ONGEZEKO LA WATOTO WA MITAANI NA OMBAOMBA

IDADI kubwa ya watoto wadogo wanaoishi katika mazingira hatarishi inaweza kutishia amani nchini, ikiwa hatua za makusudi hazitachukuliwa kuokoa kizazi hicho.
Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi wa Mradi wa Tuwalee  FHI 360, Levina Kikoyo mara baada ya kufanyika kwa uzinduzi wa ripoti iliyofadhiliwa na Shirika la Misaada na Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID) ya utafiti uliofanyika kuanzia Februari mwaka huu juu ya kasi ya ongezeko la watoto hao.
Alisema kwa sasa taifa lina watoto wengi walio katika mazingira hatarishi kutokana na kutopata elimu na kusababisha pia ongezeko la watoto hao mitaani, hali itakayozaa wimbi la ujambazi na uhalifu nchini katika siku za mbele.
       
Alieleza kuwa kwa sasa zaidi ya watoto milioni 2 wanaishi katika mazingira hatarishi na hata wengine kujihusisha na shughuli za kuomba mitaani, na hivyo kuzua hofu ya matokeo mabaya kwa taifa.
Alisema utafiti wao waliofanya katika wilaya zote tatu za Mkoa wa Dar es Salaam wamebaini asilimia 90 ya ombaomba watoto wamezaliwa katika familia iliyokuwa na ombaomba mmoja au wawili.
Naye ofisa mwandamizi wa ulinzi wa watoto kutoka FHI 360, Judith Masasi, alisema kuwa ongezeko kubwa la watoto kuomba na wazazi wao linatoa changamoto kwa wadau wote wanaofanya kazi za kuhakikisha watoto wote wanaishi katika mazingira salama, kuweka mikakati endelevu ya kuwahudumia.
Alisema suala hilo linahitaji mipango maalumu ya dhati ikijumuisha wadau mbalimbali ili kuwepo na mfumo unaolenga kuwasaidia watoto hao kwa kuimarisha familia na jamii kwa ujumla.
              
“Ripoti hii pia imeonyesha kuwa asilimia 75 ya watoto waliohojiwa wapo kati ya umri wa miaka sita hadi 14 na asilimia 64 yao wamesema wangependa kujiunga tena na masomo,” alisema Masasi.
Alisema zipo jitihada zilizofanywa hadi sasa katika kuhakikisha watoto hao na wazazi au walezi wanasaidiwa na kuondolewa katika hali ya kukosa fursa na haki zao, lakini matokeo yameshindwa kutatua matatizo yaliyochangia ongezeko la watoto wa mitaani.
Awali akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Victoria Bura alisema kuwa serikali imekuwa ikijadiliana na taasisi mbalimbali ili kujua hatua madhubuti ya kuchukua katika kudhibiti wimbi la watoto hawa.

Comments

Popular posts from this blog

WATOTO WA MITAANI NA JINSI YA KUWASAIDIA

AYA ZA BIBLIA KUHUSU WATU WENYE ULEMAVU

TUWAKUMBUKE WATOTO WENYE MTINDIO WA UBONGO KAMA KUNDI MAALUM KATIKA JAMII ZETU