TUSHIRIKIANE KUPUNGUZA WATOTO MITAANI.

SIKU zinavyozidi kwenda tatizo la watoto wa mitaani linaota mizizi na huku juhudi za kulimaliza zikishindikana. Kumekuwa na watoto wengi wanaozunguka barabarani bila kuhofia usalama wao kwani wengi wao hupenda kusimamama katika makutano ya barabara kuu. Mbali na ugumu wa maisha kuwa chanzo cha watoto wa mitaani, pia ukosefu wa elimu ya uzazi wa mpango kwa wanaume na wanawake pamoja na uvivu wa kufanya kazi vimechangia kwa kiasi kikubwa tatizo hili.

           
Ongezeko la watoto wa mitaani linatokana na wazazi kushindwa kumudu familia kwani huwa na watoto wengi zaidi ya uwezo wao kuwalea. Ikiwa elimu ya uzazi wa mpango itatolewa kwa uwazi, wataelewa umuhimu wa kuzaa watoto wanaoweza kuwalea na kumaliza tatizo hili baadaye. Hata hivyo jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na watoto wengi wa mitaani kwa kuwa watu wengi hudhani maisha ya Jijini ni rahisi hata ukikosa shughuli ya kufanya tofauti na hali halisi.

Watoto wengi wanakuwa na maisha magumu, hawapati haki ya elimu hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi wanaowatuma kuomba. Ukipita maeneo mengi ya jiji hasa sehemu za makutano ya barabara utawakuta wakiomba lakini hii hatari kwao kwakuwa inaweza kuwasababishia matatizo pindi gari inapoondoka bila wao kujua. Kwa upande wa  watoto wa kike wanapokuwa mitaani hubakwa na kusababishiwa maumivu, mimba zisizotarajiwa na wakati mwingine hata kuachiwa magojwa ya kuambukizwa.

Watoto wa kiume wanaingiliwa kinyume na maumbile na wanasababishiwa maumivu makali na hata baadhi yao wanaendelea na tabia hiyo wanapokuwa wakubwa na kusababisha ongezeko kubwa la wanaume mashoga. Watoto wengi ninaokutana nao na kuwauliza hujibu kuwa wanatumwa na wazazi wao kuomba kwa kuwa wazazi huona aibu kusimama barabarani, kwani husemwa na wapita njia. Hata hivyo Taasisi mbalimbali zimejitaidi kuanzisha vituo mbalimbali vya kulelea watoto wa mitaani lakini bado havijakidhi mahitaji kwa kuwa idadi ya watoto inazidi kuongezeka siku hadi siku.

Ongezeko hili limekuwa ni tatizo kwa kuwa limekuwa kero kila kona ya jiji la Dar es Salaam huku wengine wakijihusiha na wizi wa mifukoni. Naishauri serikali kutoa elimu ya uzazi wa mpango ili kudhibiti idadi ya watoto wanaozaliwa katika familia zisizo na uwezo wa kuwalea. Pia serikali iwajengee uwezo wanaondesha vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwatafutia shule wasome na kuwatoa katika mazingira ambayo ni hatari kwao, na hata kama ikiwezekana serikali iweke sheria kali kwa watu wote wanaowatelekeza watoto bila kuwa na matatizo yoyote.

Na ikiwezeka serikali iwakamate watoto wote na kuwarudisha  walipotoka kwani kuna baadhi yao hutoroka kwao bila kujua wataishi wapi hali inayosababishwa na ugumu wa maisha. Hata hivyo Taasisi binafsi zianzishe vituo vya watoto wa mitaani ili kupunguza idadi ya watoto  wa mitaani na wanapokuwa wanawachukua waakikishe watoto hao wanapa elimu bora ili kizazi kijacho kisiwe na watoto wa mitaani, kwani wazazi wao watakuwa na uwezo wa kuwalea bila matatizo yoyote. Pia ikiwezekana watoto hao wanapochukuliwa waulizwe wametokea wapi na ikiwezeka warudishwe huko kwa sababu karibia kila mkoa una vituo vya watoto wa mitaani.

Aidha kuna wananchi ambao wana uwezo mkubwa wa kifedha wajitolee angalau kuchukua watoto wa mitaani wawili ili  kupunguza idadi yao mitaani lakini sio kutegemea tu serikali kwa kila jambo. Na kwa upande wa viongozi wa serikali angalau kila kiongozi angejitahidi kuchukua hata watoto watatu na kuwasomesha kwa kuwa naamini kwamba viongozi wetu wana uwezo mkubwa wa kuwasidia watoto nwa mitaani hasa katika kupata elimu bora.  Pia Makampuni mbalimbali yazidi kutoa mchango kwenye vituo vya watoto wa mitaani ili kuwapa motisha  hao waliojitolea kufungua vituo hivyo, kwani bila kusaidiana itawawia vigumu  kuwalea peke yao.

Watoto hao ni wetu sote, hivyo ni jukumu la kila mtu kuhakikisha analitafutia ufumbuzi wa kudumu ili kunusuru Taifa la kesho.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU