu vya kupuuza kwa kuwa hiyo ni silaha inayoweza kumwezesha kujikomboa kimaisha.
Kutokana na ukweli huo, Maghembe anasema Serikali na taasisi nyingine binafsi pamoja na jamii ya Watanzania kwa ujumla wao, wanapaswa kushirikiana kuangalia namna bora ya kuendeleza vipaji mbalimbali walivyonavyo watoto wa mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu.
“Jambo nililoliaona baada ya kukaa na watoto hawa, ni kwamba wana vipaji vya ajabu na vya kipekee ambavyo vikiendelezwa ni ajira tosha kwao, na lakini pia vipaji vyao hivi vinaweza kuliletea taifa letu heshima katika medani za kimataifa upande wa sanaa na ubunifu, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuwasaidia watoto hawa wayafikie malengo yao,” anaeleza Maghembe. 
Maghembe anasema kuwa katika kituo chake, vijana hao wanajishughulisha na shughuli za kilimo, shughuli ambayo inawaingizia kipato hivyo kuwaepusha mujiingiza kwenye vitendo vya uporaji na biashara haramu.
Naibu Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Embrosy Mwanguku anasema wakati sasa umefika kwa jamii nzima ya Watanzania kuondokana na tabia ya kuwanyooshea vidole watoto wa mitaani na wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Badala yake, Ofisa huyo wa Uhamiaji anatoa wito kwa jamii kuwasaidia watoto hawa kwa kuwa wanaweza kuwa nguvu kazi nzuri inayotegemewa kujenga taifa imara kwa ajili ya kizazi kijacho.
Kwa upande wake, Mwinjilisti wa Kanisa la KKKT, Usharika wa Ngulelo, Peter Kilaye, anasema vipaji vya vijana hao wa mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu vikiendelezwa, vinaweza kuchangia pato la taifa na hivyo kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla.
“Hakuna mtoto anayeweza kuwa kama debe tupu ambalo halina kitu. Kila mtu ameumbwa na kitu ambacho Mungu amempa ili akitumie kwa manufaa yake na jamii inayomzunguka,” FikraPevu imemkariri Mwinjilisti huyo akisema.
Dk. Kefa Omari wa Shirika la Wamisionari la Medical Missionaries Lifestyle Center for East Afrika), ambaye hivi karibuni alitembelea kituo hicho cha kulelea watoto cha taasisi ya Gola kwa lengo la kutoa msaada wa kitabibu kwa vijana hao, ikiwa ni pamoja na kuwapatia dawa ya kuondoa sumu mwilini inayotokana na dawa za kulevya, alitoa wito kwa vijana hao kuzingatia kanuni bora za afya kwa kupata lishe bora, kuzingatia mazoezi, unywaji maji ya kutosha na kutenga muda wa kupumzika kwa ajili ya afya zao.
Baadhi ya vijana hao wanaolelewa katika kituo hicho cha Gola kilichoko maeneo ya Arumeru, Kenedy Njenga na Francis Oni, kwa nyakati tofauti wamekaririwa na FikraPevu wakisema zamani kabla ya kufikishwa katika kituo hicho, walikuwa wakijihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya.
Hata hivyo, kwa sasa wanasema wameamua kuachana na matumizi ya dawa hizo, hali ambayo imerejesha afya zao katika hali ya kawaida kiasi cha kuweza sasa kushiriki katika shughuli za kijamii, kama vile kilimo cha mazao mbalimbali na bustani za mboga na matunda. 
Kituo hicho cha Gola cha mkoani Arusha na vituo vingine kama hivyo nchini, vinaweza kuwa vituo vya mfano wa kubaini vipaji vya watoto hao wa mitaani na wengine wanaoishi katika mazingira magumu ambao hadi sasa wamekosa msaada wa kuondolewa katika maisha hayo hatarishi.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU